September 25, 2015

  • BAJAJI YAUA WATATU NA NAKUJERUHI WENGINE NANE-MBEYA


    BAJAJI YAUA WATATU NA NAKUJERUHI WENGINE NANE-MBEYA
    Watu watatu wamekufa papo hapo na wengine wanane kujeruhiwa baada ya bajaj mbili walizokuwa wakisafiria kugonga lori aina ya Fuso na nyingine kupinduka katika matukio tofauti mkoani Mbeya.


     
    Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi, alisema katika tukio la kwanza, watu wawili walikufa papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa baada ya bajaj waliyokuwa wakisafiria kugonga lori aina ya Fuso kijiji cha Hatwelo kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini. Kamanda Msangi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 11:00 jioni. Aliwataja watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Abillah Philemon (17), mkazi wa Ilemi jijini Mbeya na Baraka Seleman (23), mkazi wa Simike jijini hapa.
     
    Aliitaja bajaj iliyosababisha ajali hiyo kuwa ni yenye namba za usajili MC 276 APL iliyokuwa ikiendeshwa na marehemu Philemon ambayo iligonga lori lenye namba za usajili T588 AMR aina ya Mitsubish Fuso ikiendeshwa na Emmanuel Francis (35).
     
    Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa bajaj.
     
    "Majeruhi wa ajali hiyo wanatibiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo," alisema Kamanda Msangi. Katika ajali ya pili, Kamanda Msangi alisema mtu mmoja mkazi wa Tewele, Nakonde nchini Zambia, Freddy Ainkala (67), amekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa baada ya bajaj waliyokuwa wamepanda kuacha njia na kupinduka.
     
    Kamanda Msangi aliitaja bajaj hiyo kuwa ni yenye namba za usajili MC 630 AFC iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika na kwamba ajali hiyo ilitokea juzi saa 9:00 alasiri katika kijiji cha Nkangamo tarafa ya Ndalambo wilayani Momba. Alisema majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Kituo cha Afya Tunduma kwa matibabu na mwili wa marehemu Ainkala umehifadhiwa hospitalini hapo. Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Magreth Ntambo (52) na Anastazia Nyamungala (55), wakazi wa Kakozi, Nakonde nchini Zambia.
     
    Kamanda Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa bajaj na kwamba baada ya ajali kutokea, dereva alikimbia.
     
    Wakati huo huo, mtu mmoja amekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa baada ya basi la Sai Baba walilokuwa wakisafiria kugonga lori lililokuwa limeegeshwa kando kando ya barabara eneo la mlima Nyoka kata ya Nsaraga jijini Mbeya.
     
    Kamanda Msangi, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 4:00 usiku wakati basi hilo lenye namba za usajili T 668 BLD likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Sumbawanga. Kamanda Msangi alisema basi likiwa katika mwendo wa kasi, liligonga lori lenye namba za usajili T 771 ATV lenye tela lenye namba za usajili T 771 AUU aina ya Scania lililokuwa limeharibika na kuegeshwa kando kando ya barabara.
     
    Alifafanua kuwa aliyepoteza maisha alikuwa ni utingo wa basi hilo ambaye jina lake halijafahamika sambamba na majina ya majeruhi hao wawili.
     
    Kamanda Msangi alisema majeruhi wa ajali hiyo walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya ambako wanaendelea kupatiwa matibabu na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo.
     
    Aidha, Kamanda Msangi alisema dereva wa basi hilo alikimbia baada ya ajali na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.
     
    Kamanda Msangi alitoa wito kwa madereva kuwa makini waendeshapo vyombo vya moto barabarani ili kuepuka ajali za kuzuilika.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.