September 22, 2014

  • IRINGA MAANDAMANO YA CHADEMA YAPIGWA STOP, WARUHUSIWA KUFANYA MKUTANO WA HADHARA


    IRINGA MAANDAMANO YA CHADEMA YAPIGWA STOP, WARUHUSIWA KUFANYA MKUTANO WA HADHARA


    Frank Nyalusi, Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini
    CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Iringa Mjini jana limeshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi "tumepokea zuio kali kutoka jeshi la Polisi."

    Akizungumza Jana Nyalusi alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo ikiwa ni kuitikia wito uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano ya amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.

    Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika mtaa wenye machinga wengi maarufu kama magari mabovu, Kitanzini.

    "Kwahiyo tutakuwa na mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na mimi mwenyewe na viongozi wengine wa chama kuanzia saa 10 jioni, hivisasa tupo kwenye kikao cha kamati tendaji kuweka maazimio kuhusu zuio la maandamano hayo ya amani" alisema kwa njia ya simu.

    Akieleza kushangazwa na maamuzi ya Polisi ya kuzuia maandamano yao, Nyalusi alisema maazimio yatakayofikiwa katika kikao hicho atayatangaza kwenye mkutano huo.

    Wakati Chadema wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka katika chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.

    Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema "nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni."

    Alisema watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka kufanya kwa kuzingatia sheria vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia.

    Alisema mji wa Iringa upo shwari na kwamba jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kukabiliana na hali yoyote ile itakayoonekana inataka kuhatarisha amani.

    Aliwataka wakazi wa Iringa kuendelea na shughuli zao kama kawaida na pale watakahisi au kusikia kuna mtu au kikundi chochote cha watu kinataka kufanya jambo linaloweza kuhatarisha usalama wao na wa mali zao, watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa Polisi.
     
    kwa hisani ya francis godwin blog


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.