September 05, 2015

  • Siri ya CCM na Ukawa kukimbilia Nyanda za Juu Kusini zafichuka



    Siri ya CCM na Ukawa kukimbilia Nyanda za Juu Kusini zafichuka Mgombea urais wa Chadema, Edward          Lowassa na

     Mikoa ya Rukwa, Katavi, Iringa, Mbeya na Njombe imekuwa kimbilio la Taifa wakati wa njaa, lakini wanasiasa wana sababu nyingine ya kuwahishia kampeni zao Nyanda za Juu Kusini ambako kuna kura takriban milioni 3.92.

    Eneo hilo linajumuisha mikoa inayojulikana kama The Big Four, yaani Mbeya, Iringa Ruvuma na Rukwa, ambayo ni maarufu kwa kuzalisha chakula, lakini wagombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wanaliangalia eneo hilo kwa jicho tofauti; linaweza kuamua mshindi wa mbio za urais.

    Dk John Magufuli, mgombea urais wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema walizindulia kampeni zao jijini Dar es Salaam, lakini mara baada ya kuzindua tu walichomoka kuelekea mikoa hiyo.
    Kwa mujibu wa Makadirio ya Idadi ya Wapigakura 2015 yaliyofanywa na Taasisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Mkoa wa Mbeya ulikadiriwa kuwa na wapigakura 1,477,370, Rukwa (472,790), Iringa (524,390), Katavi (271,160), Ruvuma (783,296) na Njombe (392,634).

    Dk Magufuli, ambaye ndiye aliyefungua pazia la kampeni Agosti 23 kwenye viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam, alihamia Mkoa wa Katavi na baadaye Mbeya na Iringa, wakati Lowassa, ambaye alikuwa wa pili kufanya uzinduzi jijini Dar es Salaam, alichomokea mkoani Iringa na baadaye kwenda Njombe, Ruvuma na Rukwa.

    Chama cha ACT-Wazalendo pia kilizindulia kampeni zake Mbagala, na awali kilipanga kufanya harakati zake mikoani kwa kuanzia Mkoa wa Morogoro, lakini jana chama hicho kilitangaza kuwa kinaelekeza nguvu kwanza Mkoa wa Katavi.

    January Makamba
    "Ni ratiba tu. Sisi tunafuata ilivyopangwa," alisema January Makamba, mmoja wa makada wawili walioteuliwa na CCM kuwa wasemaji wa shughuli za kampeni za uchaguzi za chama hicho.
    Makamba alisema kitendo cha chama hicho tawala kuanzia kampeni zake mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hakimaanishi kwamba kinabagua baadhi ya maeneo, bali ni utaratibu waliojiwekea.

    "Maeneo yote ya Tanzania ni sawa na tutahakikisha tunafanya kampeni zetu kila sehemu ya nchi hii na ndiyo maana tunatumia barabara wala siyo usafiri wa anga," alisema Makamba.
    "Kwa kuwa sisi tulikuwa wa kwanza kufungua pazia la kampeni na kuanzia huko, basi na wenzetu wakaamua kutufuata kule tulipoanzia."

    Chadema watetea
    Ofisa habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama hicho kilianza kampeni zake ukanda huo kutokana na mikakati ambayo chama iliweka kwa muda mrefu.
    "Chama chetu kimegawanya kanda 10, ni uamuzi wa chama kupanga kianzie wapi mashambulizi ya kisiasa,"alisema Makene.

    Aliongeza: "Hiyo ni sababu moja lakini sababu kuu iliyotufanya tuanzie kampeni huko, hiyo ni siri ya chama."
    Alizitaja kanda hizo kuwa ni Nyasa, Victoria, Serengeti, Kusini, Magharibi, Kati, Pemba, Unguja, Kaskazini na Pwani.

    Pamoja na maelezo hayo, mikoa hiyo, ambayo hadi sasa ina jumla ya wabunge wanne kutoka vyama vya upinzani, imeonekana kuendelea kuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa katika miaka ya karibuni.

    Katika uchaguzi wa mwaka 2010, vyama vya upinzani vilifanikiwa kuingiza wabunge wanne tu kutoka mikoa yote ya kanda hiyo, lakini kumekuwa na ongezeko kubwa la mwamko wa wananchi kisiasa uliosababisha vyama hivyo kushinda viti vingi vya serikali za mitaa na vijiji.

    Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 2014, CCM ilishinda mitaa na vijiji 9,406, wakati vyama vya upinzani viligawana nafasi 3,211, hilo likiwa ni ongezeko la viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa 2009.

    Mkoani Mbeya pekee, vyama vya upinzani vilishinda zaidi ya mitaa, vitongoji na vijiji 600, ikiwa ni ongezeko kubwa kulinganisha na mwaka 2009.
    Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliohojiwa na Mwananchi kuhusu kitendo cha wagombea hao kuipa kipaumbele mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wameeleza kuwa inatokana na haja ya kuwahi kura kwenye eneo ambalo wanasiasa wanadhani lina wapigakura wengi ambao wanaweza kubadilika baada ya kuhamasishwa.

    Dk Mwakajumulo
    Dk Steven Mwakajumulo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku), alisema mazingira na hali ya kisiasa katika mikoa hiyo yamebadilika kwani asilimia kubwa ya wananchi wake wanaonekana kutotabirika licha ya baadhi yao kuhitaji mabadiliko ya uongozi wa serikali.
    Alisema mwamko huo umesababisha CCM na Ukawa kuanzia maeneo hayo ili kutengeneza ushawishi wa mapema kwa wananchi hao.

    "Idadi kubwa ya wananchi wake wamekuwa na mwamko, na kwa sasa ni miaka mitano tangu uchaguzi wa mwaka 2010, kwa hivyo kila mmoja anataka kuwahi kumiliki wapigakura wa nyanda hiyo ya kusini," anasema.

    "Kikubwa zaidi ni mwamko uliochangiwa zaidi na msingi wake wa kuwa chimbuko la vyama vya wapigania uhuru. Kwa hivyo ni mbinu za kuwahi ngome hiyo. CCM inataka kurejesha heshima yake ya zamani na Ukawa wanataka kuteka kundi linalohitaji mabadiliko, ndiyo maana wameanzia huko."
    Wakati Dk Mwakajumulo akizungumzia nia ya wanasiasa kuwahi kujenga ngome kwenye eneo hilo, Profesa Gaudence Mpangala, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, anaona sababu kubwa ni kukosekana kwa uimara wa mgombea licha ya kuwepo upepo wa mabadiliko.

    "Kwa kuwa wagombea hao wana ngome zao zinazojulikana, wametumia nafasi hiyo kuanza na maeneo magumu ili kutengeneza mazingira ya kujihakikishia hesabu za wapiga kura katika maeneo hayo," alisema.

    "Ukawa wana ngome yao (mikoa ya) kaskazini na CCM wanaonekana kuwa na ngome yao Kanda ya Ziwa, kwa hivyo kuanzia maeneo magumu hayo inaweza kuwa hesabu nzuri kisiasa.
    "Mwaka 2010, CCM ilipoteza majimbo mengi na kukosa uaminifu kwa hivyo kabla ya maeneo mengine, lazima wajipange vizuri maeneo hayo na zaidi ni kutaka kuyarudisha mikoani mwao."
    Naye Emmanuel Mallya, mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Idara ya Sayansi ya Siasa, alisema kuna siri kubwa iliyopo kwa wagombea hao kuanzia kampeni zao mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, lakini kuanza kwa kasi katika kampeni ni humu zaidi ili kutengeneza ushawishi katika mwendelezo wa mikoa mingine.

    "Ninachoamini, katika kuanza lazima ujenge ushawishi kwa kupata mwitikio mkubwa. Inawezekana CCM na Ukawa kimahesabu wameona kule ndiyo sahihi," alisema Mallya.
    "Pia kwa sasa Nyanda hiyo itakuwa na idadi kubwa ya kura kwa hivyo lazima wapiganie kwanza maeneo hayo," alisema Mallya.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.