October 10, 2014

  • WAZIRI MKUU AVUTIWA NA KASI YA MABADILIKO SOKOINE



    WAZIRI MKUU AVUTIWA NA KASI YA MABADILIKO SOKOINE
    *Maprofesa waomba kuongezewa muda wa kustaafu

    WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema amevutiwa na kasi ya mabadiliko katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na hasa uanzishwaji wa kozi mpya zinazolenga uongezaji thamani wa mazao ya kilimo (Agri-processing).

    Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 9, 2014) wakati akizungumza na wahadhiri, wakufunzi, wanafunzi na wanajumuiya ya SUA mara baada ya kutembelea chuo hicho na kukagua utekelezaji wa mradi wa Sayansi na Teknolojia ya Elimu ya Juu (Science and Technology Higher Education Project - STHEP).

    "Nimefurahia sana hili suala la Agri-processing kwa sababu hivi tuna mzigo mkubwa unaoisumbua Serikali nao ni namna ya kununua mazao ya wakulima. Tuna ziada ya tani milioni 1.5 za mahindi na tani laki nane za mpunga wakati uwezo wa NFRA ni kununua tani 240,000 tu. Haya ni matokeo ya wahitimu waliotoka SUA na kupelekwa wilayani na vijijini wakahimiza kilimo bora kwa wananchi," alifafanua.

    Waziri Mkuu ambaye aliwasili Morogoro jana mchana akitokea Dodoma, alifanya ziara ya siku kwa kutembelea Chuo Kikuu hicho pamoja na kiwanda cha kutengeneza nguo cha 21stCentury.

    Akiwa chuoni hapo, Waziri Mkuu alikagua majengo matatu yaliyojengwa chini ya mradi wa STHEP na kuzindua mawili kati ya hayo, alitembelea maabara za upimaji ubora wa vyakula na kisha kuzungumza na wanaSUA.

    Akizungumza na wanajumuiya hao, Waziri Mkuu aliwataka wawe ni viongozi wa mfano kwa kumiliki walau ekari moja ya shamba, walime au kuweka mifugo ili yale wanayofundisha darasani yaonekane kwa vitendo katika mashamba hayo.

    "Tatizo la sasa hivi miongoni mwa wasomi wengi ni kudhani kwamba kazi ya kilimo ni ya watu wa hali ya chini lakini wakifika mezani wao ndiyo wa kwanza kudai ubwabwa na kuku. Sisi wenye upeo ndiyo tunapaswa tuonyeshe njia na mashamba au mifugo yetu yawe ni ya mfano kwa wengine," alisema.

    Mapema,akiwasilisha taarifa ya mradi wa STHEP, Profesa Gerald Monella alisema mradi huo wenye thamani ya dola za Marekani milioni 7.48 (sawa na sh. milioni 12.5/-) umekisaidia chuo hicho kupata majengo manne yenye kati ya ghorofa moja na mbili, ambayo yameongeza nafasi za kufundishia wanafunzi, vyumba vya maabara na vifaa vyake, kuanzisha mitaala miwili pamoja na kusomesha walimu 21.

    Kwa kutumia majengo hayo, Chuo kinaweza kufundisha wanafunzi 807 kwa wakati mmoja ambayo ni sawa na wanafunzi 10,565 kwa wiki moja. Chuo hicho pia kimeweza kupata vifaa vya maabara vyenye thamani ya dola za marekani milioni 1.71 ambavyo vimenunuliwa na kufungwa kwenye maabara hizo.

    "Kwa upande wa elimu ya juu, mradi umeweza kusomesha walimu 21, miongoni mwao 11 wakiwa ni wa shahada ya uzamivu (PhD) na 10 ni wa shahada za uzamili (Masters').

    Aliiomba Serikali iongeze muda wa kustaafu kwa wahadhiri wa vyuo vikuu kwani wanapozeeka ndiyo wanapata muda wa kufanya tafiti zaidi. "Fani nyingie watumishi wanastaafu wakiwa na miaka 60 au zaidi, nasi tunaomba tuongezewe muda badala ya kutumia mfumo wa sasa wa kuongezewa miaka miwili miwili halafu mmoja," alisema.

    Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Mama Kate Kamba wakati akitoa salamu za shukrani kwa Waziri Mkuu, alisema Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza bajeti ya Chuo kwani kinahitaji fedha zaidi kwa ajili ya kufanya tafiti na kuboresha miundombinu.

    "Tunahitaji fedha za kufanya tafiti zaidi, fedha za kuboresha miundombinu ya kufundishia ili tuweze kwenda sambamba na azma ya Serikali ya kuimarisha viwanda vya usindikaji mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo," alisema.

    IMETOLEWA NA:
    OFISI YA WAZIRI MKUU,
    2 MTAA WA MAGOGONI,
    11410 – DAR ES SALAAM.

    IJUMAA, OKTOBA 10, 2014


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.