June 10, 2014

  • Imebainika kuwa Dar Ndio Mkoa Ghali Kuliko Yote Tanzania



    Imebainika kuwa Dar Ndio Mkoa Ghali Kuliko Yote Tanzania
    WAKATI Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) awamu ya kwanza, unapanga kuongeza nauli za daladala kwa wakazi wa Dar es Salaam ili kukabiliana na tatizo sugu la foleni, taarifa ya matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara, zimeonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam, ndio mahali ghali zaidi nchini.

    Gazeti hili lilichapisha kwa mara ya kwanza habari kuwa Dart awamu ya kwanza ikianza, nauli ya basi kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwenda na kurudi vituo vikubwa vikiwemo vya Kariakoo, Posta na Kimara, itapanda kutoka nauli ya chini ya Sh 400 ya sasa mpaka Sh 700 na 800 kwa ruti moja.

    Taarifa hiyo ya kaya, ambayo Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo, alisema jana kuwa ni ya awali tu na taarifa yenyewe itatolewa hivi karibuni, imeonesha kuwa mkoa huo ndio wenye gharama kubwa ya maisha.

    "Mfano, bei za vyakula ni kubwa jijini Dar es Salaam, ukilinganisha na maeneo ya vijijini, hivyo gharama ya kulipia mlo wa mtu mmoja kwa siku ni ya juu kwa jiji la Dar es Salaam," imeeleza taarifa hiyo. Hata hivyo, taarifa hiyo inayoangalia viashiria vya umasikini kwa kuchambua mahitaji muhimu ya mwanadamu, iliyo katika tovuti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), imefafanua pia kuwa mkoa huo ndio wenye idadi ndogo ya masikini nchini.

    "Kaya za jijini Dar es Salaam zina kiwango kidogo cha umasikini wa mahitaji ya msingi, ukilinganisha na kaya zinazoishi katika miji mingine na maeneo ya vijijini. "Ukijumuisha watu wote wenye umaskini wa mahitaji ya msingi nchini, inakadiriwa asilimia mbili (1.5) wanaishi jijini Dar es Salaam, asilimia 14.4 wanaishi maeneo mengine ya mijini na asilimia 84.1 wanaishi vijijini," alisema.

    Kuhusu umiliki wa nyumba, taarifa hiyo imeeleza kuwa wakati asilimia 76 ya kaya nchini zinamiliki nyumba wanazoishi, jijini Dar es Salaam ni asilimia 37 tu ya kaya zinazomiliki nyumba wanazoishi na kaya zilizobakia, asilimia 63 ni wapangaji.

    "Uwiano huu (wa nyumba za kuishi) ni mkubwa katika maeneo ya vijijini, ambako asilimia 89 ya kaya wanamiliki nyumba wanazoishi, huku umiliki wa nyumba katika maeneo mengine ya mijini ukiwa asilimia 58," imeeleza taarifa hiyo.

    Taarifa hiyo ingawa ni ya awali, lakini iliyochambua vema umasikini kwa kuangalia mahitaji ya lazima na mahitaji muhimu ya Watanzania, imebaini hadhi za nyumba wanazoishi Watanzania kwa ujumla imekuwa ikiboreka.

    "Asilimia 66 ya kaya mwaka 2011/12 zinaishi katika nyumba zenye paa za kisasa ukilinganisha na asilimia 55 ya kaya mwaka 2007.

    "Vivyo hivyo, asilimia 73 ya kaya zinaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa kuta imara mwaka 2011/12 ukilinganisha na asilimia 33 za mwaka 2007," imeeleza taarifa hiyo.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuta imara zinajumuisha zilizojengwa kwa mawe, matofali ya saruji, au matofali ya kuchoma na paa za kisasa ni zile zilizojengwa kwa mabati. Katika mawasiliano, taarifa hiyo imeeleza kuwa umiliki wa simu za mkononi unatofautiana sana kwa maeneo.

    "Wakati kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo mengine ya mjini na asilimia 88 ya kaya za Dar es Salaam, zinamiliki angalau simu moja ya mkononi, ni asilimia 45 tu ya kaya za maeneo ya vijijini zinazomiliki angalau simu moja ya mkononi," ilieleza taarifa hiyo.

    Taarifa hiyo, imeeleza kuwa mstari wa masikini, unaonesha masikini wa mahitaji ya msingi nchini na ambaye yupo katika mstari wa umasikini wa mahitaji yamsingi ni anayepata Sh 36,482 kwa mwezi, wakati maskini wa chakula ni anayepata Sh 26,085 kwa mwezi.

    "Kwa kutumia takwimu hizi, matokeo yanaonesha kuwa zaidi ya robo (asilimia 28.2) ya watu wote waishio Tanzania Bara, wako chini ya mstari wa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi na asilimia 9.7 ya watu wote wapo chini ya mstari wa umaskini wa chakula," imeeleza taarifa hiyo.

    Hata hivyo, taarifa hiyo imeonesha kuwa kiwango cha umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara kimekuwa kikipungua kwani mwaka 2007, kilikuwa asilimia 33.6.

    "Matokeo ya awali yanaonesha kupungua kwa kiwango cha umaskini kati ya 2007 na 2011/12. Upimaji wa mwenendo wa umaskini utaainishwa kwenye Ripoti Kuu ya Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, 2011/12," imeeleza taarifa hiyo.

    Hesabu zilizopigwa na wataalamu wa takwimu walioandaa taarifa hiyo, zimebainisha kuwa kunahitajika Sh bilioni 103.3 kwa mwezi (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.2 kwa mwaka), ili kuondoa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa watu waishio chini ya mstari wa umaskini Tanzania Bara.

    Pia imeelezwa kuwa kama watu wote wangegawanywa katika makundi matano yanayolingana na ukubwa wa matumizi yao kuanzia wa chini hadi wa juu, matumizi ya watu wa kundi la juu (matajiri sana) ni mara nne (4) ya matumizi ya kundi la chini (maskini sana) kwa Tanzania Bara.

    Katika elimu, taarifa hizo zimeonesha kuwa asilimia 20 ya Watanzania (Tanzania Bara) wenye umri wa miaka 15 au zaidi hawana elimu ambapo kwa mwaka 2007 ilikuwa ni asilimia 19.

    Aidha, uandikishwaji katika shule za msingi kwa watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 13, umeshuka na kufikia asilimia 78 kwa mwaka 2011/12 ikilinganishwa na asilimia 84 katika mwaka 2007. Hata hivyo kwa upande wa sekondari, uandikishaji umetajwa kuongezeka kutoka asilimia 15, mwaka 2007 mpaka 29, mwaka 2012.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.