June 24, 2014

  • RC Mwanza azindua msimu wa ununuzi wa pamba 2014/15



    RC Mwanza azindua msimu wa ununuzi wa pamba 2014/15

    Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Eng. Everisti Ndikilo.
    Na Mwandishi Wetu
    MKUU wa mkoa wa Mwanza, Eng. Everisti Ndikilo, hivi karibuni amezindua rasmi msimu wa ununuzi wa pamba wa 2014/15 katika kijiji cha Isole Wilayani Sengerema.
    Wadau wa msingi wa zao la pamba ambao ni pamoja na wanunuzi wa Pamba kupitia Chama cha Wafanyabiashara wa Pamba Tanzania (TCA), Wakulima kupitia Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (TACOGA) Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na Bodi ya Pamba pamoja na wadau wengine walikutana mjini Dodoma hivi karibuni (Juni 13, 2014) kujadili na kukubaliana juu ya bei elekezi (indicative price) ya kununulia pamba kwa msimu 2014/15.
    Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba nchini Tanzania (TCB), Gabriel Mwalo, amesema kuwa wadau walikubaliana bei elekezi ya kununua na kuuza pamba (indicative price) msimu huu kuwa Shilingi za Kitanzania 750/=. kwa kilo moja ya pamba mbegu.
    "Bei elekezi (indicative price) kwa msimu husika inawekwa kwa lengo la kumlinda mkulima wa pamba asipate hasara kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kununua pamba kwa bei ndogo kuliko ilivyo katika soko la kimataifa. Wanununuzi wa pamba wanatakiwa kununua pamba kwa bei iliyo juu ya bei ya elekezi na si vinginevyo. Mnunuzi atakayenunua pamba kwa bei chini ya bei elekezi atakuwa anavunja sheria na taratibu zinazosimamia zao la pamba," Bw. Mwalo amesema.
    Aidha, Bw. Mwalo, amesema kuwa bei hiyo ni elekezi kwa maana kwamba, wakulima hawatakiwi kuuza pamba chini ya bei hii, na wakati huo huo wanunuzi wanatakiwa kutonunua pamba kwa bei iliyo chini ya bei husika.
    "Ni matarajio yetu kwamba wadau wote wanohusika watazingatia utaratibu huu ambao umewekwa kisheria, kwani kufanya kinyume ni kosa chini ya sheria ya pamba namba 2 ya mwaka 2001," amesema.
    Aliongeza kuwa mchakato wa kupata bei elekezi (indicative price) unazingatia vigezo vingi ili kulinda maslahi ya wadau wote ambao kimsingi ni wakulima na wanunuzi wa pamba.
    "Kwa vile Pamba ya Tanzania kwa kiasi kikubwa inauzwa nje ya nchi ikiwa ghafi, kigezo cha kwanza kabisa kinachotumika katika kuandaa Bei elekezi ni hali ya bei ilivyo katika soko la dunia kwa wakati huo," amesema.
    Vigezo vingine ni gharama za uzalishaji wa pamba kwa mkulima, gharama za ununuzi, usafirishaji na uchambuaji wa pamba, mchango wa Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la pamba na kodi za Serikali (Ushuru wa Halmashauri za Wilaya).
    "Wakulima kupitia TACOGA wanaandaa gharama za uzalishaji wakati wanunuzi wa pamba chini ya TCA wanakokotoa bei kwa upande wao. Serikali kama msimamizi wa sheria na taratibu, haifanyi maamuzi juu ya Bei elekezi bali wadau (wakulima na wanunuzi) wanakubaliana wenyewe na serikali kupitia Bodi ya Pamba inashauri kwa kutoa taarifa ili kupata muafaka wenye manufaa kwa pande zote mbili," amesema.
    Pamba ni zao la biashara la msimu ambalo linazalishwa katika mikoa 15 nchini.; Mikoa hii imegawanyika katika Kanda mbili ambazo ni Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora, Mara, Kigoma, Singida na Kagera, wakati Kanda ya Mashariki inajumuisha mikoa ya Morogoro, Iringa, Pwani, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
    Kanda hizi mbili zinatofautia kwa kiasi kikubwa katika hali ya udongo, mtawanyiko wa mvua, magonjwa ya pamba na aina ya wadudu wanapatikana katika maeneo husika na kuanza kwa misimu ya kilimo.
    Msimu wa kilimo/kupanda pamba kwa Kanda ya Magharibi unaanza katikati ya mwezi Novemba wakati Kanda ya Mashariki msimu wa kupanda pamba unaanza mwanzoni mwa mwezi Februari.
    Kutokana na tofauti hizi uvunaji na uuzaji wa pamba unaanza katika vipindi tofauti hivyo kulazimu Tasnia ya Pamba kuweka utaratibu wa kuzindua msimu wa ununuzi mwezi wa Juni kwa Kanda ya Magharibi na Septemba kwa Kanda ya Mashariki. Uzalishaji wa pamba msimu huu unakadiriwa kuwa tani 250,000 za pamba mbegu.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.