October 16, 2015

  • LORI LA SODA LAANGUKA WANANCHI WAJISEVIA VINYWAJI WENGINE WAPELEKA NYUMBANI



    LORI LA SODA LAANGUKA WANANCHI WAJISEVIA VINYWAJI WENGINE WAPELEKA NYUMBANI

    Wananchi wa eneo la Muringato katika Kaunti ya Nyeri walijivinjari kwa vinywaji baada ya lori lililokuwa likisafirisha soda kuanguka katika eneo hilo kwenye barabara ya Nyeri – Nyahururu.

    Tukio hilo lilitokea Alhamisi mwendo wa saa nne usiku baada ya dereva kushindwa kudhibiti usukani wakati akijaribu kupiga kona.
    Inaaminika kuwa lori hilo lilikuwa likielekea Mweiga kwa kasi mno, hali iliyofanya dereva kushindwa kulidhibiti alipojaribu kupinda.

    Matokeo yake yalikuwa ni lori kuanguka ambapo kreti nyingi za soda zilitapakaa kote na mafuta aina ya dizeli yakamwagika kando ya barabara.

    "Lori lilipoteza mwelekeo wake na kupinduka kiasi cha kulalia ubavu," akasema Bw James Thatu, shahidi wa tukio hilo na mkazi wa eneo hilo.

    Wakazi na watumiazi wengine wa barabara hawakusita ila kuamua kujivinjari na kubugia vinywaji vya bure.
    Akithibitisha tukio hilo, mkuu wa polisi wa Nyeri ya Kati, Charles Rotich alisema kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

    "Idara ya trafiki alitembelea eneo la tukio. Hakuna aliyejeruhiwa," alisema.
    Kiasi cha soda iliyopotea bado hakijathibitishwa.
     Picha hapo chini ni Wakazi wa mtaa wa Muringato mjini Nyeri wakiwa katika eneo la ajali ambapo lori la kusafirisha soda lilianguka kando ya barabara ya Nyeri-Nyahururu usiku wa Oktoba 15, 2015.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.