Huku zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya kufikiwa kwa siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, wagombea urais wanaochuana kwa karibu kutokana na wingi wa watu wanaojitokeza katika kampeni zao, Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaendelea kutoa ahadi nzito kadhaa kwa wapiga kura.
Kadiri inavyoonekana, ahadi hizo zikitekelezwa kwa asilimia 100, zitafanya muujiza kwa kuibadili Tanzania kutoka katika hali duni ya upatikanaji wa baadhi ya huduma za jamii na kuonekana kama `Ulaya'.
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa wiki kadhaa tangu kampeni za uchaguzi mkuu kuanza rasmi Agosti 22, mwaka huu, umebaini kuwa hadi sasa, Magufuli na Lowassa wameshatoa ahadi nyingi nzito na ambazo zikitekelezwa kwa ukamilifu pindi yeyote kati yao akishinda zitaibadili kwa kiasi kikubwa Tanzania itakayoachwa na serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Uchunguzi huo wa Nipashe pia umebaini kuwa kati ya ahadi zote, zipo tano zinazoonekana kuwa kubwa zaidi kwao kwani huzisisitiza karibu katika kila mikutano yao.
Kwa ujumla wake, serikali ya Lowassa itahitaji takriban Sh. trilioni 28.29 ili kukamilisha ahadi hizo tano katika miaka yake mitano ya kuwa madarakani pindi akishinda urais, huku serikali ya Magufuli ikitarajiwa kutumia wastani wa Sh. trilioni 63.64 ili kutimiza ahadi zake hizo tano. Thamani ya ahadi zote kuu tano kwa pamoja zina thamani ya Sh. trilioni 91.93.
Aidha, gharama hizi za Sh.28.29 kwa ahadi tano za Lowassa ni sawa na asilimia 25.15 ya bajeti ya Serikali kwa miaka mitano (Sh. trilioni 112.475) kwa kuzingatia bajeti ya mwaka 2015/16 ambayo ni Sh. trilioni 22.495 kama ilivyowasilishwa na kupitishwa na bunge Juni mwaka huu mjini Dodoma. Kadhalika, wastani wa gharama za ahadi tano za Magufuli (Sh. trilioni 63.64) ni sawa na asilimia 56.58 ya bajeti ya sasa ya Serikali kwa miaka mitano ikiwa kiwango chake kitabaki mara zote kuwa kama cha bajeti ya mwaka 2015/16.
AHADI ZA MAGUFULI:
1. AFYA (Sh. trilioni 29.15)
Hii ni moja kati ya ahadi kubwa katika kampeni za Dk. Magufuli na amekuwa akiirudia karibu kila aendako.
Anasisitiza kuwa iwapo Watanzania watamchagua Oktoba 25 na kumfikisha Ikulu, atahakikisha anajenga zahanati katika kila kijiji, kituo cha Afya katika kila kata, hospitali katika kila wilaya na hospitali ya rufaa katika kila mkoa.
Kwa mujibu wa msemaji wa kamati ya kampeni ya CCM, January Makamba, hadi sasa asilimia 40 ya vijiji nchini tayari vina zahanati na hivyo, kazi ya serikali itakayoongozwa na Magufuli iwapo atashinda ni kumalizia ujenzi katika asilimia 60 ya vijiji vyote nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na nyingine zilizofikishwa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajili ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, idadi ya vijiji vyote nchini ni 19,200; idadi ya kata ni 3,957; idadi ya wilaya ni 133 na idadi ya mikoa ni 31. Hivyo, ili kutimiza ahadi ya kuwa na zahanati katika kila kijiji, serikali ya Dk. Magufuli italazimika kujenga zahanati mpya 11,520, ambayo ni asilimia 60 ya idadi ya vijiji ambavyo bado havijawa na zahanati.
Taarifa ambazo Nipashe imezipata kupitia uchunguzi wake kwenye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii umebainisha kuwa wastani wa kujenga zahanati moja yenye sifa zinazostahili hadi kukamilika kwake ni Sh. bilioni 1.3; kituo cha afya ni Sh. bilioni 5.5; Hospitali ya Wilaya Sh. bilioni 30 na hospitali ya mkoa kuwa na hadhi ya rufaa ni Sh. bilioni 80. Hata hivyo, inaelezwa kuwa gharama hizi zaweza kupungua au kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za mahala husika na nguvu ya soko.
Kwa sababu hiyo, gharama za jumla ambazo serikali ya Magufuli itazibeba kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika vijiji 11,520 iwapo atashinda Oktoba 25 na kuingia Ikulu ni Sh. trilioni 14.98.
Kadhalika, Nipashe inatambua kuwa baadhi ya kata nchini tayari zina vituo vya afya, kama ilivyo kwa wilaya ambazo baadhi tayari zina hospitali zake na pia baadhi ya mikoa tayari ina hospitali zenye hadhi ya rufaa. Kwa sababu hiyo, ikiwa itakadiriwa kuwa serikali ijayo chini ya Magufuli itawekeza katika kufanikisha upatikanaji wa vituo vya afya walau katika nusu ya kata zote nchini, yaani kata 1,979, maana yake italazimika kutumia Sh. trilioni 10.88. Ikiwa itakadiriwa kuwa nusu ya idadi ya wilaya zitajengewa hospitali za hadhi yake, yaani wilaya 67, maana yake serikali ya Magufuli itatumia Sh. trilioni 2.01 kukamilisha miradi hiyo. Aidha, serikali ya Dk. Magufuli italazimika pia kutumia Sh. trilioni 1.28 ikiwa walau nusu ya idadi ya mikoa yote nchini (mikoa 16) itawezeshwa kuwa na hospitali zake za rufaa kwa gharama ya Sh. bilioni 80 kwa kila moja.
Kwa ujumla, makadirio haya yanaonyesha kuwa serikali ijayo chini ya Dk. Magufuli itatumia Sh. trilioni 29.15 ili kutimiza ahadi ya kujenga zahanati kwa kila kijiji, kituo cha afya kwa kila kata, hospitali ya wilaya kwa kila wilaya na hospitali ya rufaa kwa kila mkoa.
Katika eneo hili la afya, Magufuli ameahidi pia kujaza dawa na vifaa tiba katika taasisi zote za afya za serikali ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa sasa wanaoupata kwa kuandikiwa tu cheti na kuambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi.
Katika eneo hili la afya, Magufuli ameahidi pia kujaza dawa na vifaa tiba katika taasisi zote za afya za serikali ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa sasa wanaoupata kwa kuandikiwa tu cheti na kuambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini vilevile kuwa Serikali ya Magufuli italazimika kufanya kazi kubwa ya kutimiza mahitaji ya hospitali za rufaa ambazo mahitaji yake muhimu ni pamoja na kuwa na maabara ya kompyuta, vipimo vya mionzi vya CT Scan, Ultra Sound, vipimo vya moyo, vipimo vya ngozi, vipimo vya mishipa ya kichwa na uti wa mgongo (EEG Test), maabara nzuri na ya kisasa ya damu salama, chumba cha kuhifadhia maiti kinachojitosheleza kwa vifaa na nafasi, magari ya wagonjwa, chumba maalum cha kujifungulia, vifaa kwa waliopata ajali ya mifupa maarufu kama 'jiwe.' Kadhalika, hospitali za rufaa zinahitaji pia wataalam kama madaktari bingwa wa upasuaji; watoto ; kina mama; macho; mfumo wa mwili; mifupa ; mtaalamu wa Iishe; mtaalamu wa damu; mtaalamu wa maabara; masikio, pua na mwili; ngozi na moyo. Kunatakiwa pia kuwapo wauguzi na wakunga wazoefu wa idadi ya kutosha.
2. ELIMU BURE HADI KIDATO CHA NNE (Sh. trilioni 5.14)
Katika mikutano yake yote, Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake itatoa elimu bure kwa kila mtoto wa Tanzania kuanzia awali hadi kidato cha nne.
Hivi sasa, elimu ya msingi hutolewa bure pia ingawa wapo wazazi hulalamika kuwa wingi wa michango inayotofautiana kati ya shule na shule ni mzigo mkubwa, pengine kuliko hata ada. Serikali itakayokuwa chini ya Magufuli inatarajiwa kumaliza pia kero hii ya mlolongo wa michango.
Katika hotuba yake wakati wa kilele cha maadhimisho ya pili kitaifa ya wiki ya elimu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Mei 15 mwaka huu, Rais Kikwete alisema hadi kufikia mwaka 2014, idadi ya wanafunzi wa shule za msingi nchini ilikuwa ni milioni 8.23 na idadi ya wanafunzi wa shule za sekondari ni 1,804,056.
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa wastani wa gharama za michango kwa kila mwanafunzi kwa mwaka katika Shule ya Msingi Tumaini iliyopo Iringa ni Sh. 70,000, hii ikijumuisha umeme, maji na ulinzi. Kwa sababu hiyo, ikiwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi nchini atakuwa akilipia michango ya kiwango sawa na shule hiyo ya Tumaini ya Iringa, maana yake ni kwamba gharama za jumla kwa wanafunzi wote ni Sh. bilioni 576.1 na kwa miaka mitano ya kuwa madarakani, serikali ya Magufuli itatumia Sh. trilioni 2.88.
Kadhalika, uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa licha ya kuwapo kwa ada nafuu ya Sh. 20,000 kwa shule za kutwa na Sh. 70,000 kwa shule za sekondari, bado michango imekuwa tatizo kubwa. Kwa mfano, mwanafunzi aliyeanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya kutwa ya Kihesa iliyopo Iringa mwaka huu alitakiwa kulipa takriban Sh. 250,000 kwa ajili ya ada, michango mbalimbali na vifaa kama panga, kwanja na jembe. Hata hivyo, haya ni makadirio tu kwani Nipashe inatambua kuwa michango hutofautiana kati ya shule moja na nyingine kutokana na sababu mbalimbali.
Ikiwa kila mwanafunzi wa sekondari nchini atakuwa akitozwa ada na michango kwa kiwango sawa na wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza wa shule hiyo ya Kihesa, maana yake gharama zote zitakazokuwa zikibebwa na serikali ya Magufuli kwa mwaka zitakuwa ni Sh. bilioni 451.01, hivyo kwa miaka mitano itakuwa Sh. trilioni 2.26.
Hivyo, gharama zitakazolipwa na serikali ya Magufuli ili kutekeleza ahadi ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne kwa miaka mitano ya kuwa madarakani itakuwa ni Sh. trilioni 5.14.
3. MELI 3 MPYA (Sh. Sh. bilioni 833.7)
Akiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Magufuli alisema atatimiza ahadi zilizowahi kutolewa na Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake kwani zote hizo ni sawa na 'amri'. Miongoni mwa ahadi alizozikumbushia Magufuli ni ununuzi wa meli mpya katika maziwa makubwa nchini ya Victoria, Tanganyika na Nyasa, lengo likiwa ni kumaliza kero ya usafiri katika maeneo ya mikoa yenye maziwa hayo.
Kwa mujibu wa mtandao wa ships4ever.com, bei ya meli ya mtumba iliyotengenezwa mwaka 2001, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 850 ni euro milioni 115, sawa na Sh. bilioni 277.9. Kwa sababu hiyo, ikiwa maziwa yote matatu yatanunuliwa meli za sifa hii, maana yake serikali itakayoongozwa na Magufuli itatimiza ahadi hii kwa kutumia Sh. bilioni 833.7 ndani ya miaka yake mitano.
4. MILIONI 50 KILA KIJIJI, MTAA (Sh. trilioni 1.15)
Magufuli amekuwa akiitoa ahadi hii tangu siku ya kwanza ya kampeni zake, kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, Jumapili ya Agosti 22. Hata mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu, amekuwa akiirudia ahadi hii karibu katika mikutano yake yote.
Alipokuwa Babati, Wilaya ya Hanang', viwanja vya Katesh, Magufuli alifafanua zaidi ahadi yake hii kwa kusema kuwa fedha hizo zitatolewa siyo tu kwa kila kijiji, bali pia ni kwa kila mtaa. Lengo la fedha hizo ni kwa ajili ya kuwapa mikopo vijana na kina mama ili ziwasaidie kwa shughuli za ujasiriamali.
Kwa mujibu wa Tamisemi, mbali na kuwapo kwa vijiji 19,200, pia kuna mitaa 3,741. Kwa sababu hiyo, serikali ya Magufuli italazimika kutumia fedha hizo katika maeneo 22,941 (jumla ya vijiji na mitaa), hivyo gharama zote kufikia takriban Sh. trilioni 1.15.
5. RELI MPYA YA KATI, BARABARA (Sh. trilioni 19.86)
Ahadi hii iliwahi pia kutolewa na serikali ya Rais Kikwete inayomaliza muda wake baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25. Ikitekelezwa kwa uhakika kutokana na kile anachoahidi Magufuli, ni wazi kuwa serikali itakayokuwa chini ya Magufuli itakuwa na kibarua kingine kizito.
Akizungumza katika mkutano wake mmojawapo wa kampeni kwenye viwanja vya Kawawa mkoani Kigoma, Magufuli alisema atajenga reli mpya ya kati (kiwango cha standard gauge) itakayoondoa matatizo ya usafiri kwa wakazi wa mkoa huo na mingine ya kanda za Magharibi, Kati na Ziwa. Kwa mujibu wa mtandao wa a4architect.com, Reli ya kiwango hicho (standard gauge), huwa na upana wa mita 1.435 na siyo mita 1.067 kama ilivyo kwa reli zilizojengwa enzi za ukoloni.
Mtandao huo (a4architect.com) unaonyesha kuwa kampuni ya ujenzi ya China Communiucations Construction Limited (CCC LTD), imetoa makadirio ya gharama za kujenga reli ya kiwango cha 'standard gauge' kutoka Kenya,Uganda hadi Rwanda kuwa kilomita moja ni shilingi za Kenya milioni 413, sawa na Sh. bilioni 8.4 za Tanzania. Na kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandao wa Distancefrom, makadirio ya umbali wa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ni kilomita 1,367.
Kwa sababu hiyo, ili kutekeleza ahadi ya Magufuli kwa kujenga reli ya 'standard gauge' kwa kiwango sawa na mradi wa reli ya Kenya - Uganda hadi Rwanda, maana yake zitahitajika takriban Sh. trilioni 11.48.
Kadhalika, kikokotozi cha mtandao wa Distance from kinaonyesha zaidi kuwa makadirio ya umbali wa ardhini kutoka Tabora hadi Mpanda ni Kilomita 244 na pia kutoka Tabora hadi Mwanza ni Kilomita 278. Hivyo, jumla ya umbali wa reli mpya kutoka Tabora hadi Mwanza na nyingine ya kuelekea Mpanda ni kilomita 522. Ikijengwa reli ya kiwango kama cha Kenya, Uganda na Rwanda, maana yake serikali itakayokuwa chini ya Magufuli itagharimia kiasi kingine cha Sh. trilioni 4.38.
Kadhalika, Magufuli mwenyewe ameahidi pia kuongeza mtandao wa barabara za lami nchini kutoka kilomita 17,000 zilizopo sasa hadi kufikia zaidi ya kilomita 21,000. Hii maana yake ni kwamba serikali itakayokuwa ya Magufuli itajenga barabara moja ya urefu wa Kilomita 4,000. Ikiwa wastani wa kujenga Kilomita moja ya barabara ya lami ni Sh. bilioni moja, maana yake serikali ya Magufuli italazimika kutumia takriban Sh. trilioni 4 kutimiza ahadi hii.
Hivyo, ili kukamilisha miradi yote ya reli mpya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma,Tabora - Mpanda na Tabora - Mwanza na pia kutandaza barabara za lami, serikali itakayokuwa chini ya Magufuli italazimika kutumia Sh. trilioni 19.86.
AHADI 5 ZA LOWASSA:
1. ELIMU BURE HADI CHUO KIKUU (Sh. trilioni 9.9)
Ahadi hii ya elimu hadi chuo kikuu ni mojawapo ya kete muhimu za Lowassa katika kampeni zinazoendelea. Hapa, kwa kuchukua makadirio ya jumla ya gharama za kuwasomesha wanafunzi kutoka shule ya msingi hadi kidato cha nne kwa mwaka zitokanazo na zile za Magufuli, maana yake serikali itakayokuwa chini ya utawala wa Lowassa italazimika kutenga walau Sh. trilioni 5.14 katika miaka yake mitano ya kuwa madarakani.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), wanafunzi waliochaguliwa kuendelea na kidato cha tano mwaka 2013 ni 33,683 na waliochaguliwa kujiunga na kidato hicho mwaka 2014 ni 54,085. Ukichukuliwa wastani wa wanafunzi hawa kwa uchaguzi wa miaka hiyo miwili, maana yake kila mwaka huchaguliwa wanafunzi 43,884. Ikiwa idadi hii ni sawa pia na wanafunzi wa kidato cha sita (makadirio tu), maana yake wanafunzi wa kidato cha tano na sita ni 87,768.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa wanafunzi walioingia kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Tambaza ya jijini Dar es Salaam mwaka huu walilipa ada ya Sh. 20,000 kila mmoja pamoja na michango na vifaa, jumla ikiwa ni Sh. 260,000. Mbali na ada, mchanganuo wa gharama hizo kwa shule ya Tambaza ni mchango wa tahadhari Sh. 5,000, kitambulisho Sh. 5,000, madawati Sh.15,000, taaluma Sh.10,000, maendeleo Sh.15,000, ulinzi Sh. 5,000, nembo ya shule Sh. 2,000, usafi wa vyoo Sh.3,000, matibabu Sh. 5,000, mahafali Sh. 10,000, kijiji cha michezo Sh. 5,000, mitihani ya kila mwezi Sh. 30,000, masomo ya ziada Sh. 30,000 na Sh. 100,000 kwa ajili ya fagio, dawa, reki, jembe, panga, fyekeo, ndoo na karatasi.
Hivyo, ikiwa wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita watalipia ada na michango kwa mwaka kama ilivyo kwa wanafunzi waliongia kidato cha tano Tambaza mwaka huu, maana yake serikali itakayokuwa chini ya Lowassa itagharimia jumla ya Sh. bilioni 22.82 na kwa miaka mitano itakuwa ni Sh. bilioni 114.1.
Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), idadi ya wanafunzi walioko vyuoni nchini hivi sasa ni 200,986. Aidha, tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu na pia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (udsm.ac.tz) inaonyesha kuwa gharama za mwanafunzi anayesoma Shahada ya Kwanza ya Ualimu (Sayansi), katika Shule Kuu ya Ualimu Mkwawa (DUCE) ni Sh. milioni 1.3.
Nipashe inatambua kuwa ada hiyo ikichanganywa na mahitaji mengine kwa mwaka yaweza kufikia wastani wa sh. milioni 4.5. Hivyo, ikiwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu watagharimiwa kwa makadirio hayo, maana yake serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kutenga Sh. bilioni 904. 44 kwa mwaka na hivyo kwa miaka mitano itakuwa ni Sh. trilioni 4.52.
Hata hivyo, haya ni makadirio tu kwani zipo baadhi ya shahada kama uhandisi na udaktari ambazo wanafunzi hugharimiwa kwa wastani wa Sh. milioni sita kwa mwaka kama gharama ya masomo na matumizi mengineyo.
Kadhalika, Lowassa ameahidi kusamehe madeni yote ya Watanzania waliosomeshwa kupitia mikopo itokayo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Takwimu za HESLB zinaonyesha kuwa hadi kufikia Juni, 2014, madeni haya yalikuwa na thamani ya Sh. bilioni 123.8.
Kwa sababu hiyo, ikiwa Lowassa atashinda, serikali atakayoiongoza italazimika kutumia takriban Sh. trilioni 9.90 ili kutimiza ahadi yake ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu na pia kusamehe madeni HESLB.
2. BIMA YA AFYA, HOSPITALI KILA WILAYA (Sh. trilioni 5.84)
Ahadi mojawapo maarufu ya Lowassa ni ya kuboresha huduma za afya kwa kuwawezesha Watanzania kujiunga na bima nafuu.
"Afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii," inasema sehemu ya hotuba ya Lowassa iliyosambazwa kwenye mitandao baada ya uzinduzi wa kampeni zake kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam Agosti 29, 2015.
Tovuti ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa - NHIF - (nhif.or.tz), inaonyesha kuwa yeyote anayetaka kujiunga na fao la matibabu la Kikoa ndani ya mfuko ambalo ni maalum kwa watu walio katika sekta zisizo rasmi, hulazimika kukidhi vigezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kulipia mchango wa Sh. 76,800 kwa mwaka ili wapate nafasi ya kutibiwa katika taasisi za afya 6,000 zilizopo nchini.
Kila mwanachama huwa na nafasi ya kutibiwa yeye na wategemezi wanne. Kwa mujibu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 48,522,228 huku wastani wa idadi ya watu kwa kila kaya ni 4.7 (Bara) na 5.1 (Zanzibar), kwa maana ya watu watano.
Kwa sababu hiyo, makadirio ya idadi ya kaya nchini ni 9,704,445.6. Hivyo, ikiwa kila kaya itawezeshwa na serikali itakayokuwa chini ya Lowassa kuingizwa kwenye mfumo wa Bima ya Afya wa fao la Kikoa la NHIF, maana yake utekelezaji wa ahadi hii kwa kila mwaka utahitaji takriban Sh. bilioni 745.30 na kwa miaka mitano ni Sh. trilioni 3.73.
Kadhalika, Lowassa aliahidi kujenga hospitali za wilaya katika makao makuu ya kila wilaya. Akihutubia kwenye mkutano wa kampeni jijini Arusha, Oktoba 8, alisema: "Nitahakikisha kwenye makao makuu zote za wilaya zinakuwa na hospitali za wilaya."
Kama ilivyokuwa kwenye hesabu za ahadi za Magufuli, eneo hili la hospitali za wilaya litaigharimu serikali itakayokuwa ya Lowassa takriban Sh. trilioni 2.01.
Kadhalika, alitoa ahadi ya kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa kwenye hospitali za serikali ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa kwake.
Katika kutekeleza ahadi hii, serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kuanza kwa kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 102 ambazo Bunge lilithibitishiwa Julai 2 mwaka huu kuwa serikali inadaiwa na Bohari ya Dawa (MSD).
Kwa sababu hiyo, serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kugharimia walau kiasi cha Sh. trilioni 5.84 ili kutekeleza ahadi zinazohusiana na afya, achilia mbali ununuzi wa vifaa tiba, kuajiri watumishi wa kutosha wa sekta ya afya, kuboresha maslahi yao na kulipa malimbikizo ya madai mbalimbali yatokanayo na stahili zao.
3. POSHO WENYEVITI VIJIJI, MITAA (Sh. trilioni 1.84)
Akiwa kwenye kampeni zake kwenye viwanja vya Katesh, wilaya ya Hanan'g mkoani Manyara, Oktoba 4, Lowassa aliahidi kuwa akishinda, serikali yake itawalipa posho wenyeviti wa vijiji, mitaa hadi vitongoji ili watekeleze majukumu yao kikamilifu.
"Ni lazima na wao tuwalipe kwa sababu kazi wanayofanya ni kubwa sana...hivyo na wao tutawalipa posho," alisema.
Kwa mujibu wa Tamisemi, Tanzania ina vijiji 19,200, mitaa 3,741 na vitongoji 64,616. Hii maana yake ni kwamba, jumla ya wenyeviti watakolipwa posho na serikali itakayokuwa chini ya Lowassa ni 87,557 (jumla ya wenyeviti vijiji, mitaa na vitongoji).
Aidha, kwa mujibu wa Tamisemi, posho za madiwani nchini ni Sh. 350,000 kwa mwezi. Kama serikali itakayokuwa chini ya Lowassa itaamua kuwalipa wenyeviti wa vijiji walau nusu ya kiwango hicho wanacholipwa madiwani, yaani Sh. 175,000, maana yake gharama za jumla kwa mwezi zitakuwa Sh. bilioni 30.64, sawa na Sh. bilioni 367.74 kwa mwaka au Sh. trilioni 1.84 kwa miaka yake mitano ya kuwa madarakani ikiwa posho hii haitabadilika.
4. RELI YA TANGA - ARUSHA - MARA (Sh. trilioni 7.64)
Hii ni mojawapo ya ahadi za kusisimua za Lowassa. Akihutubia mbele ya maelfu ya watu kwenye viwanja vya Tangamano jijini Tanga, alisema akiingia madarakani, serikali yake itajenga reli mpya (standard gauge) inayotoka Tanga kwenda mikoa ya Arusha na Mara.
Kwa mujibu wa kikokotozi cha mtandao wa Distancefrom, makadirio ya umbali wa barabara kutoka Tanga, Arusha hadi Mara ni Kilomita 909.
Kama ilivyokuwa kwa hesabu za makadirio ya reli atakayojenga Magufuli kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, gharama za kujenga Kilomita moja ya reli hii ni Sh. bilioni 8.4. Kwa sababu hiyo, ili kutekeleza ahadi ya kujenga reli mpya ya 'standard gauge' kutoka Tanga hadi Mara, maana yake serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kutumia takriban Sh. trilioni 7.64 katika miaka yake mitano kutimia ahadi hii.
5. KUMALIZA FOLENI JIJINI DAR (Sh. trilioni 3.07)
Miongoni mwa ahadi za Lowassa ni kuunda wizara maalum itakayoshughulikia kero za jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha uchumi wa nchi na kwamba, jambo mojawapo atakalolishughulikia mapema akiingia Ikulu ni kumaliza foleni za barabarani.
Ili kufanikisha ahadi hii, ni wazi kwamba serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kushughulikia mipango kadhaa iliyoainishwa na Wizara ya Ujenzi ili kupunguza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam, ikiwamo kujenga barabara za pembezoni (ring roads) na barabara za juu (fly-overs) kwenye maeneo ya makutano ya barabara kuu kama Mandela/Nyerere na Mandela/Morogoro.
Kwa mujibu wa makadirio ya Wizara ya Ujenzi mwaka wa fedha 2013/2014, gharama za kukamilisha barabara za pembezoni na usanifu wa barabara za juu ni Sh. bilioni 171.2. Baadhi ya miradi ya barabara za pembezoni zilitajwa kuwa ni Kigogo – Jangwani, Kimara Korogwe - Kilungule, Tangi Bovu-Goba, Baruti - Msewe na Kigogo - Tabata Dampo.
Kadhalika, taarifa iliyowahi kutolewa na Waziri wa Ujenzi Novemba 19, 2014 wakati akielezea mpango wa kujenga daraja la Salender jijini Dar es Salaam, ilieleza kuwa gharama za kukamilisha ujenzi wa barabara za juu jijini Dar es Salaam ni zaidi ya Sh. trilioni 2.9.
Kwa sababu hiyo, ili kutekeleza ahadi ya kushughulikia kero ya foleni jijini Dar, serikali itakayokuwa chini ya Lowassa italazimika kutumia takriban Sh. trilioni 3.07.
WASOMI WANENA
Akizungumzia ahadi za wagombea urais zinazoendelea kutolewa katika kampeni zinazoendelea, Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma) wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mtakatifu Stefano Moshi (SMMUCo), Dk. Gasper Mpehongwa, alisema baadhi zinatekelezeka iwapo kutakuwa na matumizi mazuri ya fedha na kuongeza makusanyo ya kodi.
Hata hivyo, alisema baadhi ya ahadi hizo haziwezi kutekelezeka na kwamba kwa mtazamo wake, zinatolewa kwa sura ya kisiasa zaidi kuliko uhalisia.
"Kwa mfano, wakurugenzi wa halmashauri wanatumia mashangingi (magari aina ya Land Cruiser) ya gharama kubwa... kukiwapo udhibiti wa matumizi ya fedha za serikali, ahadi nyingi zinazotolewa zinaweza kutekelezeka," anasema Dk. Mpehongwa.
Akitolea mfano, alisema elimu bure hadi chuo kikuu au elimu bure hadi sekondari inawezekana kwa kusimamia vizuri rasilimali za umma na pia kuwapo kwa vipaumbele vizuri.
Mhadhiri wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe (Dar es Salaam), Profesa Prosper Ngowi, alisema kutekeleza ahadi hizo kunawezekana endapo kiongozi atakayeingia madarakani atakuwa na misingi iliyo imara ya kupata fedha hizo za kutekeleza ahadi.
Alisema wagombea hao wangewaeleza wananchi njia na mikakati ya namna ya kupata fedha ili kutekeleza ahadi hizo ikiwamo kujenga zahanati kila kijiji na elimu bure hadi chuo kikuu.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment