June 18, 2014

  • JAMII YAASWA KUWASAIDIA WATOTO YATIMA



    JAMII YAASWA KUWASAIDIA WATOTO YATIMA
     Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita akimkabidhi zawadi Blessing Kikoti mwanafunzi wa darasa la nne aliyefanya vizuri katika masomo yake kwa kuwa wa kwanza katika masomo.
    Mkuu Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita akihutubia.(picha zote na Denis Mlowe)
     Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilolo Ulbad Wampemba akizungumza na watoto na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika kiwalaya yalifanyika katika ofisi za kijiji cha Ilamba kata ya Dabaga tarafa ya Kilolo mkoani Iringa.
     Baadhi ya watoto waliohudhuria maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika wakifatalia hotuba mbalimbali za viongozi walihudhuria sherehe hizo. Maadhimisho hayo kiwalaya yalifanyika katika ofisi za kijiji cha Ilamba kata ya Dabaga tarafa ya Kilolo mkoani Iringa.
     
    Na Denis Mlowe,Iringa
     
    JAMII imetakiwa kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, kwa kuwapatia elimu iliyo bora na kuwapa upendo na si kuiachia serikali ama mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasaidia.
     
    Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Ilamba kata ya Dabaga tarafa ya Kilolo.
     
    Guninita alisema jamii imekuwa ikiitupia lawama serikali mara kwa mara bila kutambua kuwa jukumu la kuwalea na kuwasaidia ni jukumu la kila mmoja katika jamii tunayoishi kwa lengo la kuwapatia elimu itakayowakomboa katika mazingira magumu.
     
    Alisema jamii inatakiwa kupanga mikakati kabambe ya kuwaepusha watoto na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au unyanyasaji wa aina yoyote katika maisha yao ya kila siku kwa kuwa nao wanahaki ya kuishi.
     
    Aidha aliitaka jamii kuacha mila na tamaduni zilizopo katika jamii ambazo zinamnyima motto haki ya kupata elimu na kusababisha baadhi ya watoto kukimbilia mitaani kwa kuwa mila hizo zinakiuka misingi ya haki za msingi za mtoto.
     
    "Ni kweli wilaya ya Kilolo ina watoto ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, wengine wanalelewa katika vituo maalum vilivyopo wilayani mwetu kama wanaoishi Amani Center ni jukumu la kila mmoja wetu kuwasaidia na kuwapatia elimu iliyo bora na kuwaondoa katika mazingira yasiyofaa katika jamii" alisema Guninita

    Katika taarifa iliyosomwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kilolo Issa Mohamed alisema jamii inatakiwa kuondokana na mila ambazo zinawazuia watoto kupata elimu au kuendelea na masomo kama vile ndoa za utotoni, ukeketaji na kusomesha watoto wa kiume.
     
    "Wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuendelea na mila zenye madhara ambazo zinawasababisha watoto kutoendelea na masomo au kutoende shule kabisa kwa kufanya hivyo ni kukiuka haki ya msingi za watoto kwani watoto wana haki ya kulindwa na kupewa huduma zote za msingi ikiwemo elimu bora." Alisema Mohamed
     
    Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Kila mtoto ana haki ya elimu bora bila vikwazo"


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.