·                     Tanzania imetimiza masharti yote ya kupatiwa raundi ya            pili ya fedha za maendeleo kutoka Shirika la Maendeleo ya            Milenia la Millennium Challenge Corporation            (MCC) la Marekani na itaanza kupata na            kunufaika na mabilioni hayo ya fedha baada ya wajumbe wa Bodi            ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo            chini ya Mpango wa MCC-2.
        Habari hizo njema zimetangazwa Jumamosi,            Septemba 26, 2015, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa            Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, na Mtendaji Mkuu            wa MCC, Bi. Dana J. Hyde katika mkutano uliofanyika katika            Hoteli ya JW Marriot Essex House, New York, na kuhudhuriwa na            watumishi waandamizi wa MCC akiwamo Bwana Kamran Khan, Makamu            wa Rais wa Operesheni za MCC. Rais Kikwete yuko New York            kuhudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja wa            Mataifa. 
        "Hongera Mheshimiwa Rais kwa sababu                nchi yako, Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata                fedha nyingine chini ya mpango wa MCC - 2, ikiwa ni pamoja                na uongozi wa MCC kuridhika kuwa Tanzania inachukua hatua                za dhati kupambana na rushwa," Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete na            viongozi wengine wa Tanzania akiwamo Waziri wa Nchi za Fedha            wa Zanzibar, Mheshimiwa Yusuf Omar Mzee.
        Bi. Hyde amemwambia Rais Kikwete kuwa Bodi            ya MCC, katika mkutano wake wa Septemba 17, mwaka huu na chini            ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bwana            John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa            kimebakia katika masharti ya kupata fedha za MMC kuwa ni kweli            Tanzania inakabiliana ipasavyo na rushwa na kuchukua hatua            stahiki kukabiliana na janga hilo la rushwa.
        MCC imetoa taarifa ya kuthibitisha kuwa            Tanzania imetimiza masharti ya kuiwezesha kufaulu kupata            raundi ya pili ya fedha za maendeleo na pia imetoa taarifa ya            kuthibitisha kuwa ni kweli Bodi ya MCC imeridhishwa na hatua            zinazochukuliwa kukabiliana na rushwa.
        Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na            wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na            nchi inayopewa fedha hizo na pia nchi husika hupewa uhuru wa            kuchagua aina ya miradi ya maendeleo ambayo inaitaka            igharimiwe na fedha hizo.
        Miongoni mwa wajumbe wengine wa Bodi ya            MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu            Mwenyekiti wa Bodi, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani            duniani, Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa            la Marekani (USAID), nafasi ambayo kwa sasa anaikaimu Bwana            Alfonsi Lenhardt, Mtendaji Mkuu wa MCC Bi. Hyde na Rais wa            Taasisi ya International Republican Institute (IRI) Balozi            Mark Green. 
        Mabalozi Lenhardt na Green walikuwa            mabalozi wa Marekani katika Tanzania wakati wa majadiliano,            upitishaji na utekelezaji wa MCC–1. 
        Bi Hyde amesema sasa linalobakia ni kwa            wajumbe wa Bodi kupelekewa muhtasari wa kuidhinisha mabilioni            hayo kwa Tanzania ambayo chini ya mpango wa uwekezaji wa MCC–2            yatakwenda katika kuboresha huduma za umeme katika Tanzania            ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme katika vijiji vingi zaidi            nchini. Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata            umeme kutoka asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya            asilimia hiyo imetokana na msaada wa MCC-1.
        Chini ya Mpango huo wa pili wa MCC,            Tanzania itapatiwa kiasi cha dola za Marekani milioni 472.8            (sawa na sh. bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha            dola milioni 698 (sawa na sh. trilioni 1.46) ambazo zilitolewa            chini ya MCC-1 basi Tanzania itakuwa imepata jumla ya dola za            Marekani trilioni 2.45 za maendeleo kutoka Marekani katika            kipindi cha miaka 10 tu iliyopita. Fedha za MCC-2 zitaanza            kutolewa mwakani, 2016.
        Kiasi kilichotolewa kwa Tanzania wakati wa            MCC-1 ndicho kilikuwa kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata            kutolewa na Marekani chini ya Mpango huo wa Millennium            Challenge Corporation na kwa kupita MCC-2 Tanzania itakuwa ni            nchi ambayo itakuwa imepata kiasi kubwa cha fedha za maendeleo            chini ya MCC duniani.
        Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1            zilitumika kujenga Barabara za Tunduma-Sumbawanga,            Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga. 
        Aidha, fedha hizo zilitumika kujenga upya            mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na            Morogoro na zilitumika kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa            10 ya Tanzania Bara. 
        Fedha hizo vile vile zilitumika kutandaza            njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi            kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga            barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za            Unguja kwa kiwango cha lami. 
        Imetolewa na:
        Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
        Ikulu,
        DAR ES SALAAM.
        27 Septemba, 2015
        
0 comments:
Post a Comment