Ratiba za kampeni za wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaonekana kuchuana vikali, Edward Lowassa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimeibua mgongano.
Hali hiyo imelalamikiwa na CCM ambayo imeitupia lawama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwamba imeshirikiana na Chadema kupanga njama hizo.
Kufuatia hali hiyo, jana Nec iliingilia kati na kuitisha kikao cha kupitia upya ratiba za kampeni za vyama.
Kampeni za vyama ambavyo vinashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, zilianza rasmi Agosti 22, mwaka huu baada ya Nec kufanya uteuzi wa wagombea.
Kwa mujibu wa taratibu na sheria, kabla ya kampeni kuanza vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi hutakiwa kuwasilisha ratiba zao Nec na baadaye tume hiyo hupanga ratiba ya nchi nzima kujumuisha vyama vyote.
Hata hivyo, kampeni za wagombea wa vyama hivyo mikoani zinaonyesha kuwa wamekuwa wakifuatiliana hususani Lowassa kwenda maeneo ambayo Magufuli anatoka kujinadi kwa wapigakura.
Lowassa alianza ziara yake mikoani Agosti 30, mwaka huu katika mkoa wa Iringa ambako alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Mufindi, Kilolo na Iringa mjini.
Baadaye aliendelea na ziara yake katika mkoa wa Njombe ambako alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Makambako na Njombe mjini.
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alitangulia kufanya ziara katika mkoa wa Njombe na kufanya mikutano katika jimbo la Njombe mjini ambako Lowassa alifanyie mkutano eneo hilo hilo.
Majimbo mengine aliyotembelea ni Makete mjini na Wanging'ombe.
Mkoa wa Ruvuma
Dk. Magufuli alitangulia kufanya ziara kwa kufanya mikutano katika majimbo ya Madaba, Nyasa, Mbinga mjini, Peramiho na kufunga pazia Songea mjini katika uwanja wa Majimaji.
Kwa upande wake, Lowassa alifanya mikutano ya kampeni katika jimbo la Madaba, Songea mjini na Tunduru.
Mkoa wa Katavi
Lowassa alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Nkasi, Mpanda mjini na Namanyele.
Kwa upande wake, Magufuli ambaye alikuwa wa kwanza kuwasili mkoani humo, alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Mpanda vijijini na Mpanda mjini.
Mkoa wa Rukwa
Dk. Magufuli alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Milele, Nkasi, Kalambo na Kwela.
Mkoa wa Morogoro
Dk. Magufuli alifanya mkutano wa kwanza wa kampeni jimbo la Mahenge, Malinyi, Ifakara na Morogoro mjini.
Walivyogongana Njombe,Iringa
Magufuli aliingia Njombe na kufanya mikutano katika jimbo la Njombe Mjini, Makete Mjini na Wang'ing'ombe.
Lowassa alianza ziara yake mikoani Agosti 30. Akatua Iringa katika majimbo ya Mufindi, Kilolo na Iringa Mjini. Kisha akatua Njombe alikotoka Magufuli na kuhutubia Makambako na Njombe mjini.
Ruvuma
Dk. Magufuli aliingia Ruvuma na kufanya mikutano Madaba, Nyasa, Mbinga Mjini, Peramiho na kumalizia Songea Mjini.
Lowassa naye akatua na kufanya mikutano ya kampeni alikopita Magufuli katika majimbo ya Madaba, Songea Mjini na kisha akafanya hivyo Tunduru.
Katavi
Magufuli aifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Mpanda Vijijini na Mpanda Mjini.
Siku chache baadaye, Lowassa alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Nkasi, Mpanda Mjini na Namanyele.
Rukwa
Dk. Magufuli alifanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya Mlele, Nkasi, Kalambo na Kwela. Hata hivyo, Lowassa hajafika katika majimbo ya mkoa huo.
Morogoro
Mwishoni mwa wiki, Dk. Magufuli alifanya mikutano ya kampeni mkoani Morogoro katika majimbo ya Mahenge, Malinyi, Ifakara na Morogoro Mjini.
Ratiba ya Lowassa inaonyesha kuwa naye atakuwa Morogoro leo kuanza mikutano yake ya kampeni mkoani humo.
Kutokana na ratiba hiyo kugonganisha wagombea hao, baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wamekuwa wakilalamikia suala hilo.
Kauli ya NEC
Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alipotafutwa ili kueleza kwa nini ratiba ya kampeni ya wagombea urais wa CCM na Chadema inagongana, alisema jana tume ilikutana na vyama vya siasa kwa ajili ya kupitia upya ratiba ya kampeni iliyotolewa awali.
"Naongoza kikao cha kamati ya vyama kupitia ratiba ya kampeni za kiti cha rais na makamu wa rais," alisema.
Kailima alisema Nec haipangi ratiba isipokuwa vyama vyenyewe hufanya hivyo chini ya uratibu wa tume.
"Leo (jana) tuko na vyama wanapitia ratiba, anayepanga ratiba siyo Nec ni wao wenyewe chini ya uratibu wa tume.
"Leo jioni (jana) tutakuwa tumemaliza kikao na vyama vyenye wagombea urais tutaweka (kwenye tovuti) ratiba mpya," alisema.
Malalamiko ya CCM
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajabu Luhavi, alisema wamebaini kuwa Nec, ilikula njama na Chadema katika kutengeneza ratiba za wagombea urais kwa kuwa walishinikiza ratiba ya CCM kuwafikia mapema.
"Tumegundua Chadema walitaka ratiba yetu itangulie, waliwasumbua wasaidizi wangu wakieleza sisi (CCM) pekee tumebaki hatujapeleka ratiba kumbe siyo kweli, na Chadema walitengeneza ratiba kwa kuangalia ya kwetu," alisema.
Luhavi alisema kwa mazingira hayo ratiba inayofanyiwa kazi awali ni iliyotangulia kufika Nec na baada ya kuligundua hilo chama kimeweka mkakati na mabadiliko yataonekana hivi karibuni.
NEC Yajibu
Hata hivyo Mkurugenzi wa Nec, Kailima, alipoulizwa kuhusu tuhuma za CCM alijibu kwa kifupi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kuwa:
"Nadhani waliosema wana nafasi nzuri ya kusema, mini siyo msemaji wao, waulize wao (CCM) waliosema."
CHADEMA: CCM wametufuata Mikoani
Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema ratiba yao ya kampeni waliipanga mapema kwa kuzingatia kanda, hivyo inawezekana CCM ndio wamewafuata katika mikoa waliokuwa wamepanga kwenye ratiba hiyo.
"Hata kama Chadema watatangulia katika mkoa au jimbo fulani kufanya mkutano wa kampeni na baadaye ikafuata CCM, eneo hilo hilo haiwezi kuaithiri Ukawa kwa sababu wananchi wameshaamua kuwa na mabadiliko," alisema.
0 comments:
Post a Comment