Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania yatakayofanyika tarehe 4 na 5 Septemba 2014 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa hiyo katika Ofisi ya Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mwenyekiti wa Maandalizi ya Bodi hiyo Mhandisi Bakari Mwinyiwiwa, amesema maadhimisho hayo yatakayobeba kauli mbiu isemayo "jukumu la wahandisi kwenye utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa" yana dhana ya kuionyesha jamii kile ambacho wahandisi wa kitanzania wanaweza kufanya katika kuleta maendeleo ya nchi.
Pia maadhimisho hayo yana lengo la kuwatia moyo wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea uhandisi ili wafanye vizuri zaidi katika masomo yao na kuwafanya vijana washawishike kusomea taaluma ya uhandisi.Alisema Mhandisi Mwinyiwiwa
"Siku hii ni kubwa kwa kuwa hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kuwa na wataalamu wahandisi hivyo ni muhimu kwa wananchi, wahandisi na wanafunzi wanaochukua taaluma ya Uhandisi kushiriki ili kupata mawazo chanya katika taaluma hii", alisisitiza Mhandisi Mwinyiwiwa
Mhandisi Mwinyiwiwa alifafanua kuwa baadhi ya shughuli zinazotarajiwa kufanywa siku hiyo ni pamoja na majadiliano ya kitaaluma, kiapo cha wahandisi wataalamu, maonyesho mbalimbali ya kiufundi na biashara pamoja na tuzo kwa wahandisi wahitimu na taasisi za uhandisi nchini wa mwaka 2013/2014.
Aidha Mhandisi Mwinyiwiwa alibainisha kuwa maonyesho hayo yanatarajiwa kushirikisha vyuo na taasisi mbalimbali zikiwemo Chuo cha Uhandisi naTeknolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam (CoET), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) , Chuo Kikuu cha Uhandisi na Teknolojia St Joseph (SJUIT) na Chuo cha Ardhi (ARU).
Washiriki wengine ni Makandarasi mbalimbali, Kampuni za ushauri wa kihandisi, mashirika na kampuni ya kibiashara na taasisi za utafiti.Aliongeza mhandisi Mwinyiwiwa.
Nae Msajili Mkuu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi Mhandisi Steven Mlote amezitaka Taasisi, Mashirika na wafanyabiashara mbalimbali kutumia fursa hiyo kuonyesha bidhaa zao katika maadhimisho ya siku hizo mbili ili kudhihirishia umma juu ya kazi wanazozifanya kwa maendeleo ya nchi.
Kwa mara ya kwanza siku ya wahandisi Tanzania ilizinduliwa tarehe 13 Januari 2003 na Rais mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa.
0 comments:
Post a Comment