September 05, 2014

  • Mtoa hukumu ya Okwi, taabani kitandani


    Mtoa hukumu ya Okwi, taabani kitandani
    Mshambuliaji mpya wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi.

    WAKATI Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitarajia kukutana kesho Jumamosi na kutoa uamuzi kuhusiana na suala la mshambuliaji Emmanuel Okwi akipige Simba au abaki Yanga, hofu imetawala.
    Hofu imetawala hasa kwa wadau upande wa Klabu ya Simba kwamba wanaweza wasimpate Okwi kwa kuwa idadi ya wajumbe wa kamati hiyo itapungua kutoka watu saba hadi sita.
    Hali hiyo inatokana na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Hussein Mwamba ambaye ni shabiki mkubwa wa Simba kuwa taabani kitandani, imefahamika.
    Wajumbe wengine sita watakaokutana na itikadi zao za ushabiki kwenye mabano ni Richard Sinamtwa-Mwenyekiti (Yanga), Moses Kaluwa-Makamu Mwenyekiti (Simba), Iman Madega (Yanga), Zacharia Hans Poppe (Simba), Phillemon Ntahilaja (Yanga) na Abdul Sauko (Yanga).
    Hofu ya wadau wa Simba inaonekana ni kwenye idadi ya wajumbe na itikadi zao za ushabiki hasa kama suala hilo litakuwa gumu na kufikia kwenye kupiga kura kwa kuinua mikono juu, maana yake Simba itapata 2 na Yanga 4. Hivyo kwenye hukumu ya mwisho Simba italala.
    Taarifa za uhakika zilizolifikia paparazi, zinaeleza kuwa, Mwamba yu taabani kitandani kwa ndugu yake katika moja ya vitongoji vya jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya kutoka hospitali.
    "Kwa kweli Mwamba ni mgonjwa sana, alikuwa hawezi hata kuzungumza na tunasikia uchungu sana maana rafiki anaumwa. Alilazwa hospitali kwa takribani wiki tatu, sasa yuko kwa ndugu yake (anataja eneo la kitongoji)," alisema rafiki wa karibu.
    Hivyo hakuna matumaini ya Mwamba ambaye ni Katibu wa Chama cha Soka Singida (SFA) kuhudhuria kikao hicho cha kesho.Yanga inaendelea kusisitiza Okwi ni mchezaji wake halali ingawa ilipeleka barua ya kuvunja naye mkataba kwa TFF.
    Msisitizo ni kwamba mkataba haujavunjwa na wana mkataba naye.
    Simba wamekuwa wakisisitiza Yanga imevunja naye mkataba ndiyo maana walikubali ombi lake arejee Simba ili kulinda kipaji chake kwa kumpa mkataba mfupi wa miezi sita.
    Okwi amekuwa akidai Yanga haikutaka acheze msimu ujao, hali ambayo ingeua kipaji chake ndiyo maana aliamua kuomba Simba impe nafasi ya kucheza, nayo ikakubali na kumchomoa beki Donald Musoti na kumpa yeye moja ya nafasi tano za wageni.
    Kutokana na hali hiyo kuwa na mkanganyiko na Yanga kuamua kushitaki TFF huku ikidai itasonga hadi Fifa au kwenye Mahakama ya Soka (CAS), kamati hiyo ya sheria, maadili na hadhi za wachezaji ndiyo inategemea kuanza kutoa mwanga wa usahihi wa jambo hilo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.