Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema serikali yake haitamshtaki askari polisi ikiwa ataua jambazi mwenye silaha.
Mgombea                huyo alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa kampeni                uliofanyika kwenye  uwanja wa Mashujaa, mjini Mtwara.
        "Katika                  serikali yangu askari akimpiga jambazi mwenye silaha kwa                  risasi hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia vituo                  vya polisi, mbona hawavamii kambi za jeshi, Jeshi la                  Kujenga Taifa au Ukonga FFU?, wanaona polisi wana                  nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua," alisema Magufuli.
        Mgombea                huyo wa urais wa CCM pia aliahidi kwamba ataboresha                maslahi ya askari polisi ili wafanye kazi zao kwa ufanisi                na wakiwa na furaha.
        Kadhalika,                aliahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais, atahakikisha                makusanyo ya kodi kwa mwezi yanaongezeka mara mbili kutoka                yanayokusanywa sasa ya Sh. bilioni 900 hadi Sh. tirioni                1.8.
         "Serikali                  ya awamu ya nne ilikuwa inakusanya mapato ya kila mwezi                  Sh. bilioni 300, lakini sasa yameongezeka hadi kufikia                  Sh. bilioni 900 kwa serikali ya Magufuli nitahakikisha                  mapato yanafikia mara mbili ya haya," alisema Dk.                Magufuli.
        Katika                hotuba yake iliyoanza saa 10:12 jioni, mgombea huyo                aliyekuwa akishangiliwa na umati uliojitokeza kumsikiliza                sera zake, aliahidi pia kuwapatia wananchi maendeleo.
        Alisema                wingi wa watu waliojitokeza kumsikiliza unadhihirisha kuwa                Watanzania wanahitaji mabadiliko ya kweli ambayo yataletwa                na CCM.
        "Kwa                  idadi hii kubwa ya watu inadhihirisha kuwa wana Mtwara                  na  Watanzania kwa ujumla sasa wanataka mabadiliko na                  siyo kusema mabadiliko tu bali ya kweli na ndiyo maana                  urais. Nilipoomba urais sikuwa najaribu, nimekuwa mbunge                  kwa miaka 20 hivyo naifahamu vizuri serikali  na                  nafahamu mahali serikali ilipolegea, nichagueni mimi                  niwatumikie," alisema                Dk. Magufuli.
        Aidha,                aliahidi  kujenga barabara zilizosalia kutoka Mtwara-                Newala -Tandahimba hadi Masasi. Mbali na hilo, aliwaahidi                wananchi wa Mtwara kuwa watajengewa bandari kubwa kama za                Dar es Salaam na Tanga pamoja na viwanda.
        "Serikali                  ya Magufuli ni ya viwanda, serikali ya Rais Kikwete                  imejenga kiwanda cha saruji kinachomilikiwa na Dangote,                  mkinichagua nitamwaga viwanda vingi zaidi ili vizalishe                  na kutoa ajira kwa watu wengi," alisema na                kushangiliwa.
        Awali                jana akizungumza katika mkutano wa kampeni wilayani                Tandahimba, mkoani Ruvuma kabla ya kwenda Mtwara, Dk.                Magufuli, alisema anatambua shida wanaozopata wakulima wa                korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na kuahidi                kuzipatia ufumbuzi.
        Wakulima                wa zao hilo mikoa ya Kusini mwa Tanzania wamekuwa                wakiulalamikia utaratibu huo kwa muda mrefu, wakisema ni                wa kinyonyaji.
        Dk.                Magufuli pia aliahidi kutatua matatizo ya  wakulima wa                korosho kucheleweshewa fedha, kulipwa nusu na uhaba wa                dawa na pembejeo kuchelewa.
        Akizungumza                katika mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali ya                wilaya ya Tandahimba, Dk. Magufuli alisema pia kuna                wabadhilifu wa fedha za wakulima ndani ya vyama vya                ushirika na kwamba serikali yake itaondoa kero hizo ili                wakulima wanufaike na kilimo hicho.
        "Nimesomea                  Shahada ya Uzamivu ya masuala ya korosho, hayo ndiyo                  masuala yangu, mnatakiwa kunufaika na korosho na pia                  maganda yake yanaweza kutengeneza gundi na vitu vya                  kuzuia kutu, tutaongeza viwanda vikubwa vya korosho ili                  kuongeza thamani ya mazao yenu mnufaike," alisema.
        Alisema                atahakikisha bei ya korosho inaongezeka kutoka ya sasa ya                Sh. 300 kwa kilo moja.
        "Hapa                  Tandahimba kuna vyama vingi vya ushirika lakini                  havifanyi vizuri, tutaviimarisha vihudumie wakulima                  ipasavyo walipwe fedha bila kukopwa, wanaodokoa fedha                  nitawadhibiti," alisema.
        Akizungumzia                gesi, alisema Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi                kama gesi, mafuta, wanyama, madini na nyingine nyingi.
        Alisema                uchumi wa gesi utawezesha viwanda vingi kujengwa na watu                kupata ajira.
        Dk.                Magufuli alisema gesi ni lazima inufaishe wananchi wa eneo                husika kabla ya kunufaisha wengine.
        "Gesi                  imetoka hapa lazima wakazi wa hapa mnufaike kwanza,                  huwezi kuwa na gesi inufaishe wengine, mpate umeme wa                  uhakika, ajira na uchumi wetu ubadilike," alisema.
        Aidha,                aliwatahadharisha wananchi hao dhidi ya nchi za Ulaya                zinazonyemelea utajiri wa Tanzania na kwamba wasiruhusiwe                kuwagawa Watanzania.
        "Siku                  zote vita ya panzi ni furaha ya  kunguru, mtu akihubiri                  ugomvi, chuki na kutokuwa na amani siyo mwenzetu,                  msikubali kuchonganishwa na wanaotumika na wanaozitamani                  rasilimali zetu," alisema.
        Alisema                kugunduliwa kwa  gesi kutawezesha ujenzi wa viwanda                vidogo,  vya kati na vikubwa kwa kuwa rasilimali hiyo                inaweza kufanya mambo mengi ikiwamo Tanzania kuwa na                kiwanda cha ndege.
        Alisema                kwa sasa kiwanda cha saruji cha Dangote kinaendelea                kujengwa na kwamba pamoja na vingine kitasaidia bei ya                vifaa vya ujenzi kupungua bei na kurahisisha wananchi                kujenga nyumba nzuri na kisasa na vijana kupata ajira.
        
0 comments:
Post a Comment