June 20, 2014

  • WAATHIRIKA WA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI SASA KUSAIDIWA KUPITIA AKAUNTI MAALUM



    WAATHIRIKA WA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI SASA KUSAIDIWA KUPITIA AKAUNTI MAALUM
    Picha na 1Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya Ilala Bw. Raymond Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu kuanzishwa kwa mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara wa soko la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto kwa lengo la kurejesha hali ya maisha waliyokuwa nayo hapo awali. 

    Picha na 2Mmoja wa waanzilishi wa mfuko wa kuwasaidia waathirika wa moto soko la Mchikichini ambaye pia ni Meneja wa Vituo vya mizigo vya nchi kavu wa Kampuni ya AZAM Bw. Raymond Adolph akieleza namna walivyoguswa na tukio la moto lililotokea katika soko hilo na kuwaomba watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
    Picha na 4Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Mchikichini Bw. Jumanne Kongolo akiongea na waandishi wa habari  kuishukuru serikali na wananchi waliojitokeza kufungua mfuko wa kuwasaidia waathirika wa moto katika soko hilo. 
    Picha na 5Baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto wakifuatilia masuala mbalimbali ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mfuko wa kuwasaidia wafanyabiashara hao.

    Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
    MFUKO WA KUWASIDIA WAFANYABIASHARA WALIOATHIRIWA NA MOTO SOKO LA MCHIKICHINI WAANZISHWA.
     
    Na Aron Msigwa – MAELEZO,  Dar es salaam.
     
    Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wamejitokeza kuanzisha mfuko maaluum wa kuwasaidia wafanyabiashara wapatao 5700  wa soko la Mchikichini walioathiriwa na janga la moto  lililotokea usiku wa kuamkia tarehe 12 mwezi  huu eneo la Karume,jijini Dar es salaam.
     
    Akaunti hiyo maalum inayojulikana kwa jina la Mkono wa Pole Chinga 2014 imefunguliwa katika Benki ya CRDB Tawi la Lumumba ili kuwawezesha wadau mbalimbali wanaoguswa na tukio hilo kutoa mkono wa pole kupitia akaunti namba 0152270491300.
     
    Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye pia ni mkuu wa wilaya Ilala Bw. Raymond Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam amesema kuwa mfuko huo unalenga kurejesha hali ya maisha waliyokuwa nayo wafanyabiashara hao hapo awali kabla ya kuungua kwa vibanda na bidhaa zao. 
     
    Amesema akaunti hiyo itasimamiwa kwa pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, wadau waanzilishi na wafanyabishara walioathirika.
     
    "Tumeanzisha akaunti hii kutokana na wananchi kuguswa na tukio hili kwa kuonesha nia thabiti ya kutaka kutoa mkono wa pole kwa waathirika wa janga hili, nachoweza kusema jambo hili tumeliwekea utaratibu na tutaliendesha kwa uwazi mkubwa kwa kushirikiana na wahusika wa tukio" amesema Bw. Raymond. 
     
    Aidha, amefafanua kuwa serikali kupitia Manispaa ya Ilala ambayo soko hilo liko chini yake itahakikisha inaboresha hali ya miundombinu katika soko hilo zikiwemo barabara za kuwezesha magari na vifaa vya uokoaji kupita wakati wa majanga ya moto huku akiwataka  wafanyabiashara hao kutojenga na kuzuia maeneo ya barabara katika soko hilo. 
     
     Mmoja wa waanzilishi wa mfuko huo ambaye pia ni Meneja wa Vituo vya mizigo vya nchi kavu vya vya Kampuni ya AZAM Raymond Adolph ameeleza kuwa yeye kama mfanyakazi na wafanyakazi wengine wameguswa na tukio la moto lililotokea katika soko hilo na kufafanua kuwa kiasi cha fedha kitakachopatikana kitakabidhiwa kwa walengwa kwa uwazi huku akiwaomba watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
     
    "Akaunti hii tuliyoifungua itakuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kiasi tutakachopata tutakikabidhi kwa wahusika kwa uwazi na tunawaomba watanzania wajitokeze ili kwa pamoja tuwasaidie ndugu zetu hawa waliopata matatizo" amesisitiza.
     
    Kwa upande wake mwenyekiti wa wafanyabiashara hao ambaye pia aliathiriwa na moto huo Bw. Jumanne Kongolo ameeleza ameishukuru serikali na wananchi waliojitokeza kufungua mfuko huo kwa lengo la kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika na moto huo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.