Miaka 130 iliyopita, ulifanyika mkutano wa Berlin ambao ndiyo ulikuwa mwanzo wa ukoloni barani Afrika, ulimalizika. Ni Katika mkutano huo ambapo wakoloni waliweka mipaka ya makoloni yao barani Afrika.
Tarehe 26 Februari mwaka 1885 ilikuwa siku ya mwisho ya mkutano wa Berlin ambao ulileta mabadiliko ya kudumu barani Afrika. Wawakilishi wa nchi 13 za Ulaya na wengine kutoka Marekani walikutana kwenye ofisi ya Kansela wa Ujerumani Berlin kugawa maeneo ya bara la Afrika.
Katika chumba cha mkutano palikuwa na ramani ya Afrika yenye urefu wa mita tano. Ilionyesha milima, maziwa na mito mbali mbali iliko. Ni mkutano uliokuwa umeitishwa na Kansela Otto von Bismarck na lengo lilikuwa kuwapa wakoloni maeneo ya kutawala. Hata hivyo hakuna hata mwakilishi mmoja wa Afrka aliyealikwa kwenye mkutano huo. Miaka michache baada ya mkutano huu nchi zote za kiafrika, isipokuwa tu Ethiopia na Liberia, zilikuwa chini ya utawala wa kikoloni.
Profesa wa historia katika chuo kikuu cha Nasarawa nchini Nigeria Olayemi Akinwumi, anasema katika mkutano huo maeneo yaligawiwa kiholela, na hilo limekuwa na athari zake hadi leo.
"Sisi watafiti wa masuala ya Afrika, wengi wetu tunaamini kuwa chanzo cha migogoro mingi inayoendelea Afrika kwa wakati huu ni mkutano wa Berlin wa mwaka 1884/1885. Waliligawa bara la Afrika bila kujali historia ya jamii zilizokuwepo." Amesema Akinwumi.
Jamii zilitenganishwa
Kwa sababu hiyo, hata makabila yalitenganishwa na hivyo sehemu ya watu wa jamii moja kuwa kwenye nchi fulani huku wenzao wakijikuta nchi nyingine. Hata njia za biashara zilikatishwa kwa kuwa haikuruhusiwa tena kufanya biashara na watu wa koloni jingine. Utafiti unaonyesha kwamba maeneo ambapo jamii zilitengwa kwa mipaka ya nchi yanashuhudia migogoro mingi zaidi.
Katika miaka ya 1960 nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru na hivyo kulikuwa na fursa ya kufuta mipaka ya nchi iliyowekwa na wakoloni. Lakini kama anavyosema mtafiti wa Historia ya Afrika katika chuo kikuu cha Dresden nchini Ujerumani, Michael Pesek.
'Idadi kubwa ya wanasiasa wa Kiafrika mwaka 1960 walisema, "mkifanya hivyo mtakuwa mnaanzisha balaa". Ni kweli kwamba katika miaka 80 iliyopita Afrika imeshuhudia migogoro mingi baina ya nchi na nchi lakini ni mara chache kabisa migogoro hiyo ilihusiana na masuala ya mipaka", amesema mtafiti huyo.
Fidia kwa Afrika ni kama ndoto
Mwaka 2010, miaka 125 baada ya mkutano wa Berlin, wawakilishi wa nchi Kiafrika walikwenda Berlin kudai kulipwa fidia na kuombwa msamaha kwa sababu ya athari za ukoloni kwa nchi zao. Katika tamko lao waliutaja uamuzi wa kuigawanya Afrika bila kuzingatia sheria wala utamaduni wa Kiafrika kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Lakini hakuna chochote kilichotokea.
Mtafiti Michael Pesek ameendelea kusema, "Tunazungumza sana kuhusu fidia kwa ajili ya biashara ya watumwa ama mauaji ya Wayahudi. Lakini ni mara chache utasikia wakizungumzia uhalifu uliofanywa na Wakoloni walipokuwa barani Afrika kwa zaidi ya miaka 100,"
Naye Olayemi Akinwumi kutoka Nigeria amekubaliana na maoni hayo ya mwenzake wa Ujerumani, akisema haamini kama utakuja kuwepo muda wa kufikiria aina yoyote ya fidia kwa Afrika.
Ni muhimu kuashiria kwamba, wanaafrika wanatakiwa wawe na uchungu wa kukumbuka matukio ya zamani na kujifunza kupitia matukio hayo, inawapasa kufahamu na kukumbuka dhulma, uadui, na uhalifu uliyofanywa na wakoloni dhidi yao, wanapaswa wajitegemee badala ya kuwategemea watu waliowadhulumu na kuwanyanyasa.
TAFAKURI.COM
0 comments:
Post a Comment