September 15, 2015

  • Wahariri Walaani Mwandishi wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo Kupigwa Na Vijana wa CHADEMA



    Wahariri Walaani Mwandishi wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo Kupigwa Na Vijana wa CHADEMA

    JUKWAA la Wahariri Nchini (TEF), limewataka wanahabari kuwa makini na maisha yao wakati huu wa mchakato wa uchaguzi sambamba na kulaani kitendo cha vijana wa Chadema cha kumshambulia na kumpiga mwandishi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Christopher Lissa.

    Aidha, limewataka vyama vya siasa na watu binafsi wanaoandaa mikutano ya waandishi wa habari kutowaalika makada wa vyama vyao ambao si wanataaluma katika mikutano hiyo.

    Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda alisema kitendo cha kumpiga mwandishi wa habari hakivumiliki, kwani ni sawa na kuipiga na kushambulia taaluma nzima ya wanahabari.

    Alisema tukio la kupigwa Lissa ni mwendelezo wa vitendo vyenye mwelekeo wa kuwazuia waandishi wa habari kutekeleza wajibu wao wa msingi wa kukusanya taarifa na kuuhabarisha umma wa Watanzania.

    “Ifahamike kuwa vitendo vya watu kuwashambulia waandishi wa habari wakiwa kazini siyo tu vinakwaza utendaji wao wa kazi, bali vinadhalilisha utu wao mbele wa jamii inayowazunguka."

    Kibanda alisema huu ni wakati wa waandishi wa habari kuchukua tahadhari wakati wakiripoti matukio ambayo yanaweza kusababisha vurugu na madhara kwao na kwa vitendea kazi kama kamera, magari.

    “ Hakuna habari yenye thamani zaidi ya maisha yako mwandishi wa habari,” alisisitiza.
      
     Kibanda amevitaka vyama vya siasa kama taasisi, viongozi, wanachama na wapenzi wa vyama hivyo, kuacha mara moja vitendo vya kuwashambulia waandishi wa habari kwa sababu zozote zile na kama vitendo hivyo vitaendelea hawatasita kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kususia matukio na mikutano yao.

    “ Tukiona vitendo hivi vinaendelea TEF kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kihabari haitasita kuchukua hatua zaidi dhidi ya vyama husika na ikibidi, kususia matukio na mikutano ya vyama hivyo.

    "Hatutaki kuona waandishi wa habari wanakuwa punching box kwani urafiki wa mwandishi wa habari na mwanasiasa au mchumi ni wa kitaaluma, hivyo hatutamvumilia mtu awaye yeyote atakayeingilia msingi wa wanataaluma ya habari ,” alisema.

    Akihojiwa juu ya taarifa hiyo ya TEF, kwa njia ya simu jana, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema hawezi kujibu kwa simu kuhusu walichokisema wahariri na kudai apewe muda wa kupitia taarifa hiyo ili atoe jibu lenye uhakika.

    Mwishoni mwa wiki, Mwandishi wa UPL, Lissa alipigwa na vijana wa Chadema kwenye makao makuu ya chama hicho wakati mwandishi huyo alipokwenda kupiga picha maandamano ya vijana waliopinga kuondoka kwa katibu wa chama hicho Dk Willbrod Slaa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.