October 29, 2014

  • UHABA WA DAWA VIFAA NA TIBA MZIGO KWA SERIKALI



    UHABA WA DAWA VIFAA NA TIBA MZIGO KWA SERIKALI
    Suala la uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali nchini ikiwamo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, limeonekana kuielemea Wizara ya Afya baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid kuthibitisha, huku akidai kuwa Serikali itapeleka fedha kwa awamu Bohari ya Kuu ya Dawa ili kupunguza uhaba huo.

    Waziri Rashid alikiri kuwa MSD inaidai Serikali kiasi cha Sh90 bilioni, jambo ambalo linaifanya bohari hiyo kushindwa kununua dawa kutoka kwa wauzaji ndani na nje ya nchi. "Ni kweli bohari kuu ya dawa imepungukiwa fedha za kununulia dawa, lakini siyo kwa kiasi cha kushindwa kutoa huduma kabisa kama inavyoelezwa. Kiasi cha pesa kinachotajwa si kigeni na Serikali imekuwa ikitoa kiasi cha fedha kidogo kidogo ili kuongeza uwezo wa bohari ya dawa kununua na kusambaza dawa," alisema waziri katika tamko lake jana.
    Juzi gazeti hili lilichapisha taarifa ya uhaba wa dawa Taasisi ya ORCI na kufuatiwa na taarifa kutoka shirika lisilo la kiserikali la Sikika ambayo ilieleza kuwa Serikali haijalipa kiasi cha Sh90 bilioni kwa MSD.
    Waziri Rashid alikiri kuwapo kwa ukosefu wa matibabu OCRI kutokana na uhaba wa dawa na ubovu wa baadhi ya mashine za mionzi.
    Kadhalika waziri alionyesha kuwa suala la ORCI ni zito kwa Serikali baada ya kusema kuwa matibabu katika taasisi hiyo hutolewa bila malipo.
    "Katika kukabiliana na hali hii, hospitali zote kupitia waganga wakuu wa mikoa na wilaya zimeagizwa kupeleka asilimia 50 ya mapato yanayotokana na uchangiaji kwenda MSD," alisema waziri.
    Alisema wataalamu kutoka Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN) wanamalizia kazi za utekelezaji wa mpango huo na wamesisitizwa kuzingatia dawa zinapatikana kwa wakati katika vituo vya matibabu na kuiboresha MSD.
    Rashid alizitaka hospitali kuhakikisha zinapeleka asilimia 50 ya mapato licha ya kuwa wizara inapeleka fedha MSD kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kuonya kuwa kiongozi atakayekiuka hilo atawajibishwa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.