Kikwete                      aliyasema hayo jana wakati akiwaaga wananchi wa                      Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na kumtaka                      Lissu amtaje mwenye Richmond.
              "Endapo                      Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond,                      nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe," alisema                      Kikwete.
              Kabla                      ya mkutano huo, Rais Kikwete alifungua jengo la                      Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) ambalo                      limejengwa kwa Sh7 bilioni.
              Akifungua                      jengo hilo, aliwaomba wawekezaji na mifuko ya                      kijamii kuiga mfano wa NSSF kwa kuwekeza katika                      sekta ya majengo kwa kuwa yanapendezesha mji.
              Kadhalika,                      Rais Kikwete alizindua jengo la Shirika la Nyumba la                      Taifa (NHC) pamoja na nyumba 36 za bei nafuu                      zilizopo katika eneo la Mlole, Kigoma Mjini.
              Richmond
              Suala                      la Richmond imekuwa moja ya ajenda za CCM katika                      kampeni za urais hasa baada ya Waziri mkuu wa zamani                      Edward Lowassa aliyejiuzulu wadhifa huyo kwa kashfa                      hiyo kuhamia upinzani.
              Kila                      sehemu ambako mgombea urais wa CCM anakwenda, suala                      hilo limekuwa likiibuliwa, huku Lowassa akisema yeye                      hakuhusika, bali alijiuzulu kuiokoa Serikali                      isianguke kwa kuwa ulikuwa uamuzi wa wakubwa.
              Mgombea                      urais wa CCM, Dk John Magufuli amekuwa akienda mbali                      zaidi akisema akichaguliwa ataanzisha mahakama                      maalumu ya kushughulikia mafisadi wanaosababisha                      umaskini nchini.
              Bashe                      ataka mahakama ya mafisadi mapema
              Wakati                      Magufuli akiahidi mahakama hiyo, mgombea ubunge                      Jimbo la Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe alimtaka                      mgombea huyo jana kuiwahisha mapema iwezekanavyo                      akiingia Ikulu la sivyo atakuwa akihoji bungeni kila                      mara.
              Bashe                      alisema akipatiwa ridhaa na wakazi wa jimbo hilo                      kuingia bungeni hatakuwa mbunge wa "ndiyo mzee"                      badala yake atakuwa akiisumbua Serikali mara kwa                      mara likiwamo suala la kudhibiti ufisadi nchini.
              "Umesema                      utafungua mahakama ya mafisadi na majizi...                      nikuhakikishie waziri wako wa sheria utakayemteua                      ajue atakutana na mtu anaitwa Bashe, kila akiingia                      bungeni nitakuwa namuuliza kila mara upo wapi                      muswada wa sheria ya kuanzisha mahakama maalumu ya                      mafisadi na majizi," alisema Bashe na kushangiliwa.
              "Ni                      lazima tufike mahali Taifa hili tuache kuwa watu wa                      porojo....Taifa hili siyo maskini kuna wezi wapo                      bandarini. Najua saa hizi wanatafuta biashara                      nyingine."
              Mgombea                      huyo alisema wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea                      wa urais, kulikuwa na makundi ndani ya chama akiwamo                      na yeye lakini baada ya kumpata, Dk Magufuli tofauti                      zimekwisha.
              Bashe                      alikuwa miongoni mwa vinara wa kumuunga mkono                      mgombea wa urais wa mwamvuli wa Ukawa kupitia                      Chadema, Edward Lowassa wakati akiomba ridhaa ya                      kuteuliwa na CCM kabla ya kuhamia upinzani.
              Hata                      hivyo, jana alisema hataihama CCM kwa kuwa yeye na                      chama hicho hawakukutana barabarani na kwamba ni                      muumini wa mabadiliko ndani ya chama hicho.
              Huku                      akigusia tuhuma zilizowahi kuvuma za yeye kuwaambia                      wananchi wamchague yeye halafu urais wampigie                      Lowassa, Bashe alisema wanaNzega watampigia kura Dk                      Magufuli asilimia zote na zikipungua hazitazidi                      asilimia tano.
              Bulembo                      amvaa Sumaye
              Mwenyekiti                      wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo                      amemvaa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na                      kumtaka aache kuchukua mshahara na kurudisha walinzi                      wanaomlinda iwapo ataendelea kukitusi chama hicho                      kwamba hakijafanya chochote tangu uhuru.
              Akiwahutubia                      wakazi wa Nzega jana, Bulembo alisema maisha yote ya                      kiongozi huyo na familia yake yametengenezwa na CCM                      lakini anashangaa kuona sasa anasimama kwenye                      majukwaa na kuwaeleza wananchi kuwa CCM haijafanya                      kitu.
              "...Analipwa                      asilimia 80 ya mshahara wa Waziri Mkuu aliyepo                      madarakani, Mizengo Pinda. Mpaka leo bado ana ulinzi                      na anahudumiwa na  Serikali hii. Kwa kupitia jukwaa                      hili la Nzega hebu Sumaye aache mshahara huo,                      arudishe walinzi awe raia kama sisi," alisema                      Bulembo.
              Aliendelea                      kurusha vijembe kwa kiongozi huyo akidai kuwa                      alinyang'anya ardhi ya wana ushirika wa Mvomero                      mkoani Morogoro baada ya kutetereka.
              Magufuli                      na michango ya shule
              Dk                      Magufuli jana aliendelea na kampeni zake mkoani                      Tabora na kuahidi kuwa akiingia madarakani atafuta                       michango yote shuleni inayosababisha baadhi ya                      wazazi washindwe kuwapeleka watoto shule.
              Alisema                      anatambua kuwa baada ya sera yake ya elimu bure                      kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne kuanza                      kutekelezwa iwapo atachaguliwa, kuna baadhi watu                      wataanzisha michango isiyo na maana na kwamba                      atawashughulikia.
              "Kuna                      mambo ya kuwaambia wazazi peleka dawati, peleka                      dawati na hata kama mtoto wa kwanza akishamaliza                      shule, ukimpeleka mwingine lile dawati hulikuti.                      Ninafahamu haya yote nitayashughulikia lakini pia,                      hakuna sababu shule kukosa madawati au viti wakati                      ipo karibu na miti, mbao zipo, haya yote tutaangalia                      tukizingatia masilahi ya walimu wetu," alisema Dk                      Magufuli.
              Akiwa                      Bukene wilayani Nzega, Dk Magufuli aliwatahadharisha                      makandarasi wazembe walioshindwa kukamilisha miradi                      yao kwa wakati akiwataka kufanya hivyo kabla ya                      Oktoba 25 kwa kuwa yeye ni kiboko yao.
                
CHANZO MWANANCHI
            CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment