Na Samwel Mtuwa.
Wakala wa Jiolojia Tanzania , umefanikiwa kupunguza gharama za upimaji wa sampuli za dhahabu katika maabara yake kwa kufanikiwa kwa asilimia mia moja kuweza kutengeneza vikombe vya kupimia dhahabu (Crucible) ndani ya maabara yake ya Jiolojia mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa mtaalam wa Jioloji katika Maabara ya GST, Bw. Philipo Momburi alieleza kuwa hapo awali maabara ilikuwa inaagiza vikombe vya kupimia dhahabu maabara kutoka nje ya nchi , jambo ambalo lilikuwa likiingiza taasisi katika gharama kubwa , lakini baada ya utafiti wa kuandaa vikombe vya kupimia sampuli ya dhahabu kukamilika umeweza kupunguza ghara kwa asilimia hamsini (50%).
Bw. Momburi aliongeza kuwa utafiti ulianza mwaka 1994 ambapo ulidumu kwa miaka ishirini kabla ya kukamilika, ambapo baada ya kukamilika utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2013, kutokana na kukamilika kwa utafiti GST imeweza kuongeza huduma za kibiashara kwa kuongeza idadi ya upimaji wa sampuli kutoka vikombe 20 mpaka 40 kwa siku.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maabara ya Jioloji GST Bi Augustine Rutaihwa, aliongeza kuwa baada ya kuweza kutengeneza vikombe hivyo , taasisi imeweza kupata ubora mzuri wa upimaji wa sampuli katika maabara ya GST , kuongeza ujuzi kwa wataalamu , kutoa huduma kwa wakati , lakini pia kuweza kutumia malighafi za ndani badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
Maabara ya upimaji wa sampuli za madini ilianzishwa mwaka 1929 kwa ajili ya kuboresha shughuli za Idara hasa kwa upande wa uchambuzi wa kimaabara wa sampuli za miamba , madini na maji.
Mtaalam wa Jiolojia Bw. P.B Momburi akieonesha vikombe vya kupimia dhahabu katika maabara ya Wakala wa Jiolojia Tanzania.
0 comments:
Post a Comment