June 08, 2014

  • Mvutano Mkali Bunge, Mahakama



    Mvutano Mkali Bunge, Mahakama
    Kitendo cha Mahakama kufungua milango kwa mawaziri na wabunge kufunguliwa mashtaka kutokana na kauli watakazozitoa bungeni ambazo ni kinyume cha Katiba na Sheria, kimeonekana kuwachanganya viongozi hao ambao wamesema kuwa wanalindwa na sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

    Wamesema licha ya kuwa kazi ya Mahakama ni kutafsiri sheria, Bunge kutunga na Serikali kusimamia sheria, nchi nyingi duniani wabunge wake wana kinga na hawashtakiwi kwa kauli watakazozitoa bungeni.

    Kauli za wabunge hao zimekuja ikiwa imepita siku moja tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa msimamo huo wakati ikitoa uamuzi wa pingamizi la awali katika kesi ya kikatiba iliyokuwa ikimkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, lililowasilishwa na Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (DAG, George Masaju.

    Kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013 ilifunguliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), dhidi ya Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), aliyeunganishwa kama mlalamikiwa wa pili.

    Mahakama Kuu katika uamuzi wake juzi ilikubaliana na baadhi ya hoja za mawakili wa utetezi (Serikali) na kuitupilia mbali kesi hiyo, lakini ikatamka kuwa wabunge na mawaziri wanaweza kushtakiwa kwa kauli au jambo walilolitamka bungeni, linalokiuka sheria na haki za binadamu.

    Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, Naibu Spika Job Ndugai alisema, "Mahakama ikisema, imesema licha ya kuwa Katiba inaeleza wazi kuwa Bunge lipo huru."

    Alisema kuwa suala hilo linaweza kuwekwa sawa katika Katiba Mpya ambayo mjadala wake utaendelea Agosti mwaka huu.

    "Nchi nyingi duniani wabunge wana kinga kwa kauli zao watakazozitoa bungeni. Kama hapa kwetu tumeamua hivyo ni sawa tu, ila mashtaka yatakuwa mengi kwelikweli," alisema Ndugai.

    Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla (CCM) alisema, "Sidhani kama tafsiri hii ni sahihi sana kwa sababu wabunge wanalindwa na Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge."

    Kigwangalla alisema sheria hiyo ipo wazi kwamba mbunge akizungumza lugha isiyofaa mtu ambaye anataka kuchukulia hatua anatakiwa kuiandika barua Ofisi ya Bunge.

    "Barua hiyo itakwenda kwa Spika wa Bunge na kama akiridhika atalipeleka suala hilo katika Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge ambayo inaweza kumwita mlalamikaji ili kumsikiliza," alisema Kigwangalla.

    Alifafanua kuwa sheria hiyo haijawahi kufanyiwa marekebisho na kama mahakama imetoa tafsiri hiyo maana yake ni kwamba kesi za wabunge zitarundikana mahakamani.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.