October 29, 2015

  • APIGWA KWA KUZANIWA MWIZI


    APIGWA KWA KUZANIWA MWIZI


    SWADAKTA! Katika hali ya kustaajabisha, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Ramadhan, ambaye mwishoni mwa wiki amejikuta akishushiwa kipigo kwa kudhaniwa kuwa kibaka, alisalimika baada ya kuanza kusali kwa kuwashtakia kwa Mwenyezi Mungu waliokuwa wakimpiga, akisema hakuwa na hatia na ghafla watu hao kusitisha kipigo.

    Ramadhan alikutana na hali hiyo baada ya kutuhumiwa kuiba redio kutoka katika duka moja lililopo stendi ya daladala mjini hapa.

    Ilidaiwa kuwa kibaka huyo baada ya kuchukua redio hiyo alianza kukimbia kutokana na mwenye duka kumwitia mwizi na Ramadhan akawa mmoja kati ya watu waliokuwa wakimfukuza, kabla ya mdokozi huyo kujichanganya na watu hivyo kutotambulika kirahisi.

    Baada ya kuona hivyo, wananchi hao wenye hasira walimgeukia kijana huyo na kuanza kumpa kipigo kama cha mbwa mwizi kwa vile nguo zake zilikuwa zimefanana na zile zilizokuwa zimevaliwa na kibaka aliyekuwa akifukuzwa.

    "Ewe Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa msaada wako niepushie na mtihani huu niliosingiziwa kwani wewe ndiwe unayejua ukweli wa tukio hili," mtu huyo alisikika akisema kufuatia kipigo alichokuwa akikipata, baada ya kukimbia na kwenda kujibanza pembeni ya duka linalouza vinywaji baridi.

    Kufuatia maneno hayo, watu wote walijikuta wakisitisha zoezi la kumpiga na mmoja wa bodaboda wa kijiwe cha Juwata aliingia kati na kusema; "Jamani huyu jamaa anaonekana siyo mwizi na ni mtu wa dini, hivyo naomba aliyeibiwa ajitokeze na kutoa ushuhuda," alisema na hakuna aliyejitokeza.

    Kijana Ramadhan akishusha dua zito baada ya kushushiwa kipigo kikali.
    Baada ya kuona hivyo, kijana huyo aliwataka watu hao kumuacha aende zake huku baadhi ya walioshiriki kumpiga wakimuomba msamaha mtu huyo aliyekuwa akivuja damu mwili mzima.Akizungumza na mwandishi wetu, Ramadhan alisema alishuka kwenye daladala na kuungana na watu waliokuwa wakimfukuza mwizi kabla hawajamgeuzia kibao kutokana na nguo zake kufanana na za kibaka.

    "Mwizi alijichanganya na watu ndipo nikageukiwa mimi, nikakimbilia hapa dukani kwa Mhindi na kuamua kuomba msaada kwa Mungu kwa kuomba na akafanikiwa kuniokoa," alisema kijana huyo.

    Katika stendi ya daladala, mfanyabiashara wa duka lililoibiwa, aliyejitambulisha kwa jina la Shaaban, alisema alikuwa amekwenda kutafuta chenchi, ndipo alipomuona mtu akiondoka na redio yake na yeye akapiga kelele za mwizi, akadondosha bidhaa hiyo na kukimbia, lakini akashindwa kuungana na watu kumkimbiza kwa vile hakukuwa na mtu mwingine dukani.

    Wananchi wenye hasira kali wakiwa eneo la tukio.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.