Rais wa shirikisho la soka Tanzania, TFF, Jamal Malinzi ( wa kwanza kushoto) akiongea na waandishi wa habari leo mchana
UCHAGUZI wa Simba sc kwa asilimia kubwa utaweza kufanyika juni 29 kama ilivyopangwa kufuatia kauli ya Rais wa shirikisho la soka Tanzania, TFF, Jamal Emil Malinzi akimpongeza rais wa Simba Ismail Aden Rage kwa kufanya juhudi ya kufanya mazungumzo na shirikisho hilo.
Akuzungumza mchana huu na waandishi wa habari katika ofisi za shirikisho hilo zilizopo katikati ya jiji, Posta, Rais Malinzi amesema tangu alipotangaza kusimamisha uchaguzi huo jumapili iliyopita na kuwataka Simba kuunda kamati ya maadili itakayosikiliza masuala yao ya maadili, rais wa Simba, Aden Rage amekuwa akiwasiliana naye vizuri na kwa heshima ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Malinzi alisema wamekuwa na maelewano mazuri na Rage, hivyo ana imani ufumbuzi utapatikana .
Maneno ya Malinzi yanatoa imani kuwa yeye na Rage wameshafikia hatua nzuri na bila shaka uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.
"Nimpongeze sana mwenyekiti wa klabu ya Simba pamoja na kamati yake ya utendaji, kuanzia siku ya jumapili hadi leo hii tumekuwa tukiwasiliana kwa karibu sana, katika hali ya maelewano, heshima kubwa". Alisema Malinzi mchana huu.
"Na niseme tu kwamba leo mgombea mmoja ambaye kamati ya uchaguzi ilimuondoa katika uchaguzi, sina haja ya kutaja majina hapa, alileta rufaa yake, leo saa nane mchana kamati ya rufaa inakaa". Aliongeza Malinzi.
Malinzi alisisitiza kuwa baada ya zoezi la leo la kusikiliza rufaa kukamilika, mazungumzo yataendelea baina ya TFF na Simba kwa ajili ya ustawi wa soka la nchi hii.
"Baada ya hapo, vyovyote vile itakavyokuwa baada ya zoezi ya leo, mazungumzo yataendelea baina ya TFF na klabu ya Simba, ni imani yetu kwamba kwa ajili ya ustawi wa mpira wa nchi hii, kwa maana yoyote ile, tunaamini ufumbuzi utapatikana".
"Sasa ni ufumbuzi gani utapatikana, siwezi kuuzungumzia sasa hivi, mimi nimeruhusu kwa maana ya shirikisho kwamba kikao kifanyike leo cha kamati ya rufaa ya uchaguzi".
"Na baada ya hapo, mazungumzo yataendelea kuweza kuona ni kwa namna gani tutaweza kuwa katika hali nzuri ambayo itaweza kuwasaidia ndugu zetu wa Simba wakaendeleza ustawi wa klabu yao". Alisema Malinzi".
Mgombea aliyeenguliwa kwa mara ya pili na kamati ya uchaguzi wa Simba chini ya mwenyekiti wake, Wakili Damas Daniel Ndumbaro, Bwana Michael Richard Wambura amekata rufaa kupinga maamuzi hayo kwa mara nyingine.
Kamati ya Ndumbaro ilimuondoa tena Wambura kwa madai kuwa baada ya kurudishwa katika uchaguzi na kamati ya rufani ya TFF chini ya mwenyekiti wake, Wakili Julius Mutabazi Lugaziya aliongea maneno ambayo ni kampeni kwenye vyombo vya habari wakati zoezi la kampeni bado halijaanza.
0 comments:
Post a Comment