Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, anadaiwa kuporwa vitu mbalimbali zikiwamo nguo pamoja na fedha, wakati akiwa amelala kwenye moja ya nyumba za kulala wageni iliyoko mjini Bariadi mkoani Simiyu.
Habari zilizoifikia NIPASHE Jumapili jana zilisema uhalifu huo dhidi ya Waziri ulifanywa usiku wa kuamkia jana.
Akithibitisha habari hizo Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Charles Mkumbo, alisema Dk Kamani ambaye ni mbunge wa jimbo la Busega (CCM) pia Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, aliibiwa usiku wa kuamkia jana.
" Ni kweli tukio hilo lipo. Lakini nipigie simu baadaye kwa sababu nipo kwenye kikao" alisema Kamanda Mkumbo.
Chanzo chetu ndani ya nyumba hiyo kilieleza kuwa vitu vilivyoibwa ni pamoja na nguo, kadi za benki na fedha taslimu, lakini kilikataa kutajwa gazetini.
Inadaiwa Waziri huyo alibaini kuwapo kwa wizi huo alipoamka asubuhi, na hivyo kutoa taarifa katika kituo cha polisi kwa ajili ya ufuatiliaji.
Jitihada za kumtafuta Dk Kamani hazikufanikiwa kwa vile simu yake japo iliita kwa muda mrefu lakini haikuwa na majibu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment