June 14, 2014

  • MTOTO ATESWA MIAKA MIWILI


    MTOTO ATESWA MIAKA MIWILI
    merina                    moi 0ecc9
    Mtoto Merina Mathayo (15) amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (Moi) Muhimbili Dar es Salaam, baada ya kuteswa na kujeruhiwa kichwani kwa kipigo maeneo mbalimbali ya mwili na bosi wake kwa miaka miwili..Merina amelazwa Moi baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya Mwananyamala alipokuwa amelazwa awali, kutokana na majeraha hayo ambayo yanadaiwa kusababishwa kung'atwa kwa meno na kupigwa kwa vitu mbalimbali mara kwa mara.Akizungumza kwa shida Merina alisema amekuwa katika hali ya mateso tangu mwaka 2012, kwani bosi wake huyo ambaye anamtaja kuwa ni mwanasheria mkazi wa Boko amekuwa na tabia ya kumpiga na vitu mbalimbali akiwa amemvua nguo.
    "Haya marejaha niliyonayo sasa, alinipiga kwa fagio la chooni akamalizia na jagi, kisha akapiga simu nyumbani kwetu huko Ishozi Kiziba mkoani Kagera, akawaambia wazazi kwamba amenikung'uta kichwa kwa sababu mimi ni mjeuri," alieleza Merina na kuongeza:
    "Mara kwa mara amekuwa na tabia ya kunivua nguo na kunipiga na chochote anachojisikia, ananing'ata kisha ananipakaza chumvi kwenye majeraha," alisema Merina.
    "Mara zote anazonipiga huniambia kwamba sijafanya kazi vizuri au sijamaliza kuzifanya, lakini mwanaye ambaye ninamlea huwa analia sana akimwambia usimpige dada, mwachie," alisema Merina.
    Alibainisha kwamba dada wa mtuhumiwa huyo anayemtaja kwa jina la Josephine Rwechungura, baada ya kukerwa na vitendo hivyo vya kikatili alivyotendewa ndiye alimpeleka hospitali.
    Merina alisema kuwa hajawahi kupewa malipo yake na bosi huyo ambaye walikubaliana mshahara wa Sh40,000 na Sh20,000 hutumwa kwa wazazi wake na zilizobaki alikuwa anadai kwamba anamwekea.
    Moi yajitolea kumsaidia
    Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema wamempokea Merina juzi saa 7.00 usiku, baada ya kuelezwa historia ya majeraha yake uongozi umeguswa na kujitolea kugharimia matibabu yake.
    "Madaktari wamesema kwamba anatakiwa kufanyiwa kipimo kikubwa cha CTS can ambacho kitawezesha kujua majeraha aliyonayo yana ukubwa gani, gharama zake ni Sh250,000 ambazo Moi itazitoa na kumpatia matibabu bure," alisema Mvungi.
    Awali Katibu Afya wa Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala alisema Merina alipelekwa hospitalini hapo Juni 11 mwaka huu na msamaria mwema, baada ya madaktari kumwona walibaini kwamba ana majeraha makubwa kichwani."Walimwona ana maumivu makali pia majeraha kichwani, kwa kiwango cha hospitali yetu hatuwezi kutibu kichwa, kwa sababu anatakiwa kuchunguzwa kwa kina kiwango cha majeraha yake kwa vifaa vya kitaalamu, hivyo tumempa rufaa ya Muhimbili," alisema.
    Polisi
    Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alikiri kupokea taarifa ya tukio hilo, ambapo mtuhumiwa ametoweka nyumbani kwake hivyo anasakwa, polisi wanaoshughulikia ni wa Kituo cha Wazo.
    "Taarifa hiyo tunayo kwa sasa tunamsaka mtuhumiwa huyo maana ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, kwa sasa hatuwezi kumtaja jina lake," alisema.
    Tukio hili ni mfululizo wa matukio ya kusisimua yanayozidi kuibuliwa ndani ya jamii katika kipindi cha mwezi sasa, likiwamo lililohusisha mtoto Nasra Mvungi (marehemu) aliyekutwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka mitatu huko mkoani Morogoro.
    Watu watatu akiwamo baba mzazi wa Nasra, Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe pamoja na wanandoa Mariam Said (38) ambaye ni mama yake mkubwa na mumewe Mtonga Omar (30), wakazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha Ndege, wameshtakiwa wakidaiwa kumtesa na kumsababishia kifo mtoto huyo.
    Mtoto huyo aligundulika akiwa katika hali ya mateso, kwani alikutwa akiwa mchafu na ilithibitika kwamba kwa mara ya mwisho aliogeshwa Julai mwaka jana, huku viungo vya mwili wake mikono na mgongo vikiwa vimepinda.
    Tukio lingine linahusu mtumishi wa kazi za ndani Yusta Kashinde, anayedaiwa kung'atwa sehemu mbalimbali za mwili na kuunguzwa na pasi na bosi wake Amina Maige, hivyo kumsababishia majeraha makubwa. Tayari Maige amefikishwa mahakamani kwa tukio hilo.
    CHANZO mwananchi


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.