June 01, 2014

  • Mhadhiri UDSM Ndio Rais Mpya wa Malawi



    Mhadhiri UDSM Ndio Rais Mpya wa Malawi
    Kwa ushindi wa Profesa Mutharika katika kiti cha urais wa Malawi, anaongeza idadi ya jamii ya wasomi waliopitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ama wakiwa wahadhiri au wanafunzi, kwani alifundisha chuoni hapo mwishoni mwa miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970.

    Nje ya kazi za uhadhiri, Profesa Mutharika aliyebobea katika masuala ya sheria ambaye pia ni mwanasiasa mzoefu na mashuhuri, ameshika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Sheria, Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, nafasi aliyoishika hadi anaingia katika uchaguzi mkuu hivi karibuni.

    Mbali ya Profesa Mutharika, wasomi wengine waliopitia UDSM na kufanikiwa katika ulingo wa kisiasa na hata kuwa marais au viongozi waandamizi katika nchi zao ni Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa zamani wa Zaire (sasa DRC) Laurent Desire-Kabila.

    Aidha, Makamu wa Rais wa zamani wa Uganda, Eriya Kategaya alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama ilivyo kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Sudan, John Garang.

    Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa Sheria na Katiba, naye alisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama ilivyo kwa Mawaziri wakuu watatu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.

    Getrude Mongella, Rais wa zamani wa Bunge la Afrika ambaye pia alishika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake Duniani uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

    Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa sasa wa Tanzania,naye amesoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

    Watu wengine mashuhuri waliosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni pamoja na mwanasheria Mkuu wa Kenya, Dk Willy Mutunga na Donald Kaberuka, Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambaye ni raia wa Rwanda.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.