June 25, 2014

  • MIRADI YA MCA-T YANUFAISHA SERIKALI YA MUUNGANO


    MIRADI YA MCA-T YANUFAISHA SERIKALI YA MUUNGANO
    4-ujenzi-wa-wa-Davis-Corner-Vituka-Jet-Corner-ukiendelea-1
    Na Mwandishi wetu- Hazina

    Maendeleo ya nchi yoyote duniani yanatokana na rasilimali zilizopo katika nchi husika na mipango madhubuti iliyojiwekea.
    Serikali imeanzisha sera za uchumi na programu za maendeleo kwa lengo la kuwawezesha watu na kukuza  uchumi nchini.

    Sera hizo pamoja na mikakati  mbalimbali ilitungwa kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi Watanzania  ili wamiliki, waendeshe na wanufaike na uchumi  wao kufuatia Dira ya Maendeleo iliyojiwekea ya 2025.
    Kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia Tanzania (MCA-T) ambao ni moja ya programu za kimuungano, kumekuwa na mafanikio ambayo yametokana na utekelezaji mzuri wa  miradi na kuwa na faida kwa pande zote za Muungano. 
    Miradi iliyotekelezwa chini ya programu hii ilihusu shughuli 13 za kuendeleza miundombinu katika sekta 3 tofauti ambazo ni usafirishaji, nishati na maji.
    Miradi hiyo ilifadhiliwa na Serikali ya Marekani na kutekelezwa na Serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia makubaliano ambayo yalisimamiwa na Millenium Challenge Corporation   (MCC) Shirika la Umma lililoanzishwa kusimamia Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCA).
    Makubaliano ya Msaada (Compact) kwa Tanzania ya jumla ya Dola za Marekani milioni 698.136, ndio yaliyoweka misingi ya ufadhili wa miradi iliyoibuliwa katika pande   zote mbili za Muungano na Timu Maalumu ya Maandalizi ya Miradi iliyojumuisha watu wa pande zote mbili, yaani Zanzibar  na Tanganyika.
    Makubaliano haya ya msaada yalisainiwa tarehe 17 Februari  mwaka 2008 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Marekani wa kipindi hicho George W. Bushi. Compact iliweka kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa miradi yote ambapo kipindi hiki kiliishia tarehe 17 Septemba  mwaka 2013. Tarehe ya kuanza rasmi utekelezaji wa miradi (Entry into Force), baada ya kipindi cha maandalizi ya miradi kukamilika, ilikuwa Septemba 17, 2008, ambapo makubaliano ya taratibu za utekezaji (Program Implementation Agreement -PIA) yalisainiwa. Kwa mujibu wa taratibu za utekelezaji (yaani PIA) kulikuwa na siku 120 za kufunga shughuli zote za compact, baada ya kipindi cha miaka 5 ya utekelezaji kukamilika, ambapo siku rasmi ya kufungwa kwa shughuli zote za Compact ilikuwa Januari 15, 2014.
    Sekta hizi za usafirishaji, nishati na maji ni miongoni mwa sekta zilizopo katika mipango ya maendeleo ya taifa ambapo zaidi ya hiyo zimo sekta ya elimu, afya, uvuvi, usafirishaji, sheria, ardhi na utalii.
    Taarifa za utekelezaji wa miradi baada ya mkataba kufungwa zinaleta faraja kwa Watanzania ambao wana matumaini na Serikali yao ambayo ndio inayosimamia miradi mbalimbali nchini.
    Sekta ya usafirishaji nchini ni miongoni mwa sekta ambayo inasimamiwa chini ya muungano ambapo imesaidia kutengamanisha ushindani, kuimarisha soko na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kukuza biashara, utalii na uwekezaji wa kigeni, na imechangia mapato ya serikali.
    Hii imewezekana kutokana na kupitia utelekezaji wa programu nyingi za maendeleo ya usafirishaji, matengenezo na marekebisho yanayolenga kuendeleza utoaji wa mfumo wa usafirishaji salama, wenye ufanisi na gharama nafuu nchini.
    Miradi ya sekta ya usafirishaji chini ya Compact ilijumuisha shughuli za ujenzi wa barabara tano kubwa Tanzania Bara zenye jumla ya kilometa 438 na barabara 5 za vijijini Pemba Kaskazini zenye jumla ya kilometa 35. Aidha kulikuwepo na mradi wa uboreshaji wa kiwanja kimoja cha ndege .
    Shughuli hiyo ilihusisha barabara mbalimbali ili kuhakikisha nchi nzima imekuwa na utengamano kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa urahisi zaidi.
    Kwa kuzingatia umuhimu huo, miradi iliyokamilika ni   Bararaba ya Tanga hadi Horohoro yenye umbali wa km 65, Barabara ya Namtumbo hadi Songea yenye umbali wa km. 71.4, Barabara ya Peramiho hadi Mbinga yenye umbali wa km 78, na vipande viwili katika barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga yenye urefu wa km 224 yaani Tunduma mpaka Ikana km 63.7 na Ikana hadi Laela km 64.3
    Nyingine ni barabara tano za Pemba vijijini zenye umbali wa km 35 ambazo ni Mzambarauni Takao hadi Pandani Finya, Mzambarauni Karimu hadi Mapofu, Bahanasa Daya hadi Makongeni Mtambwe, Chwele hadi Kojani, Kipangani hadi Kangagani na uboreshaji wa uwanja wa Ndege Kisiwani Mafia.
    Ujenzi wa kipande cha barabara cha Laela- Sumbawanga yenye umbali wa km 95.3 ulikuwa mgumu, wenye changamoto nzito na bado unaendelea kujengwa.
    Barabara ya Tanga hadi Horohoro na Uwanja wa ndege wa kisiwa cha Mafia vilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Aprili, 2013 na Oktoba, 2013.
    Barabara tano za Pemba vijijini zilizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar,Dk. Ali Mohammed Shein Machi, 2014.  Miradi mingine ya barabara pia iko tayari kwa uzinduzi.
    Miradi ya Sekta ya Nishati ilijumuisha shughuli  nne ambayo ni  Mradi wa kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini ya bahari ambao shughuli zake ni pamoja na Kebo ya umeme chini ya bahari kutoka RAS Kiromoni Tegeta, Dar es Salaam hadi RAS Fumba Unguja, Zanzibar. Uunganishaji umeme wa nguzo kutoka kituo cha Ubungo mpaka RAS  Kiromoni, Tanzania Bara na kutoka RAS Fumba hadi kituo cha mtoni Zanzibar. Vilevile  Kukarabati vituo  vinne  vya  kupoozea umeme yaani Ubungo na Tegeta kwa Bara na RAS Fumba na mtoni kwa Zanzibar.
    Pia kulikuwepo mradi wa ukarabati wa njia kuu za kupitisha umeme na upanuzi wa mtandao wa umeme katika mikoa 10 kwa Tanzania Bara ambayo ni Tanga, Morogoro, Iringa, Mbeya, Njombe, Mwanza, Geita, Dodoma, Manyara na Kigoma.
    Vilevile   Ukarabati wa vituo 24 vya kupoozea umeme ukijumuisha vituo 4 vya mradi wa kupeleka umeme Zanzibar kupitia chini ya bahari. 
    Kwa kuzingatia umuhimu wa umeme kwa maendeleo endelevu ya nchi na watu wake, programu ya umeme wa jua Kigoma ilizingatiwa ili kuwarahisishia wananchi shughuli zao za kila siku. Mradi wa umeme wa jua uliibuliwa baada ya kukwama kwa mradi wa umeme wa maji katika mto Malagarasi, kutokana na sababu za utunzaji wa mazingira.
    Miradi ya uunganishaji na usambazaji nguzo za umeme iliyohusisha vituo vya Dodoma, Manyara, Mwanza na Geita ilizunduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Machi 2013 na Septemba 2013.
    Na mradi wa kupeleka umeme Zanzibar kupitia  chini ya bahari pamoja na vituo vyake ilizinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Machi, 2013.
    Dhamira hii ya kuwawezesha Watanzania wengi kupata huduma za nishati za kisasa na endelevu, kuboresha matumizi ya teknolojia za nishati, kujenga uwezo, uhamasishaji jamii, ujasiriamali na uraghibishi kwa ajili ya sera saidizi kunaendelea kupunguza umasikini na kuboresha uhifadhi wa mazingira nchini.
    Kwa kuongozwa na Dira ya Maendeleo ya 2025, Tanzania inakusudia kutokomeza kabisa ufukara na kupata maisha bora kwa watu wote ifikapo mwaka 2025.
    Ili kuwa na maendeleo endelevu ni lazima kuwepo na upataji wa maji kwa usawa na haki, uwezo wa usimamizi wa maji, na utunzaji bora wa mifumo ya maji ikiwa ni pamoja na usafi, matumizi ya teknologia zinazozingatia mazingira, na gharama ya maji yenye tija.
    Miradi ya sekta ya maji iliyofanyika chini ya ufadhili huu ilikuwa ni pamoja na upanuzi wa Mtambo wa kusafisha maji wa eneo la Ruvu chini, ukarabati na upanuzi  wa mfumo wa maji kwa manispaa ya Morogoro unaosimamiwa na MORUWASA na upunguzaji wa maji yanayopotea katika mfumo wa maji Dar es salaam, unaosimamiwa na DAWASA/DAWASCO.
    Kazi kubwa za miradi ya sekta ya maji zimekamilika.  Mtambo mpya wa maji wa Ruvu Chini umeanza kazi na sasa unasukuma maji safi kwenda Dar es Salaam lakini kutokukamilika  kwa bomba kubwa la kuleta maji katika matanki ya akiba yaliyoko maeneo ya chuo kikuu cha Dar es salaam ni kikwazo kinachosababisha kushindwa kutumia uwezo wote wa mtambo mpya.
    Mtambo mpya wa kusafisha maji wa Mambogo, Morogoro uko katika hatua za mwisho  na utaanza kufanya kazi Juni 2014, na pampu mpya za kusafisha maji za Mafiga, Morogoro zinafanya kazi.
    Usimamizi wa rasilimali ya maji, ugavi wa maji safi na salama na mfumo mzuri wa maji taka ni mojawapo ya vipaumbele kwenye Dira ya maendeleo ya Taifa.
    Miradi hii yote iliyotekelezwa na Serikali inatokana na umahiri wa usimamizi wa Wizara ya Fedha ambayo ndio kiunganishi cha wizara zote ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Jemedari wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
    Kwa kuzingatia uzoefu wa zaidi ya Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanganyika, Miaka Hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar na Miaka Hamsini ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Serikali ya Watu wa Zanzibar, Watanzania wote tuna kila sababu ya kuulinda kuutunza na kuuenzi Muungano huo ambao unajali misingi ya utu, uhuru, haki, usawa, udugu, amani, umoja na mshikamano katika nyanja zote za maisha yetu.
    Hivyo, "Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha" kauli mbiu hii ya muungano iwe ni taswira inayoonesha utaifa wetu kwa nusu karne mpaka sasa na uendelee kudumu zaidi ya miaka hamsini ijayo ambapo dhamira hiyo inadhihirishwa kwa wimbo wa taifa unaobeba dhana ya watanzania wote kuheshimu utaifa wetu kama watoto wa  Tanzania na Afrika.
    chanzo:full shangwe.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.