May 14, 2014

  • MZIGO MZITO ULIOMSHINDA KOFI ANNAN WAMSHINDA BRAHIMI

     
     
     
     
    Na Mwandishi Maalum
    Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa masikitiko makubwa ametangaza kukubali kwake kujiuzuru kwa mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa
    na Muungano wa nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi aliyekuwa akisimamia mazungumzo ya kutafuta Amani nchini Syria. Akitangaza mbele ya waandishi wa habari kuhusu kujiuzulu kwa Bw. Brahimi ambaye pia alikuwapo kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema mwanadiplomasia huyo mzoefu ataachia wadhifa wake ifikapo Mei 31.
    Huku hali ikiendelea kuwa ya sitofahamu na kutokuwapo kwa mwanga wowote wa maridhiano au kumalizwa kwa mgogoro nchini Syria, Ban Ki moon anasema kujiuzuru kwa Mwakilishi huyo maaulum ni pigo kwa watu wa Syria na ni kielelezo cha kushindwa kwa Umoja wa Mataifa.
    Bw. Brahimi aliteuliwa Agosti 17 mwaka 2012 akichukua nafasi ya Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliyeteuliwa mwanzoni kabisa mwa mgogoro huo na baada ya muda mfupi alitangaza kujiuzuru.
    Bw. Brahimi ameelezea masikitiko ya kuondoka kwake huku akiiacha Syria katika hali mbaya. Lakini akaelezea matumaini yake kuwa, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon, atafanya kila ubinadamu iwezekanavyo kufanya kazi na Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, pande zinazopigana nchini Syria pamoja na nchi jirani kumaliza mgogoro huo.
    " Nina hakika kuwa mgogoro huu utamalizika, lakini wadau wote wanatakiwa kulizingatia hili je ni vifo vingapi zaidi, ni uharibifu kiasi gani utokee kabla Syria haijawa Syria mpya" akasema Bw. Brahimi.
    Naye Katibu Mkuu akasema, kwa miaka miwili Bw. Brahimi amejitahidi sana kumaliza ukatili na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria. " Kwa kweli, mwanadiplomasia huyo mwenye asili ya Algeria ( 80). Amepitia changamoto nyingi kuanzia taifa lenyewe ya Syria, eneo la Mashariki ya Kati na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na ambayo imegawanyika vibaya juu ya namna ya kuumaliza mgogoro wa Syria. Takwimu zinaonyesha kwamba tangu mgogoro wa Syria ulipoanza mwezi Marchi 2011 zaidi ya watu 100,000 wamepoteza maisha na zaidi ya 680,000 wakiwa ni majeruhi.
    Aidha zaidi ya watu milioni 9.3 wanahitaji misaada ya kibinadamu ndani ya Syria, ikiwa ni pamoja na watu milioni 6.5 ambao ni wakimbizi wa ndani. Vile vile mgogoro huo wa Syria umesababisha kuwapo kwa wakimbizi zaidi ya milioni 2.5 ambao wametafuta hifadhi katika nchi jirani. Katika kumuelezea zaidi Bw. Brahimi, Katibu Mkuu amemtaja kama mmoja ya watu mashuhuri wanaotambuliwa duniani na mwana-diplomasia mwenye uwezo mkubwa na mtetezi mkubwa wa Misingi na Katiba ya Umoja wa Mataifa.
    Ban Ki moon akaongeza kuwa, kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa na ambalo ndilo limepewa dhamana ya kusimamia usalama na amani. Pamoja na nchi zenye ushawishi mkubwa kuhusu hali ya Syria kushindwa kumpatia ushirikiano wa kutosha Bw. Brahimi, ni kushindwa kwetu sote.
    Katibu Mkuu amesema ataendelea kutegemea uzoefu na ushauri wa Bw. Brahimi na kwamba kutoka na kazi nzuri aliyoifanya anastahili kupumzika. Na akazitaka pande zote zinazohusika na mgogoro wa Syria pamoja na mataifa yenye ushawishi kwenye mgogoro huo , kujiangalia upya na kutafakari nini kinachotakiwa kufanywa ili kuwarejeshea matumaini wananchi wa Syria.

    Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiwa na   Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa  na Muungano wa nchi za Kiarabu Bw. Lakhdar Brahimi, wakati    Katibu Mkuu alipotanganza  mbele ya waandishi wa habari  kuhusu kujiuzuru kwa Bw.  Brahimi kama msuluhishaji  mkuu wa mgogoro wa  Syria.  Katibu Mkuu Ban Ki Moon alisema amekubali kwa masikikitiko makubwa  kujiuzuru kwa Bw. Brahimi na hasa katika kipindi hiki ambacho  hakujapatikana muafaka katika mustakabari mzima wa mgogoro wa Syria.     Bw. Lakhdar Brahimi mwanadiplomasia mzoefu na anaye heshimika katika Jumuiya ya Kimataifa anakuwa  mwanadiplomasia wa pili kuachia ngazi akitanguliwa na  Katibu Mkuu  Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan aliyekuwa  mjumbe wa kwanza kupewa  dhamana ya kutafuta suluhu ya mgogogoro wa Syria.
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.