Na Mwandishi Maalum, New York
Malkia Maxima wa Uholanzi jana ( June 17) aliongoza majadiliano ya mkakati juu ya ujumuishi wa kifedha (Inclusive Financing) kama mojawapo ya misingi ya agenda ya Maendeleo baada ya 2015.
Malkia Maxima alishiriki katika majadiliaho hayo yaliyoitishwa na Wakilishi za Kudumu za Tanzania, Peru na Indonesia katika Umoja wa Mataifa.
Nchi hizi tatu zinaongoza mchakato wa kusukuma mbele agenda hiyo ya ujumuishi wa kifedha katika Umoja wa Mataifa. Pamoja na Malkia Maxima, ambaye ni Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ( UNSGSA) kuhusu mkakati huo wa ujumuishi wa Kifedha kwa maendeleo, majadiliano hayo pia yalihudhuriwa na Mabalozi 20 kutoka Wakilishi mbalimbali.
Inakadiriwa kwamba takriban theluthi moja ya wakazi wote duniani na ambao wengi wao ni maskini, wanaendesha maisha yao bila ya huduma za msingi za kifedha kama vile akiba, bima na mikopo na hivyo kurudisha nyuma kasi yao ya kujikomboa na umaskini na kujipatia maendeleo. Katika nafasi yake kama UNSGSA, Malkia Maxima amekuwa mstari wa mbele katika kuonyesha ni kwa jinsi gani suala la ujumuishi wa kifedha unavyoweza kuzisadia familia na wajasiriamali kuimarisha uzalishaji wa mapato, kusimamia mtitiriko wa fedha , kuwa na fursa za kuwekeza, kujipatia mali na kujijengea ujasiri wa kukabiliana na vikwazo mbalimbali katika uendeshaji wa maisha yao.
Ni kwa sababu hiyo Tanzania, Peru na Indonesi, zimeamua kusimamia mchakato huo hasa katika kipindi hiki ambacho Jumuiya ya Kimataifa inaendelea na majadiliano ya maandalizi ya agenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015.
Kwa lengo la kujenga ushawishi wa kuhakikisha kwamba jumuiya ya kimataifa, taasisi za fedha na wadau wengine wanaupa mchakato huo muhimu na kuwa moja wa agenda ya Maendeleo baada ya 2015 kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba watu maskini haawachwi nyuma katika eneo hilo muhimu kwa maendeleo.
Malkia Maxima wa Uholanzi akiongoza majadiliano kuhusu mchakato wa Ujumuishi wa Kifedha, mchango unaoongozwa na wenye-viti wenza watatu ambao ni wawakilishi wa kudumu wa Tanzania, Peru na Indonesia. Malkia Maxima ambaye ni Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu aliongoza majadiliano hayo kwa mwaliko wa wenyeviti wenza hao watatu.
Malkia Maxima wa Uholanzi akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti- wenza wa mchakato kuhusu ujumuishi wa kifedha kwa maendeleo, kutoka kushoto ni Balozi wa Peru Gustavo MezaCuadra, Malkia Maxima wa Uholanzi, Balozti Tuvako Manongi na Balozi wa Indonesia Desva Percaya
Washiriki wa Majadiliaho kuhusu Ujumuishi wa Kifedha wakiwa katika picha ya pamoja na Malkia Maxima, majadiliano hayo yalifanyika katika Makazi wa Muwakilishi wa Peru.
0 comments:
Post a Comment