June 25, 2014

  • Mataifa 31kushiriki Maonesho ya 38 ya Biashara ya SABASABA MWAKA HUU



    Mataifa 31kushiriki Maonesho ya 38 ya Biashara ya SABASABA MWAKA HUU
    Zikiwa imebakia siku chache kuanza Maonesho ya 38 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (maarufu kama Saba Saba), tayari Mataifa 31 na makampuni zaidi ya 500 yamethibitisha kushiriki katika maonesho hayo. Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Jacqueline Mneney Maleko ametanabaisha hayo katika hafla ya kusaini Mkataba wa Udhamini wa Mawasiliano na kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom ambao utawezesha kufanikisha maandalizi na Mawasiliano katika kipindi chote cha Maonesho hayo.
     "Maonesho haya yamekuwa kiungo kikubwa sana, kwa Makampuni ya nje na makampuni ya ndani na pia yanatoa nafasi kwa kampuni hizo kukutana na wateja wao na kuzungumza ana kwa ana," alisema na kuongeza. " Mwaka huu Mataifa 31 na makampuni zaidi ya 500 yamethibitisha kushiriki katika maonesho ya mwaka huu." 
    Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa washiriki ambao hawajajiandikisha kwa ajili ya zoezi la kutafuta washindi katika makundi mbalimbali kuchukua fomu na kujiandikisha. Zoezi hilo limepangwa kufanyika kuanzia saa 6.00 mchana tarehe 28 Juni na kumalizika tarehe 29, Juni 2014. Bi. Maleko, alihitimisha kwa kutoa wito kwa washiriki kujiandaa kutembelea maonesho hayo ili kupata fursa za masoko, uwekezaji na ajira. Milango itafunguliwa kuanzia Jumamosi tarehe 28 Juni, 2014. 
    Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa amesema, ushirikiano kati yao na TanTarde umekuwa na manufaa kwani umewezesha kujenga daraja na kutoa fursa kwa kampuni za ndani na kampuni za nje. "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (maarufu kama Sabasaba) ni fursa ambayo makampuni huitumia kujitangaza na kukutana na wateja wao ana kwa ana, Kwetu sisi huu ni uwanja wa kuwadhihirishia wateja na watanzania kwa ujumla ubunifu tulio nao katika huduma na bidhaa wanazozihitaji." Alisema Twissa 
    "Miongoni mwa huduma hizi ni M Pawa, ambayo kupitia huduma hiyo tumewawezesha watanzania kuwa na akaunti ya benki katika simu zao ambapo sasa wanaweza kuweka akiba ili kufikia malengo yao na hata kukopa pale wanapohitaji." Aidha, Twissa aliendelea kwa kufafanua umuhimu wa huduma za kifedha kwa njia ya simu za mkononi kuwa ni mapinduzi ya mtandao wake unaojivunia mawakala zaidi ya 75,000 wa kuaminika nchi nzima. Mteja kuwa na huduma ya M Pesa ni zaidi ya benki kiganjani mwake kwani ana uwezo mkubwa wa kufanya miamala ya fedha ikiwemo kutuma, kupokea na kutoa pamoja na biashara zaidi ya 600 zilizounganishwa na huduma hiyo.
    "Natoa wito kwa Watanzania kutembelea banda letu kupatiwa huduma na bidhaa zetu, pia kupata maelezo juu ya ofa lukuki tulizonazo. Napenda kuwashukuru TanTrade kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kipindi hiki muhimu kwa wafanyabiashara nchini." Alihitimisha Twissa. 
    Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam "SabaSaba" ni maonesho ya biashara yanayoongoza siyo nchini Tanzania tu bali katika eneo lote la Afrika Mashariki kwani huwapatia fursa wafanyabiashara fursa ya kuonyesha na kutafuta masoko ya bidhaa na huduma walizonazo. Mbali na hapo pia huwakutanisha wafanyabiashara mbalimbali kujionea bidhaa wanazozalisha ili kusaidia ubora na ushindani. 
    Maonesho haya yanayofanyika kwa siku kumi huwavutia wageni zaidi ya 350,000 na kujenga mahusiano mazuri baina ya watoa huduma na wateja wao. Katika maonesho haya, waoneshaji hupata fursa ya kukutana na wateja wao na watembeleaji hupata nafasi ya kuangalia na kulinganisha ubora wa bidhaa, bei, teknologia na hata kujifunza kutoka kwa waoneshaji mbinu za kuboresha au kuanzisha biashara zao. 
    ILI KULETA MAFANIKIO NA KUHAKIKISHA USALAMA UNAKUWAPO KIPINDI CHOTE CHA MAONESHO, SILAHA ZA AINA YOYOTE AU MIFANO YAKE HAZITARUHUSIWA KATIKA UWANJA WA MAONESHO'.
     Mkurugenzi Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacquiline Maleko, akizungumza na waandishi wa haabari kuhusiana na kuingia Ubia na kampuni  ya Mawasiliano ya Vodacom, Kama mdhamini Mkuu wa Mawasiliano wakati wa maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakayo anza 28 juni na kumalizika julai 8 mwaka huu. Kulia ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Masoko wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa.
     MKURUGENZI Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacquiline Maleko na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Masoko wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, wakioneshwa na Mwanasheria wa TanTrade, Godwin Mutahangarwa,(Kushoto) Mkataba wa Udhamini wa maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakayo anza 28 juni na kumalizika julai 8 mwaka huu.
      MKURUGENZI Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacquiline Maleko, akipitia Mkataba wa Udhamini wa maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakayoanza 28 juni  na kumalizika julai 8 mwaka huu. Wanaoshuhudia ni Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa (Kulia) na Mwanasheria wa TanTrade, Godwin Mutahangarwa (Katikati)
    MKURUGENZI Mkuu wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacquiline Maleko, na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa, wakibadilishana mkataba wa Udhamini wa maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam yatakayoanza 28 juni  na kumalizika julai 8 mwaka huu. Kushoto ni Mwanasheria wa TanTrade, Godwin Mutahangarwa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.