Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja wa Mataifa unaitambua Western Sahara kuwa ni Koloni ambalo linapashwa kuondokana na minyororo ya ukoloni , liwe huru na lijiamulie mambo yake yenyewe kama taifa huru.
Hata hivyo tangu mwaka 1963 Western Sahara ilipotambuliwa kuwa koloni, pamoja na michakato mbalimbali inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na wadau wengine wengi, bado safari ya koloni hilo pekee Barani Afrika ya kuikata minyororo ya ukoloni inazidi kuwa ndefu na yenye mabonde mengi.
Kama hiyo haitoshi, mchakato wa kuisaidia Western Sahara kufikia hatua ya kuwa nchi huru inaelekea sasa kuigawa Jumuiya ya Kimataifa katika pande zinazokinzana.
Kwa zaidi ya wiki Moja sasa wajumbe wa Kamati Maalum ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na Masuala ya Siasa na Umalizaji wa Ukoloni, wamekuwa wakijadiliana na kubadilishana mawazo ya namna, pamoja na mambo mengine, kuchagiza umalizwaji wa ukoloni kwenye makoloni 17 yanayotambuliwa rasmi ndani ya Umoja wa Mataifa ikiwamo Western Sahara.
Ni katika majadaliano hayo, ambapo pia wajumbe wa Kamati waliwasikiliza petitioners zaidi ya 60 waliojenga hoja mbalimbali zikiwamo zinazoitaka Jumuiya ya Kimataifa kwa maana ya Umoja wa Mataifa kuharakisha mchakato wa kuipatia Western Sahara uhuru wake kamili au iwe sehemu ya Morocco.
Ni katika majadiliano hayo, ambapo pia, misimamo ya wazi wazi imejitokeza kwa baadhi ya wajumbe kusimamia au kuegemema upande wa Morocco ambaye ndiye mtawala ( Mkoloni)wa sasa wa Western Sahara baada ya mkoloni wa awali Hispania kuliacha mwaka 1963. Wajumbe wengine zikiwamo nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza pamoja na nchi za Amerika ya Kati wao zenyewe zinasimamia katika kutaka Western Sahara iachwe huru na iwe na haki kuajiamulia hatima yake. Kwa wale wanaogemea upande wa Morocco, zikiwamo baadhi ya nchi zinazozungumza Kifaransa nyingi zikiwa za Kiafrika.
Wao wanapigia chapuo hoja inayopendekezwa na Morocco ya kuipatia Western Sahara uhuru wa kujiamulia baadhi ya mambo yake ( limited autonomy) lakini ibaki kuwa sehemu kamili ya Morocco.
Wanaounga mkono hoja hii wanaamini kwamba pengine huu ndiyo mwelekeo sahihi wa kisiasa na wenye kutekelezeka. Lakini wakati huo huo unakosa hoja ya msingi ya uhuru kamili na kujitawala. Hata hivyo kundi la pili na ambalo pengine ni kubwa zaidi lenyewe linapendekeza kuwa wananchi wa Western Sahara na kwa mujibu wa maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu la Usalama wanapashwa kuachiwa wenyewe fursa ya nini wanataka iwe hatima yao kama ni kuwa na uhuru kamili nakujiamulia mambo yao au pendekezo hilo la limited autonomy.
Lakini wafanya hivyo bila ya kushinikizwa na wala wasiamuliwe. Wanaopendekeza hivyo wanasimamia katika ile misingi inatoainishwa na katiba ya Umoja wa Mataifa inayowapatia watu wa Saharawi haki yao ya msingi inayoainishwa katika maazimio mbalimbali ya Umoja wa yanayowataka wafanye hivyo kupitia kura ya maoni ( referendum), kama ilivyopendekezwa na kupitishwa na Baraza Kuu la Usalama kupitia maazimo 658 ( 1990) na 690 ( 1991). Hata hivyo pamoja na kupitishwa kwa maazimio hayo pamoja na kuundwa kwa chombo cha kusimamia kura hiyo ya maaoni ( MINURSO).
Kura hiyo haijafanyika kutoka na kile kinachoelezwa ni pingamizi zinayowekwa na Morocco. Jitihada mbalimbali za Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Christopher Ross zimeshindwa kusukuma mbele mchakato wa kuipatia Western Sahara uhuru wa kujiamulia mambo yake.
Kama hiyo haitoshi, Umoja wa Afrika umemteua Rais mstaafu wa Msumbiji Joachim Chisano kuwa mjumbe wake maalum wa kulishughulikia suala la Western Sahara na afanye kazi kwa karibu na Umoja wa Mataifa. Wajumbe wa Kamati ya Nne wameelezwa kuwa kadri suala la Western Sahara linavyochelewa kupatiwa ufumbuzi ndivyo hali inavyozidi kuwa tete hususani katika makambi ya wakimbizi yanayohudumia wakimbizi wa Western Sahara wanaohifadhi humo.
Wakati wa majadiliano hayo zilitolewa taarifa zinazoonyesha kuwa katika kambi hizo za wakimbizi hususani ile ya Tinduff imegeuka au imo katika hatari ya kugeuzwa eneo ambalo vijana wa Kisaharawi wanarubuniwa na kuingizwa katika makundi ya ugaidi. Waliozungumza wanasema vijana hao wameamua kuingia katika vitendo vya ugaidi kwa kile kinachodaiwa kukata tamaa na mkwamo wamchakato mzima wa kuamua hatima yao yaani kuwa huru.
Ni kwa sababu hiyo na tishio hilo la ugaidi katika kambi hizo na mstakabali mzima wa hali ya Amani na usalama katika eneo la Maghereb, imefikia wakati sasa ambapo Jumuiya ya Kimataifa inashauriwa kuliangalia kwa jicho pana zaidi suala la Western Sahara.
Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akichangia majadiliano ya jumla kuhusu agenda ya umalizaji wa ukoloni katika makoloni 17 yanayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa likiwamo la Western Sahara koloni pekee katika Bara la Afrika. Akizungumza kwa niaba ya Tanzania Balozi Mwinyi pamoja na mambo mengine alirejea wito Uliotolewa na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba, ambapo alilitaka Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kutumia uwezo wake kulitafutia ufumbuzi wa kudumu na wa mwisho kuhusu Koloni hilo la Western Sahara. Tanzania ni kati ya nchi ambazo zimesisitiza haki na uhuru wa watu wa Saharawi kujiamulia hatima yake kwa mujibu wa maazimio na mapendekezo ya Umoja wa Mataifa. Tanzania licha ya kuwa mjumbe wa Kamati ya Nne inayohusika na masuala ya Siasa na Umalizaji wa Ukoloni pia ni mjumbe wa Kamati ya nchi 24 ( C24) ambayo imekasimiwa jukumu la kumaliza ukoloni.
0 comments:
Post a Comment