Mtaalamu kutoka Idara ya Nishati iliyopo chini ya Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Nyaso Makwaya akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusiana na mikakati ya Wizara katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi
Na Greyson Mwase, Morogoro
Na Greyson Mwase, Morogoro
Wizara ya nishati na madini inatarajia kuanzisha mpango wa taifa wa matumizi bora ya nishati unaotarajiwa kuanza kutekelezwa mara baada ya maandalizi yake kukamilika.
Akizungumza katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi lililokutanisha wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linaloendelea mjini Morogoro, Mhandisi Nyaso Makwaya kutoka Idara ya Nishati, Wizara ya Nishati na Madini alisema kuwa mpango huo uko katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wake.
Mhandisi Makwaya alisema kuwa maandalizi ya mpango huo yalianza mwaka 2013 na kuongeza kuwa lengo la mpango huu ni kuweka malengo ya kitaifa kwa kila sekta kwa ajili ya matumizi bora ya nishati, kuzichanganua changamoto zilizopo za matumizi bora ya nishati na kuzitafutia utatuzi na kuandaa miradi ya matumizi bora ya nishati.
" Nishati ya umeme ni muhimu sehemu yoyote, inahitaji usimamizi bora hivyo mpango huu unalenga kuboresha matumizi ya nishati katika sekta zote nchini, iwe viwanda, kilimo, ujenzi,mawasiliano n.k, mpango huu unatoa dira sahihi kwa kila sekta" Alisema Mhandisi Makwaya
Mhandisi Makwaya aliongeza kuwa mpango huu utapelekea uanzishwaji wa sheria na kanuni katika usimamizi wa matumizi bora ya nishati.
Aliongeza kuwa wadau na watekelezaji wakuu wa mpango huo ni Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Taifa la Viwango (TBS) ambao watajengewa uwezo na mradi huu.
Akizungumzia changamoto zilizopo katika usimamizi wa matumizi bora ya nishati Mhandisi Makwaya alieleza kuwa ni kutokuwepo kwa kanuni zinazosimamia matumizi bora ya nishati katika ujenzi na matokeo yake ni wajenzi kujenga majengo yasiyokuwa na uwiano kati ya ukubwa wake na kiasi cha nishati ya umeme kinachohitajika.
Mhandisi Makwaya alisisitiza kuwa changamoto hiyo ilipelekea Wizara kubuni mkakati huo ambao utaisaidia nchi kuokoa kiasi cha nishati kinachopotea na kuongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo elimu kwa umma itatolewa ili wananchi wawe na uelewa wa kusimamia vyema matumizi bora ya nishati .
"Wananchi wengi hususani wafanyakazi maofisini na viwandani hawana uelewa juu ya matumizi sahihi ya nishati ya umeme, mpango huu utakuwa ni mkombozi na hii itachangia uchumi wa nchi kukua kwa haraka kwa kuokoa gharama zisizo za lazima. " Alisisitiza Mhandisi Makwaya
0 comments:
Post a Comment