Serikali ya kaunti ya Nairobi nchini Kenya imebadilisha jina la barabara moja na kuipa jina la Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.
Kiongozi huyo alikuwa nchini Kenya kwa ziara ya siku tatu na Jumanne alihutubia kikao cha pamoja cha Bunge la Seneti na Bunge la Kitaifa.
Rais Kikwete alihudhuria sherehe ya kubadilisha jina barabara hiyo ya Milimani iliyoko karibu na ikulu ya Nairobi.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 0.49 huanzia makutano ya barabara ya Kenyatta Avenue na Valley Road na kufululiza hadi barabara ya Dennis Pritt.
"Rais Kenyatta aliposema kwamba utazuru hapa tulishauriana kujua iwapo tungeweza kubadilisha jina la barabara hii na kwa kuwa sisi ni marafiki, alikubali, na kama uonavyo, inaelekea hadi lango la ikulu yake (Bw Kenyatta)," Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero alimwambia Bw Kikwete, kwa mujibu wa gazeti la The Star la Kenya.
Barabara hiyo imo karibu na barabara ya Nyerere.
Rais Kikwete sasa anajiunga na kiongozi wa kwanza wa Tanzania Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Karume katika kuwa na barabara zilizopewa majina yao Nairobi.
Kabla ya kuondoka mamlakani mwaka 2013, aliyekuwa rais wa Kenya wakati huo Mwai Kibaki, alibahatika kuwa na barabara yenye jina lake jijini Dar es Salaam.
Sherehe ya kubadilisha jina la barabara hiyo ya Old Bagamoyo ilihudhuriwa na Bw Kibaki mwenyewe, Rais Kikwete na Bw John Magufuli aliyekuwa waziri.
Bw Magufuli kwa sasa ni mgombea wa urais wa chama tawala cha CCM.
0 comments:
Post a Comment