June 01, 2014

  • HUDUMA YA MAJI MIJINI YAZIDI KUIMARIKA



    HUDUMA YA MAJI MIJINI YAZIDI KUIMARIKA
    maji-darKiwango cha utoaji huduma ya majisafi kwenye miji mikuu ya mikoa imeendelea kuimarika kutokana na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya majisafi katika mamlaka zote za maji za miji mikuu ya mikoa.

    Akisoma hutuba yake ya makadiri ya fedha ya mwaka 2014/2015, Waziri wa Maji Profesa Jumanne  Maghembe alisema, Hadi mwezi Machi, 2014 upatikanaji wa huduma ya maji kwenye mamlaka za maji 19 isipokuwa DAWASA na Mamlaka za miji minne ya Mikoa mipya imefikia wastani wa asilimia 86.
    Profesa Maghembe alisema, upatikanaji wa huduma ya maji kwa miji minne ya Mpanda, Njombe, Geita na Bariadi ni wastani wa asilimia 53.

    Aidha alisema, idadi ya wateja waliounganishwa kwenye mitandao ya majisafi mijini imeongezeka kutoka wateja 311,478 mwezi Machi, 2013 hadi kufikia wateja 336,898 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 8.
    Katika hatua nyingine, alisema uzalishaji wa majisafi kwa Mamlaka zote 23 za miji mikuu ya mikoa uliongezeka kutoka wastani wa lita milioni 348.76 kwa siku mwezi Machi 2013 hadi kufikia wastani wa lita milioni 376.07 mwezi Machi 2014.
    Akielezea upotevu wa maji, Waziri Maghembe alisema, Wastani wa upotevu wa maji (Non Revenue Water – NRW) kwenye mifumo ya usambazaji maji umefikia asilimia 38 tokana  na uchakavu wa miundombinu ya usambazaji wa maji na wizi wa maji.
    Aidha Profesa Maghembe alisema, makusanyo ya maduhuli yatokanayo na mauzo ya maji kwa mwezi kwa Mamlaka zote za maji mijini isipokuwa DAWASCO, yameongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 6.36 (kwa mwezi) mwezi Machi 2014 kutoka wastani wa shilingi bilioni 5.58, mwezi Machi 2013. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 14.
    Akielezea huduma ya majisafi jijini Dar es Salaam, Waziri Maghembe alisema, idadi ya wakazi wanaopata huduma ya majisafi sasa katika Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 68 kwa wastani wa saa tisa (9) kwa siku.
    Pia alisema, kati ya hao, asilimia 55 wanapata huduma ya maji kutoka kwenye mitandao ya mabomba na wanaobaki wanapata huduma ya maji kutoka kwenye visima, magati na huduma ya magari (water bowsers).
    Akitoa ahadi ya serikali kwa jiji la Dar es Salaam, Profesa maghembe alisema, "Lengo la Serikali ni kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 75 mwezi Juni, 2016". Aliahidi Prof. Maghembe.  
    Mahitaji ya maji kwa hivi sasa ni lita milioni 450 kwa siku ikilinganishwa na uwezo wa mitambo wa kuzalisha maji lita milioni 300 kwa siku. Hata hivyo, mwezi Machi 2014, uzalishaji wa maji ulishuka na kufikia wastani wa lita milioni 260 kwa siku.
    Upungufu huo wa uzalishaji unatokana na tatizo la kuharibika kwa mara kwa mara kwa mitambo ya kusukuma maji (pampu kubwa za Ruvu Juu), muda mrefu wa matengenezo, miundombinu chakavu na hitilafu za umeme.
    Profesa Maghembe aliomba Bunge limuidhinishie jumla ya shilingi 520,906,475,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2014/2015, ili Wizara iweze kutekeleza majukumu na malengo yaliyoelezwa katika hotuba hii.
    Aliezeza kuw kati ya fedha hizo, Matumizi ya Kawaida ni shilingi 30,899,443,000 ambapo shilingi 15,384,999,000 ni Mishahara ya Watumishi (PE), na shilingi 15,514,444,000 ni fedha za Matumizi Mengineyo (OC).
    Hivyo, Jumla ya Bajeti ya Maendeleo ni shilingi 490,007,032,000 ambapo kati ya fedha hizo shilingi 312,066,164,000 ni fedha za ndani na shilingi 177,940,868,000 ni fedha za nje.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.