HATIMAYE mradi wa Mabasi            Yaendayo Haraka (BRT) katika jiji la Dar es Salaam unatarajiwa            kuanza Oktoba 2 mwaka huu kwa njia moja.
        Aidha, wamiliki wa magari,            pikipiki na baiskeli ambao watakutwa wakitumia barabara ya            mabasi ya haraka, kama maegesho watapewa adhabu kali ya faini            au kifungo gerezani.
        Hayo yalibainishwa jana na            Ofisa wa Fidia wa Wakala wa Usafiri Haraka wa Mabasi (DART),            Deo Mutasingwa baada ya wafanyakazi wa Wakala wa Barabara            nchini (TANROADS) kufanya ziara ya kujionea jinsi huduma hiyo            itakavyotolewa.
        Alisema huduma hiyo ambayo ni            ya muda na kufanywa kwa kipindi cha miaka mwili, itakayofanywa            na Kampuni ya UDA, itaanza Oktoba 2 mwaka huu kwanjia moja ya            kutoka Kimara hadi Kivukoni yenye urefu wa kilomita 20.9.
        Alisema kwa njia za barabara            ya Msimbazi kutoka Faya hadi Kariakoo-Gerezani na sehemu ya            barabara ya Kawawa kuanzia Magomeni hadi eneo la makutano ya            Morocco jijini Dar es Salaam, itaanza kutumika baada ya            miundombinu yake kukamilika.
        Alisema katika mradi huo wa            muda wa miaka miwili, mabasi 100 yatakayoendeshwa na madereva            200 yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo.
        Aidha, Mutasingwa alisema            wenye magari, pikipiki baiskeli ambao watakutwa wakitumia            barabara hizo au kuegesha vyombo vyao watatozwa faini ya kati            ya sh 250,000 hadi sh 300,000 au kifungo cha miaka miwili jela            au adhabu zote kwa pamoja.
        " Tumekuwa na changamoto kwa            watumiaji wengine wa barabara, jambo ambalo linaleta uharibifu            na pia kuingilia safari. Tumeshazungumza na wenzetu wa            halmashauri kushughulikia hili, hivyo kuanzia mwezi ujao            atakayekutwa akitumia barabara hizo au kupaki chombo chake            adhabu kali itakuwa juu yake," alisema.
        Alipoulizwa suala la nauli,            alisema hilo liko kwenye mchakato kati ya DART, wamiliki wa            mabasi na walaji lengo ni kuja na nauli ambayo haitamuumiza            mwananchi lakini pia yule anayeendesha apate faida.
        Alisema wakati utoaji wa            huduma hiyo utakapokuwa kamili, watanzania takribani 300,000            watahudumiwa kwa siku.
        Msimamizi wa Mifumo wa DART,            Junn Mlingi alisema vituo vikuu vya mabasi vitakuwa na            miundombinu ya kumwezesha mtumiaji yeyote kama ni mgeni,            mlemavu wa viungo kuona au kusikia kuweza kupata huduma            hiyokwani kutakuwa na matangazo ya sauti na maandishi.
        Alisema mabasi hayo yatakuwa            yakiendeshwa kwa kilomita 50 kwa saa kwa mwendo wa kasi na            kilomita 24 kwa saa kwa mwendo wa wastani."
        
0 comments:
Post a Comment