June 24, 2014

  • TANESCO Yaibuka Mtoaji Huduma Bora na Ubunifu



    KATIBU MKUU KIONGOZI AELIMISHWA KUHUSU UTHAMINI MADINI YA ALMAS
    ·        TANESCO  Yaibuka Mtoaji Huduma Bora na Ubunifu
    ·        Wizara yaingia 10 Bora

    Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam

    Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi Ombeni Sefue ametembelea banda la Wizara ya Nishati na Madini wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na kupata fursa ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wataalam wa Wizara kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Nishati na Madini.

    Akiwa katika banda la Wizara, Balozi Sefue ameelimishwa namna Kitengo cha Uthamini Madini ya Almas na Vito (TANSORT) kinavyofanya shughuli za Uthamini madini ya Almas na namna kitengo hicho kinavyopata bei za madini katika soko la Kimataifa na namna kinavyowasiliana na wachimbaji kuwafahamisha kuhusu bei hizo katika soko la Kimataifa.

    Aidha, Katibu Mkuu Kiongozi amefahamishwa kuhusu namna mashine ya Umeme Tayari (UMETA) "Ready Board" inavyofanya kazi. Akitoa maelezo namna kifaa hicho kinavyofanya kazi, Mhandisi  Mwandamizi  Masoko na Huduma kwa Wateja, Juliana Pallangyo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ameeleza kuwa, kifaa hicho kinatumika katika maeneo yasiyohitaji 'wiring' hasa vijijini na kinatolewa bure vijijini.

    Katika hatua nyingine, TANESCO limeibuka na ushindi wa kuwa miongoni  mwa taasisi tatu bora zinazotoa huduma kwa ubunifu katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, ambapo Wizara ya Nishati na Madini imekuwa miongoni mwa taasisi  10  zenye mabanda bora katika maonesho hayo yaliyofikia kilele leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. 

    Akifunga rasmi maonesho hayo, mgeni rasmi Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesisitiza watumishi wa umma kuwatumikia wananchi kwa uadilifu, ukarimu, upendo, weledi na kwa wakati. 
       Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akimsikiliza Mtaalamu wa madini ya Vito vya Rangi na Almas Bibi Teddy Goliama kutoka Kitengo cha Uthamini Madini ya Almas na Vito (TANSORT), Wizara ya Nishati na Madini, akimweleza namna Idara hiyo inavyofanya shughuli za Uthamini wa Madini ya Almas. Kushoto kwa Katibu Mkuu Kiongozi ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Bw. Eliakim Maswi na anayefuatia ni mmoja wa wateja waliofika bandani hapo.
     Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini  Bw. Eliakim Maswi  (kushoto)akimweleza jambo mgeni aliyefika katika Banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) aliyetaka kufahamu kuhusu Mradi wa Umeme Vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Wa pili kulia anayesikiliza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ngosi Mwihava na katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Nishati na Madini Bibi Badra Masoud.
      Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiwa katika picha ya pamoja baada ya TANESCO kupata kombe la Ushindi katika kipengele cha Taasisi iliyotoa huduma Bora na Ubunifu wakati wa Maonesho hayo.
    Mhandisi Mwandamizi Masoko na Huduma kwa Wateja, Juliana Pallangyo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) akimweleza Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue namna mashine ya Umeme Tayari (UMETA) "Ready Board" inavyofanya kazi. Anaesikiliza ni Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi wa pili kushoto kwa Katibu Mkuu Kiongozi na anayefuatia ni mgeni aliyefika banda la Wizara.

      


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.