Wazee kijiji cha Nyamihuu wakimpa baraka na kumpongeza mbunge Mgimwa kwa uchapa kazi wake |
Na Francis Godwin Blog
MBUNGE wa jimbo la Kalenga Bw Godfrey Mgimwa amesema atahakikisha anafanya kazi na vyama vyote vya siasa na kuwa kuwataka wananchi wa jimbo la Kalenga kuachana na makundi ya vyama vya siasa na kuunagana pamoja ili kufanikisha jimbo hilo kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
Mbali ya kuwataka kuachana na makundi ya kisiasa pia amewataka waliokuwa wagombea wa nafasi za ubunge katika uchaguzi mdogo kupitia CCM kuacha kujipitisha kwa sasa kwa wananchi na badala yake kusubiri uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya hadhara kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa kumchagua na leo katika kata ya Nzihi ,mbunge huyo alisema kuwa amelazimika kuomba ruhusa bungeni kwa spika ili kurudi kuwashukuru wananchi hao hasa kutokana na upendo mkubwa ambao wananchi wa jimbo hilo walionyesha kwake.
"Ndugu zangu nilianza kuzunguka katika baadhi ya maeneo na kutekeleza ahadi mbali mbali hata kabla ya kuapishwa rasmi bungeni ……na nitajitahidi kulingana na uwezo wangu ili kuona natimiza wajibu wangu kwenu na kamwe sitawaangusha ndani ya bunge na nje ya bunge"
Hivyo aliwataka wananchi kwa umoja wao kuendelea kumuombea afya njema ili kufanikisha kutimiza ndoto yake ya kufikisha maendeleo katika jimbo hilo ikiwa ni pamoja na kutimiza sehemu kubwa ya ahadi ambazo zilitolewa na marehemu Dr Wiliam Mgimwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo.
Kuhusu suala la kuyawezesha makundi mbali mbali Mbunge Mgimwa aliwataka wananchi kujiunga na vikundi vya VICOBA ili kuviwezesha vikundi hivyo kiuchumi zaidi badala ya kuwa mtu mmoja mmoja na kuwataka wazee pia kuanzisha umoja wao na kupeleka mahitaji yao katika ofisi yake.
"Kuna vikundi vya VICOBA ambavyo tayari vimeanzishwa na moja kati ya vikundi hivyo tayari nimechangia kiasi cha Tsh 500,000 na nitaendelea kuchangia na kuna eneo ambalo marehemu mbunge wetu aliyepita aliahidi kuchangia milioni 1 katika kikundi cha VICOBA Magubike nasema fedha hizo nitazitoa mimi "
Alisema kuwa tayari ameanza kupigania suala la umeme na maji katika vijiji vya jimbo la Kalenga bungeni na kuwa mawaziri wa wizara hizo wameahidi kulifanyia kazi na kuendelea kusaidia miradi hiyo mikubwa ambazo ndizo ahadi kubwa zaidi.
Awali wananchi wa kijiji cha Magubike walimpongeza mbunge huyo na kuwa katika historia ya jimbo la Kalenga hawajapata kuwa na mbunge mkweli na mchakakazi kama huyo na kurudi mapema zaidi kwa wananchi kuwashukuru na hivyo kumhakikishia kuwa hawana mpango wa kumchagua mbunge mwingine mwaka 2015 na kukiomba chama cha mapinduzi kumbariki kuendelea kuongoza jimbo hilo .
Kwa upande wake katibu mwenezi wa CCM wilaya ya Iringa Denis Lupala alisema kuwa utendaji kazi mzuri wa mbunge huo ndio ambao unakishawishi chama kuendelea kumpa ushirikiano zaidi na kuwa wananchi hawana sababu ya kubabaishwa na wapinzani ambao wameanza kujipitisha katika jimbo hilo.
0 comments:
Post a Comment