September 27, 2015

  • Wahadhiri UDOM kugoma, wadai mishahara



    Wahadhiri UDOM kugoma, wadai mishahara

    WAHADHIRI takriban 800 waliopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameazimia kutoingia madarasani kufundisha kuanzia Novemba 2 mwaka huu mpaka hapo serikali itakaposhughulikia suala la muundo mpya wa mishahara.

    Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma wa UDOM (Udomasa), Gerald Shija alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya mkutano mkuu wa wanataaluma hao uliofanyika Septemba 21 mwaka huu.

    Amesema kwa pamoja wameazimia na kutoa msimamo huo mpaka hapo serikali itakapotekeleza.

    Kwa mujibu wa Shija alidai kuwa Rais alitoa taarifa kupitia vyombo vya habari Agosti 22 mwaka 2013 ambao uliagiza muundo huo uanze kutumika Julai Mosi mwaka huu lakini mpaka sasa haujaanza.

    Amesema kumekuwepo na mishahara isiyofanana kwa watu wenye elimu inayofanana na kufanya kazi inayofanana na hivyo kutofautiana na sera ya Serikali inayoelekeza kuwa watu wenye elimu inayofanana kulipwa mishahara inayofanana.

    Shija amesema wanaamini kuwa muundo huo wa utumishi ulioanishwa na wanataaluma ndio muundo bora ukilinganisha na muundo unaotumika sasa hivi.

    Aliiomba serikali kutekeleza muundo huo ili kuondoa kero ambazo zilibainishwa kwa Rais, hali iliyomfanya aagize uanzishwaji na utekelezwaji wa muundo huo.

    Aidha amesema hivi sasa hawana imani na viongozi wa serikali kutokana na kutotekeleza muundo huo katika kutatua kero za muundo uliopo hivi sasa.

    "Ucheweleshwaji wa muundo huu umekuwa ukikwamishwa na Hazina, Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na Utumishi wa umma ambapo wamekuwa wakitupiana mpira," amesema Shija.

    Hata hivyo amesema mnamo Desemba 11, 2014, Ofisi ya Msajili wa Hazina ilitoa waraka kuagiza Vyuo kupitia Ofisi za rasilimali watu kuzingatia utaratibu ulioanishwa katika muundo na wanataaluma ikiwemo masuala ya vyeo na kuajiri kwakuzingatia vigezo na kuwapanga watumishi wanataaluma.

    Naye Katibu Mkuu wa Umoja huo, Lameck Thomas amesema kuwa muundo huo ulilenga kuweka usawa wa maslahi ya watendaji wa Vyuo vikuu na Vyuo vya Umma na vyuo vikuu vishiriki ili wawe sawa lakini hakuna kilichotekelezwa.

    "Kwa kweli nieleze kwa masikitiko makubwa na tusingependa tufikie hatua hii lakini serikali ndio imetufanya tufikie hapa, tutahakikisha tunapigania muundo huu hadi tupate haki zetu kwani ni nyenzo sahihi lakini tatizo la kulipwa mishahara tofauti kwa wahadhiri lipo katika Chuo Kikuu cha Dodoma tofauti na vyuo vingine," amesema Thomas.

    Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Utendaji ya Udomasa, Mandela Peter amesema bora muundo huo uje ili kuleta usawa kutokana na kutofautiana kwa kiasi kikubwa mishahara kwa wahadhiri wa UDOM na vyuo vingine kama vile Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM).

    "Yaani ukiangalia katika vyuo vya UDSM, Sokoine, Mzumbe ukilinganisha na UDOM kuna tofauti kubwa kati ya Sh. 700,000 hadi 1,000,000 kwa mshahara anaopokea mhadhiri msaidizi, sasa hapo utaona kutokana na tofauti hiyo ni bora muundo huu uanze kutekelezwa ili tuwe sawa," amesema Mandela.

    Aidha Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) katika chuo hicho, Nashon Maisori aliiomba serikali kutopuuza madai hao kwani wasipoyapatia ufumbuzi watasababisha zaidi ya wanafunzi 18,000 kuathirika kutokana na hali hiyo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.