October 07, 2014

  • JK AOMBOLEZA MISIBA YA BRIGEDIA JENERALI MUHIDIN KIMARIO NA DKT WILLIAM SHIJA



    JK AOMBOLEZA MISIBA YA BRIGEDIA JENERALI MUHIDIN KIMARIO NA DKT WILLIAM SHIJA
    Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, kuomboleza kifo cha Meja Jenerali Muhidin Kimario, Waziri Mwandamizi wa Zamani wa Serikali na Jenerali Mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
    Aidha, Rais Kikwete amewatumia pole nyingi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange na familia ya Meja Jenerali Kimario kufuatia kifo hicho kilichotokea mchana wa leo, Jumatatu, Oktoba 6, 2014, nchini India, ambako alikuwa anapata matibabu.
    Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo kwa Waziri Mwinyi: "Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Meja Jenerali Muhidin Kimario, ambaye alilitumikia Jeshi letu kwa heshima kubwa na weledi wa kuigwa na baadaye kulitumikia Taifa letu kwa uaminifu na uadilifu wa kujivunia katika nafasi ya uwaziri."
    Ameongeza Rais Kikwete katika rambirambi zake: "Uhodari na ujasiri ule ule ambao Meja Jenerali Kimario aliuonyesha akiwa askari na ofisa mkuu ndio ule ule uliomwongoza katika utumishi wa umma na kwa nafasi zote za waziri mwandamizi, ambazo alizishikilia katika maisha yake iwe ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mkuu wa Mkoa ama Mkurugenzi wa Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA). Daima tutakosa uongozi na ushauri wake."
    "Nakutumia wewe Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki. Aidha, kupitia kwako, namtumia pole nyingi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na Jeshi letu lote kwa kuondokewa na ofisa mwenzao, kiongozi wao na mpiganaji mwenzao,"amesema Rais Kikwete na kuongeza:
    "Aidha, kupitia kwako, natuma salamu zenye huzuni nyingi kwa familia ya Meja Jenerali Muhidin Kimario. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa wa kuondokewa na mhimili wa familia. Vile vile wajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi roho ya Marehemu. Amin."

    Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea huzuni na masikitiko yake kuomboleza kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mabunge ya Nchi za Jumuia ya Madola (CPA), Mheshimiwa Dkt. William Shija.
    Dkt. Shija aliyefariki dunia Jumamosi asubuhi mjini London, Uingereza, ambacho ndicho kilikuwa kituo chake cha kazi, alisomea na kuwa mhadhiri wa uandishi wa habari kabla ya kuwa mbunge wa Sengerema kwa miaka 15 mfululizo na Waziri Mwandamizi wa Serikali katika Wizara mbali mbali.
    Katika salamu zake kwa Sekretarieti ya CPA, Kanda ya Afrika, Rais Kikwete amesema kuwa amestushwa sana na kifo cha Dkt. Shija ambacho kimeinyang'anya Afrika na dunia, na hasa Tanzania na Jumuia ya Madola, mtumishi mwadilifu na mwaminifu, ambaye alitoa maisha yake kwa utumishi wa umma.
    "Alikuwa kiongozi mfano katika nafasi zote za umma alizozishikilia. Aliifanya kazi yake ya uhadhiri wa uandishi wa habari kwa ufanisi mkubwa na aliwapa utumishi uliotukuka wananchi wake wa Sengerema katika nafasi yake ya Ubunge. Dkt. Shija alitumainiwa sana katika nafasi zote nyingi na za uandamizi za Uwaziri wa serikali," amesema rais Kikwete na kuongeza:
    "Nawatumieni salamu za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Dkt. Shija na naungana nanyi katika kumlilia. Kupitia kwenu, nawatumia wajumbe wote wa CPA na Sekretarieti ya Chama hicho pole nyingi sana kwa kuondokewa na kiongozi na mtendaji wao mkuu. Aidha, naomba pia mniwasilishie pole zangu kwa wana-Sengerema ambao Dkt. Shija aliwatumikia kwa uaminifu na kwa miaka mingi."
    "Wajulisheni wote kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa na naomboleza nao na niko nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweka peponi roho ya Marehemu William Shija. Amin."

    Imetolewa na;
    Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
    Ikulu – Dar es Salaam.
    6 Oktoba, 2014.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.