Akizungumza na wananchi wa Mkuranga wilayani Kisarawe, Duni Haji alisema Serikali ya CCM imeshindwa kuondoa tatizo la ajira na hivyo kusababisha vijana kujitumbukiza kwenye vitendo hivyo vya kihalifu, kama kuunda vikundi vya panya road.
Alisema tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, CCM iliweka kwenye ilani yake nia ya kuondoa umaskini, lakini imeshindwa kutekeleza hadi leo na hivyo kusababisha vijana wengi kutopata ajira na kuingia kwenye uhalifu.
"Walikuwa wapi kuondoa umaskini kwa miaka zaidi ya hamsini waliyotawala, leo wataondoaje," alisema Haji kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya watu kwenye Uwanja wa Godown, Mkuranga Mjini.
Kuhusu kauli ya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ya kuwataka polisi kutoogopa majambazi na ikiwezekana kuwaua, Duni Haji alisema wangeanzia kwa majambazi walioko ofisini.
"Kuna watu wanakaa ofisini ambao wamelifikisha Taifa hapa lilipo," alisema Duni Haji. Mfano wale majambazi waliochukua fedha za escrow, tena nasikia wengine wako Ikulu. Kama ni kuua majambazi, basi waanzie hao walio Ikulu."
Alisema kutokana na kauli hiyo, Dk Magufuli anatakiwa kuogopwa na hafai kuwa Rais.
"Hivi hajaingia Ikulu anasema maneno hayo, akiingia itakuwaje? Hao panya road watapona?" alihoji.
Duni Haji, ambaye alihama CUF na kujiunga na Chadema katika mkakati maalum baina ya vyama hivyo viwili wa kujiandaa kushika dola, aliwashangaa wakazi wa Mkuramga kwa kuendelea kunywa maji ya kinyesi, akisema matatizo ya maji yanasababishwa na Serikali ya CCM
Awali, mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoani Dar es Salaam, John Guninita alimuelezea Dk Magufuli kuwa ni mtu asiyefaa kupewa urais, akimtuhumu kuhusika katika uuzwaji wa nyumba za Serikali na ujenzi wa barabara zilizo chini ya kiwango.
0 comments:
Post a Comment