Mahakama kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi dhidi ya waziri mkuu, Mh. Mizengo Pinda iliyofunguliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu LHRC na chama cha wanasheria Tanganyika TLS kwa sababu hawana mamlaka kisheria ya kumshtaki. Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakih Jundu imetupiliwa mbali baada ya jopo hilo kukubaliana na hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju.Kituo cha sheria na haki za binadamu na TLS walimshtaki Waziri Mkuu Pinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kauli aliyoitoa bungeni Juni 20 mwaka jana ya kuwataka polisi kuwapiga watakaokaidi amri halali ya polisi.
Akisoma hukumu hiyo jaji Jundu huku akinukuu baadhi ya ibara amesema Ibara ya 100 (2) inaweza kujadiliwa mahakamani, ambayo inasema bila kuathiri katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yoyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo.
Amesema kutokana na sababu hizo, mahakama inatupilia mbali kesi hiyo kwa sababu waliofungua kesi, LHRC na TLS hawakustahili kisheria kufungua kesi hiyo kwa sababu hawakuathirika.
0 comments:
Post a Comment