June 10, 2014

  • Mnigeria mwingine anaswa na ‘unga’ Dar



    Mnigeria mwingine anaswa na 'unga' Dar

    Raia wa Nigeria, Anthony Ifeanyichukwa Okafor (52), amekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akidaiwa kumeza kete 100 za dawa za kulevya aina ya cocaine ambazo thamani yake bado haijafahamika.

    Tukio hilo limetokea takribani siku 22 baada ya raia mwingine wa Nigeria, Olabisi Ibidun Cole (65) kuvunja rekodi ya umri wa watu wanaokamatwa wakiwa na dawa za kulevya katika uwanja huo.

    Cole alikamatwa Jumatatu ya Mei 19, mwaka huu saa tisa alasiri akijiandaa kwenda Paris, Ufaransa kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, akiwa amemeza kete 82 aina ya heroini zilizokuwa zimefungwa kwenye karatasi zinazofanana na ganda la sigara, ambazo si rahisi kuonekana katika mitambo.

    Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa (pichani) alisema jana kuwa mtuhumiwa huyo alidai kuwa amefika nchini kumfuata rafiki yake wa kike aliyekutana naye Hong Kong, China na baadaye Douala, Cameroon.

    Nzowa alisema mtuhumiwa huyo alisema rafiki yake huyo wa Tanzania ni mpenzi wake na wako pamoja katika kazi hiyo.

    Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege, Hamisi Selemani alisema wauzaji wa dawa hizo siku hizi wamegundua mtindo mpya wa kuwatumia watu wazima ili wasigundulike kutokana na mwonekano wao.

    "Muda si mrefu ametoa kete mbili na kufikisha 100 na anavyoonekana bado ataendelea kutoa nyingine, tunaye hapa tunaendelea kumhoji," alisema Selemani na kuongeza kuwa alikamatwa Jumamosi iliyopita saa saba usiku akitokea Douala kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.

    Alisema alikamatwa baada ya maofisa wa uwanja huo kufuatilia mwenendo wa taarifa zake za safari na kuangalia nchi alizokuwa akisafiri.

    "Tunapomkagua mtu tunaangalia taarifa zake jinsi alivyosafiri, tunaangalia nchi zenye matukio ya kuuza na kuchukua dawa za kulevya," alisema na kuongeza:

    "Watu wanaofanya biashara hii ni wajanja sana na hujiamini kama huyu Mnigeria, alituambia tufanye kazi yetu yeye yupo fresh, hana kitu na tulipomfanyia uchunguzi wa kina tukabaini amemeza dawa za kulevya.

    "Huyu alitumia ujanja wa kwenda nchini Cameroon kwa kuwa nchi ile haitengenezi dawa hizo hivyo alipitia huko aweze kuja hapa nchini asigundulike," alisema.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.