June 08, 2014

  • UNYANYAPAA KWA WAGONJWA WA HIV NI TATIZO MKOANI TABORA



    UNYANYAPAA KWA WAGONJWA WA HIV NI TATIZO MKOANI TABORA
     Meneja wa program ya (EMTCT) katika shirika la EGPAF
    mkoa wa  Tabora Alphaxard Lwitakubi akifafanua jambo kuhusu hali
    halisi ya huduma ya EMTCT mbele ya waandishi wa habari ofisi za EGPAF mkoani Tabora Picha na habari na Allan Ntana wa Globu ya Jamii Tabora
    *Wajawazito hufukuzwa na kutelekezwa na waume zao. 
    *Waomba sheria kali zitumike kuwalinda.  
    *Hali ya kijiografia ni tatizo kuhudhuria tiba kliniki. 

    "WAJAWAZITO tunapenda kupima afya zetu ili kujua hali tulizonazo, lakini hali ya unyanyapaa kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya ukimwi hususani kinamama tunaonyonyesha tunalazimika kujificha kwa kuogopa kutengwa na familia na jamii kwa ujumla".......

    Hiyo ni kauli ya kina mama wajawazito na walioambukizwa virusi vya (VVU) katika wilaya za Kaliua na Uyui mkoani Tabora wakati walipokuwa wakiongea na mwandishi wa makala hii. 

    Hayo yamebainika baada ya ujumbe wa Shirika la EGPAF linalofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia mashirika yake ya USAID na CDC ukiongozwa na Afisa Mawasiliano Anna Sawaki kutembelea wilaya hizo ili kujua ukubwa wa tatizo la unyanyapaa, huduma na changamoto zilizopo. Aidha hatua hiyo pia katika kuendeleza harakati za kuhamasisha elimu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi toka kwa mama kwenda kwa mtoto. 
    Ujumbe huo ulishuhudia akinamama wanaopata huduma ya afya katika vituo mbalimbali wakielezea adha wanazopata hasa baada ya kugundulika wameambukiza virusi vya ukimwi. 
    Akina mama tuliowakuta katika Zahanati ya kata ya Usinge wilaya ya Kaliua, kituo cha afya Misheni Kaliua na kituo cha afya Ilolangulu katika kata ya Ilolangulu wilayani Uyui walibainisha ukweli huo kuwa baadhi yao wamekuwa wakipata shida kwa ndugu na jamaa zao na mara kadhaa wametengwa na familia zao kwa kigezo cha kuambukizwa virusi vya ukimwi. 
    Walisema baadhi yao hadi sasa wamefukuzwa na waume zao huku wengine wakidai waume wamewatelekeza na watoto. 
    Hata hivyo walieleza kuwa wanapenda kuendelea kutumia dawa za kumkinga mtoto na virusi vya ukimwi akiwa tumboni kwa wenye ujauzito lakini vitendo vya kunyooshewa vidole na ndugu zao au jamii, ikiwemo kufukuzwa na wenza imekuwa ikiwatia hofu kubwa kuhudhuria Zahanati na Vituo vya afya kupata huduma. 
    Wakielezea zaidi adha wanazokutana nazo walisema wanapenda huduma zinazotolewa lakini wanashindwa kujiweka wazi kutokana na hali ya unyanyapaa wa jamii na ndugu ambao wamekuwa wakiwatenga kama hawastahili kuishi. 
     Aidha waliongeza kuwa wanakuwa katika wakati mgumu hasa wanapotaka kwenda kupata dawa ya kupunguza makali ya VVU katika vituo vya afya kwani mara kadhaa wanalazimika kufanya siri na wenza wao ili ndugu na jamii wasijue. 
     Ndugu wanapojua hali zao wanawatenga na kuwanyanyapaa kwa kiasi kikubwa huku jamii iliyoko mitaani ikiwanyooshea vidole pindi wanapokuwa katika shughuli za kijamii ama za kuwaingizia kipato na wanapenda kuwa mabalozi kuhusiana na afya zao lakini wanaamua kujificha kukwepa adha hiyo, waliongeza. 
     Hata hivyo wameiomba serikali itupie macho suala hilo japokuwa ipo sheria inayowalinda waathirika lakini sheria hiyo haijaonyesha makali yake. 
    Hali ya kijiografia yawa kikwazo. Kwa upande mwingine walisema kukosekana kwao kuhudhuria kliniki wanalazimika kukatisha huduma hiyo kutokana na hali ya kijiografia kwa mkoa wa Tabora kwani yapo maeneo ambayo usafiri ni wa shida hasa kutokana na vituo vya kutolea huduma kuwa mbali. 
     Walisema yapo maeneo ambayo kipindi cha kiangazi usafiri hupatikana lakini kipindi cha masika hali huwa mbaya kwani usafiri haufiki maeneo wanayoishi kutokana na hali ya barabara kadhaa kutopitika. Waliishauri serikali kuangalia namna ya kuboresha miundombinu ya barabara ili huduma kama hiyo na nyinginezo ziwafikie wote na wazipate kwa wakati. Watoa huduma wanazungumziaje. 
     Mganga wa zahanati ya kata ya Usinge wilaya ya Kaliua Abdulaziz Adinan Kishangagha alikiri kuwepo tatizo la unyanyapaa japokuwa wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa jamii. Alisema licha ya hali hiyo kuwepo bado kuna wagonjwa ambao wamebainika kuambukizwa wamekuwa wakikatisha tiba na wengine wakijificha kwa hofu ya kunyanyapaliwa.
     "Kero ya unyanyapaa kwa wagonjwa imekuwa ni kubwa sana kiasi cha wagonjwa kuamua kujificha…..ikiwemo ukosefu wa vifaa tiba vya wagonjwa ni vitu ambavyo vinaathiri utendaji wetu."alisema. 
     Upimaji wa VVU kwa wajawazito waongezeka. Meneja wa program ya (EMTCT) katika shirika la EGPAF mkoa wa Tabora Alphaxard Lwitakubi anasema mwitikio wa upimaji wa virusi wa ukimwi kwa wajawazito kutoka mwezi februari 2006 hadi machi 2014 hali ya maambukizi imepungua toka asilimia 3 hadi asilimia 2.3. 
     Lwitakubi alifafanua wajawazito walioweka wazi kipindi cha 2006 hadi 2014 hali zao ni asilimia 63 wakati waliopata dawa za kuzuia maambukizi ya (VVU) toka kwa mama kwenda kwa mtoto imepanda toka asilimia 26 hadi 97 kwa mwaka 2014. 
     Aidha alisema watoto waliozaliwa na kinamama wenye VVU na kusajiliwa katika huduma za RCH ni 143 ambao wote waliochukuwa damu ni asilimia 100 na waliogudulika na VVU ni 5 sawa na asilimia 3.4 na wote wameanzishiwa dawa na vituo vya (PMTCT) meneja alisema vimeongezeka kutoka vituo 5 katika mwaka 2006 hadi 44 mwaka 2014. 
     Changamoto zilizopo. Akizungumzia changamoto alisema ushirikiano mdogo kwa upande wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na upimaji (VVU). 
     Alitaja changamoto nyingine ni kinamama wajawazito kujifungulia nyumbani kwa wakunga wa jadi, waliogundulika na (VVU) kupotea na kutorudi vituoni kutokana na unyanyapaa unaoendelea. Aidha aliongeza changamoto ya walezi na wazazi kutopeleka katika vituo watoto waliogundulika wana maambukizi ya (VVU) wapate dawa za ARV, hali ya jiografia ya mkoa wa Tabora yapo maeneo ambayo vituo viko mbali, upungufu wa dawa na vifaa tiba.
     Namna watakavyokabiliana na changamoto hizo. Hata hivyo Lwitakubi alibainisha wamejipanga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma zote za (MHCH), uagizaji wa dawa,vigaa tiba na vitendanishi.
     Aliongeza mipango mingine ni kuendelea kuomba watumishi toka wizara ya afya na ustawi wa jamii,kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHW) na kutenga bajeti ya kununua mashine za kupima kinga ya mwili CD4. 
     Mratibu msaidizi wa afya ya uzazi na mtoto anasemaje. Mratibu msaidizi huduma za Afya ya uzazi na mtoto Audrey Bakuza wa hospitali ya rufaa Kitete mkoani Tabora anazungumzia huduma ya Elimination of Mother To Child Transmission of HIV (EMTCT). 
     Bakuza alisema kabla ya hapo huduma hiyo ilijulikana kama Prevention of Mother To Child Transmission of HIV (PMTCT) iliyolenga kupunguza maambukizi ya VVU toka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto lakini sasa mkakati uliopo ni kutokomeza kabisa au kuzuia maambukizi. 
     Bakuza anasema kwa huduma hiyo inajulikana kama huduma mpya ya Elimination of Mother To Child Transmission of HIV (EMTCT) mjamzito kabla na baada ya kujifungua. 
     Alisema katika jitihada za kufanikisha mkakati huo wamekuwa wakishirikiana na EGPAF, ambapo Wizara ya Afya na ustawi wa jamii ilitoa maelekezo vituo vya afya kutoa elimu kwa mama mjamzito namna anavyoweza kujikinga mwenyewe na namna anavyoweza kumkinga mtoto. Changamoto wanazokutana nazo. 
     Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo Bakuza alisema wazazi wengi hasa akina mama na wenza wao wanaogopa kujitokeza kupima afya na elimu duni ya wenza wao kugoma kuongozana kuja kupima afya imekuwa tatizo kwa watoa huduma. 
     Alitaja changamoto zingine ni upungufu wa watoa huduma za mama na mtoto , uhaba wa dawa kwa baadhi ya maeneo, ubadilishaji namba za kadi kwa waliogundulika kuambukizwa. 
    Mafunzo kwa watoa huduma. 
     Bakuza anasema kuhusu mafunzo kwa watoa huduma zaidi ya robo tatu wamepatiwa mafunzo hayo na robo iliyobaki watapatiwa mafunzo kabla ya mwezi Julai mwaka 2014. 
     Afisa wa mawasiliano ya shirika la EGPAF Anna Sawaki alisema bado lipo tatizo katika mwitikio wa huduma za Elimination of Mother To Child Transmission of HIV (EMTCT) hasa kwa upande wa wanaume na jamii, ipo haja kuongeza nguvu ya kutafuta ufumbuzi wa kuduma kufikia malengo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.