Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
Wafanyabiashara wamekuwa wakitoa shutuma nyingi za kuvurugwa kibiashara wanapokuwa wameenda kufanya biashara katika moja ya nchi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Yamekuwapo malalamiko mengi na miongoni ni kupata hasara wakati wanabadilisha fedha ya nchi moja kwenda nyingine.
Hata hivyo, kuna habari njema kuwa mataifa hayo tayari yameona tatizo hilo na wanaangalia uwezekano wa kufanikisha mpango wa sarafu moja ifikapo mwaka 2024.
Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji wa Wizara ya Afrika Mashariki, Geofrey Mwambe anasema taratibu na vigezo vimeshaainishwa, kinachosubiriwa ni utekelezaji ili kurahisisha biashara miongoni mwa nchi wanachama.
Anakiri kuwa zaidi ya asilimia 20 ya mapato baina ya mataifa hupotea kutokana na gharama za kubadilisha fedha.
"Kiasi hicho ni kikubwa na kinachohimiza kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja. Ilikuwa tuanze majadiliano Julai mwaka huu, lakini tumesogeza mbele kidogo. Nadhani mwezi ujao, mkakati utafanyika kuelekea kwenye utekelezaji wa Itifaki ya Sarafu hiyo," anasema.
Nchi za EAC, anasema zitajadili miswada minne itakayoanzisha taasisi mbalimbali, kama vile ya takwimu, kamisheni ya huduma za fedha na Taasisi ya Fedha (EAMI) itakayokuwa na jukumu la kuanzisha Benki Kuu ya Afrika Mashariki.
Anafafanua kuwa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa itifaki hiyo kila nchi mwanachama itapaswa kukidhi vigezo vilivyokubaliwa, ambavyo ni pamoja na kuwa na deni la taifa lisilozidi asilimia 50 ya pato la taifa, mfumuko wa bei kuwa wa tarakimu moja na ikiwezekana uwe chini ya asilimia tano.
Vigezo vingine ni upungufu wa mapato ya ndani ya kugharamia bajeti za Serikali ili isizidi asilimia tatu kama kuna misaada na asilimia sita kama hakuna na kuwa na uwezo kujitegemea kwa muda bila kuagiza bidhaa nje.
"Kama nchi tatu zitakuwa zimekidhi vigezo hivi, basi mchakato huo unaweza ukaanza kutekelezwa huku milango ikiwa wazi kwa wanachama waliosalia kujiunga muda wowote watakaokuwa tayari kufanya hivyo. Sharti lililopo ni kwamba, hakuna kujitoa kwa sababu ili kutekeleza hilo ni lazima jumuiya ivunjwe," anaeleza.
Suala la kuwa na sarafu ya pamoja ni pana na jumuiya kadhaa barani Afrika zinalenga kufika huko ndani ya muda zilizojiwekea. Kwenye Mkutano wa Pili wa Wadau wa Kodi Afrika (TJN-Afrika) uliofanyika Agosti mwaka huu mjini Machakos, Kenya, wadau wanaeleza kuwa ipo haja ya kuondoa vikwazo vya biashara vinavyochangiwa na tofauti za sarafu.
Mwakilishi wa Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA), Yinka Adeyemi, anaeleza juhudi zinazochukuliwa ili kuhakikisha Afrika inaungana zaidi kwa maendeleo ya wananchi, pamoja na mataifa husika ili kuondokana na utegemezi wa nchi wahisani.
"Kukamilika kwa mchakato huo ndani ya jumuiya, kutawezesha kuanza kwa utekelezaji wa Benki Kuu ya Afrika ifikapo 2028. Haya yote yanafanywa ili kupunguza gharama za biashara pamoja na kurahisisha miingiliano ya nguvukazi na mitaji," anasema Adeyemi.
Katika harakati za kufika huko, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji na ukuaji wa biashara nchini.
Matokeo ya jitihada hizo ni kupanuka kwa soko la bidhaa za ndani na kuongezeka kwa shughuli za uwekezaji kutoka nchi wanachama, ili kuhakikisha Watanzania wananufaika ipasavyo na fursa za kiuchumi na kijamii zinazotokana na mtangamano wa EAC.
Hata hivyo nchi itakayokuwa imejiimarisha katika sekta mbalimbali, inaweza kufaidi vyema faida za sarafu ya pamoja. Hii ni pamoja na kuepuka kujikuta kwenye mtikisiko wa kiuchumi.
Tanzania ndani ya EAC
Ripoti ya miaka 10 ya Wizara ya Afrika Mashariki hapa nchini inaeleza mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika kipindi cha utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuimarisha miundombinu ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka eneo moja kwenda jingine.
Kwa mfano, kwa sasa mtandao wa barabara nchini umeimarishwa na kilometa 35,000 zimejengwa. Kati ya hizo, kilometa 12,786 ni barabara kuu na kilometa 22,214 ni zile za mikoa.
Wakati jitihada zikiendelea kuwekwa ili kuyaunganisha maeneo mengi zaidi, ripoti inaeleza kuwa wizara pia imeboresha huduma za afya, elimu na nishati.
Ripoti hiyo inasema: "Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 112 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2005 hadi vifo 54 mwaka 2015."
Kwa upande wa elimu, mambo kadhaa yamefanywa ili kuifanya Tanzania ilingane au iwe juu ya majirani zake ndani ya jumuiya. Kwa kipindi hicho, inaelezwa kwamba Serikali imeongeza shule za sekondari kutoka 1,745 mwaka 2005 hadi 4,576 mwaka 2015, ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaoendelea na masomo baada ya kuhitimu shule za msingi.
Jitihada hizi zimeenda sanjari na ujenzi wa barabara ambazo zimeongezeka kutoka 1,478 mwaka 2005 hadi 5,114 mwaka 2015, huku uwiano wa walimu, wanafunzi pamoja na ujenzi wa mabweni ukiendelea kuimarishwa.
Wakati hayo yakifanywa, idadi ya vyuo vikuu imeongezeka sambamba na wanafunzi husika. Idadi ya wanafunzi waliopata mikopo imebadilika kutoka 42,729 mwaka 2005 hadi 94,477 mwaka 2014 huku jumla ya Sh1.452 trilioni zikitumika kuwakopesha wanafunzi 560,982 kwa kipindi hicho chote.
Ili kuongeza chachu ya ukuaji wa viwanda vidogo na biashara kwa jumla, huduma ya umeme imeimarishwa kwa kuongeza uunganishaji wa wateja wapya kupitia programu mbalimbali kama vile Mradi wa Umeme Vijijini (REA).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi Christian Msyani anasema kuwa mara gesi itakapoanza kutumika, shirika hilo linalenga kuongeza wateja kutoka asilimia 36 ya Watanzania hadi kufikia asilimia 70.
"Miundombinu imeshaanza kuwekwa sawa. Vituo vya kufua na kupozea umeme wa gesi vinajengwa na pindi vitakapoanza uzalishaji huo, uunganishaji utaongezeka mpaka asilimia 75 kwa mwaka wa kwanza wa matumizi ya gesi," anasema.
Anasema mwaka 2005 ni asilimia 13 ya Watanzania walikuwa wanapata nishati ya umeme lakini kwa sasa wameongeza asilimia 23, jambo ambalo ni la kujivunia.
Anasema nishati ya umeme ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta nyingine kama vile usambazaji wa maji safi ambao imeongezeka kutoka asilimia 40 mwaka 2005 mpaka asilimia 51 mwaka jana.
Wakati sekta hizo zikionyesha mafanikio hayo, Serikali imeimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika Mashariki na Kati kujenga Mkongo wa Taifa wa mawasiliano ili kumepunguza gharama za kisekta na kuchochea ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kusambaza huduma hiyo kwa nchi jirani.
Tanzania kwa sasa imejiwekea lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Hili linatarajiwa kufikiwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kwa kuwajengea uwezo wananchi na hasa wajasiriamali na wafanyabiashara ili waweze kuzitumia fursa zilizopo ndani na nje ya jumuiya.
"Soko letu hivi sasa lina zaidi ya wateja milioni 143 na kwa kuwa hakuna ushuru kwa bidhaa za ndani ni jukumu la wazalishaji kuamua wapi wapeleke bidhaa zao katika ya nchi nne zilizopo," anasema Mwambe.
Umuhimu wa sarafu moja EAC
Mfanyabiashara wa mazao ya kilimo James Butagu ana imani kuwa endapo Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji kwenye miundombinu ya msingi pamoja na kuhakikisha kunakuwa na sera nzuri za kuivutia sekta binafsi kuwekeza mitaji, huenda mafanikio yakapatikana ndani ya muda mfupi ujao. "Kuna wakati huwa napeleka vitunguu Kenya na hata Sudan Kusini. Nina soko la karanga Uganda ambako ninapeleka kilo 500 kila baada ya miezi mitatu," anasema James.
Alisema kuwa, "Tofauti za sarafu zetu huchelewesha mzunguko wa biashara. Ukiwa na shilingi ya Uganda ni lazima utafute duka lenye viwango vizuri vya kubadilishia fedha ili upate ile ya Tanzania au Kenya. Ukiwa mgeni ni suala linaloweza kukusumbua kwa muda."
Anasema inahitaji uzoefu kuweza kubadili fedha kwa faida, iwe kwenye taasisi au kwenye maduka. Mfanyabiashara anaweza kujikuta anapata hasara baada ya kufanya hivyo, licha ya kwamba alikuwa na faida ya kutosha wakati anauza bidhaa yake.
Kulingana na kauli za wachumi, nguvu za ziada ni vyema zikaelekezwa kwenye tofauti za thamani ya sarafu za nchi wanachama, ili kuwanusuru wafanyabiashara wa jumuiya. Endapo benki ya EAC itaanzishwa na kuleta sarafu moja, bila shaka mambo yataenda vizuri zaidi. Ni kutokana na ukweli kwamba suala la fedha halitawaumiza wafanyabiashara, hivyo kuondoa hofu ya kusafirisha bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment