September 02, 2015

  • SIASA ZA KEJELI‭, ‬MATUSI TUTAISHIA GEREZANI‭!‬



    SIASA ZA KEJELI‭, ‬MATUSI TUTAISHIA GEREZANI‭!‬
    KWENU Watanzania wenzangu. Bila shaka kila mmoja kwa sasa anaendelea na majukumu yake huku siasa ikiwa imetawala kila sehemu. Kuanzia maofisini, vijiweni, kwenye usafiri wa umma, baa, vyuoni na kila sehemu ambayo inakuwa na mkusanyiko.
    Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu naendelea vizuri na majukumu yangu ya kila siku likiwemo hili la kuwaandikia barua watu mbalimbali maarufu na wasio maarufu.Leo nimeona niwaandikie Watanzania wote kwa ujumla maana nimeguswa na hali ya kisiasa inayoendelea nchini, siasa ndiyo kila kitu kwa sasa.
    Dhumuni la kuwaandikia barua hii ni kutaka kuwakumbusha kwamba katika kipindi hiki cha uchaguzi, tunapaswa kutofautiana kiitikadi lakini tuepuke mihemuko iliyopitiliza kiasi cha kuanza kutukanana 'live' au mitandaoni.
    Ndugu zangu, uchaguzi utapita Oktoba 25, mwaka huu. Maisha yataendelea kama kawaida. Maendeleo ya mtu mmojammoja mbali na kuwezeshwa na serikali kwa namna moja au nyingine, lakini jitihada binafsi zinahitajika ili uweze kupiga hatua.
    Hakuna kiongozi atakayekuletea mafanikio wakati wewe hujishughulishi. Kilichonisukuma zaidi kuwaandikia barua hii, nafahamu juu ya matusi, kejeli ambazo mmekuwa mkizifanya katika mitandao ya kijamii na hata mnapokuwa vijiweni.
    Tunachafuana, tunawachafua viongozi wetu tena wakati mwingine hawana kosa lolote. Tunatengeneza chuki. Chuki hii itatugharimu sasa na hata baada ya uchaguzi. Tuwe makini sana kipindi hiki.
    Taarifa kwa Watanzania ambao wamekuwa na tabia ya kutukanana mitandaoni, sheria mpya ya mitandao imeanza kufanya kazi jana Septemba 1.Hii ni sheria ambayo hakika tusipokuwa makini, wengi tutajikuta katika mikono ya sheria.
    Mtu anashiriki kusambaza kejeli kwa mtu ilimradi tu amkomoe kutokana na chuki zake binafsi, si ustaarabu jamani.
    Kutoijua sheria hakuzuii sheria kuchukua mkondo wake. Tujielimishe kupitia mitandao na sehemu nyingine ambapo sheria hii inapatikana.
    Niwatakie maandalizi mema ya uchaguzi na Mungu aibariki Tanzania!
    Ni mimi katika ujenzi wa taifa,
    ............
    Erick Evarist


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.