September 18, 2014

  • Baraza la ushindani: Tutumieni kwa manufaa ya Taifa na ustawi wa uchumi nchini


    Baraza la ushindani: Tutumieni kwa manufaa ya Taifa na ustawi wa uchumi nchini
    Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi wa Baraza la Ushindani (FCT) Bw. Nzinyangwa Mchany akiwaeleza waandishi wa Habari (Hawapo pichani)Kuhusu majukumu ya Baraza hilo na kutoa wito kwa wananchi kulitumia baraza hilo pale itakapohitajika kwa madhumuni ya ustawi wa uchumi wa Jamii na Taifa kwa ujumla.wakati wa Mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Sheria wa Baraza hilo Bi. Hafsa Said. Hassan Silayo MAELEZO.

    Na Hassan Silayo-MAELEZO

    Baraza la ushindani limewataka wananchi kulitumia Baraza hili kwa manufaa ya Taifa na ustawi wa uchumi nchini.

    Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Uchumi Nzinyangwa Mchany wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam. "Baraza la ushindani lipo kwa ajili ya watu wote hivyo wananchi hawana budi kulitumia kwa manufaa ya Taifa". Alisema Nzinyangwa.

    Aidha, Nzinyangwa alisema kuwa baraza la ushindani ni chombo maalum cha rufaa za maamuzi au amri za Tume ya Ushindani na mamlaka za udhibiti kwenye sekta za Miundombinu,huduma za maji na nishati.

    Pia alisema kuwa kesi zinazosikilizwa kwenye baraza zinahakikisha uzingatiaji wa misingi ya udhibiti ili kuleta umakini katika kusimamia sekta husika na ushindani wa haki sokoni.

    Akizungumzia kuhusu rufaa zilizowahi kusikilizwa na baraza hilo Nzinyangwa alisema kuwa rufaa zinazosikilizwa na baraza la Ushindani zimegawanyika katika makundi manne.

    Akizitaja rufaa hizo Nzinyangwa alisema ni rufaa kati ya mtoa huduma na mlaji, hii ni pale mlaji anapopewa huduma mbovu au hafifu kwenye sekta inayosimamiwa na mdhibiti kama maji, simu, nishati ya umeme pamoja na bidhaa za mafuta ya nishati.

    Pia kuna aina ya rufaa kati ya wauzaji wawili wa bidhaa ya aina moja ama mbadala wake kama kampuni za usafirisha au kampuni za simu ambapo shauri hili litapelekwa kwa mdhibiti wa sekta husika na iwapo upande mmoja hautaridhika na uamuzi unahaki ya kuombea rufaa uamuzi huo kwenye baraza la ushindani.

    Akiendelea kutaja Rufaa hizo Nzinyangwa alisema kuwa pia ipo rufaa kati ya mtoa huduma na mdhibiti wa sekta na hii ni pale mdhibiti wa sekta anapoandaa utaratibu wa kudhibiti sekta na ikiwa mdau anaona utaratibu huo hautoshelezi au haukufuata sheria mdau ana haki ya kuwasilisha malalamiko kwenye chombo kilichotoa uamuzi huo.

    Pia mdau wa soko anaweza kukata rufaa kwenye Baraza la ushindani ikiwa tume ya ushindani imetoa amri kwenye soko au kutunga kanuni Fulani juu ya utaratibu kuhusu usimamizi wa ushindani kwenye soko ambao mdau anaona uamuzi huo haukuwa sawa.

    Tume ya ushindani ina jukumu la kukataza uzalishaji na uuzaji wa bidhaa bandia sokoni,katika jukumu hilo maamuzi hayo yanaweza kukatiwa rufaa na mdau kwenye Baraza la Ushindani


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.