September 03, 2015

  • Sera kumweka Rais madarakani - utafiti Twaweza



    Sera kumweka Rais madarakani - utafiti Twaweza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Twaweza,
    By Raymond Kaminyoge
    Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Twaweza, umebaini kuwa sera ndiyo kigezo muhimu watakachokitumia wananchi kumchagua Rais katika Uchaguzi Mkuu.
    Akitoa matokeo ya utafiti huo jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema asilimia 46 ya wananchi walisema watamchagua Rais kwa sera zake nzuri huku asilimia 17 wakisema kwa maadili na uadilifu wake.
    Akifafanua, alisema utafiti huo wenye jina la 'Je wajua takwimu kuhusu uelewa wa wapiga kura', uliwahoji wananchi 1,335 wa Tanzania Bara. Vigezo vingine na asilimia katika mabano ni utajiri (0) uzoefu wa kisiasa (11), uzoefu wa kitaaluma (3) na ukabila (3).
    Eyakuze alisema ingawa kwenye majukwaa ya kisiasa wagombea wa urais wanapigana vijembe, matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa wananchi wanahitaji zaidi sera ili kumpata Rais bora ajaye.
    Alisema wananchi 82 wanaamini kwamba Uchaguzi Mkuu utakuwa huru na uamuzi wao utaheshimika.
    Alisema asilimia 54 ya watu waliohojiwa wana wasiwasi wa kutokea machafuko ingawa Twaweza haikukusanya takwimu za nani anaweza kuwa chanzo cha vurugu.
    Kuhusu Sheria ya Uchaguzi, Eyakuze alisema asilimia 75 ya walisema wanafahamu kuwa wagombea hawaruhusiwi kugawa fedha kwa wapiga kura ili wawachague, wakati asilimia 25 hawajui.
    Pia, asilimia 76 walisema wanaamini vyombo vya habari vitaripoti kwa usahihi masuala yanayohusu uchaguzi mkuu.
    wakati asilimia 24 walisema vitakuwa na upendeleo kwa sababu ya kupatiwa motisha na fedha.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.