October 20, 2014

  • ZAIDI YA NYUMBA 38 ZAEZULIWA MAPAA NA UPEPO MKALI ULIOAMBATANA NA MVUA KIJIJI CHA MAPOGOLO WILAYANI CHUNYA


    ZAIDI YA NYUMBA 38 ZAEZULIWA MAPAA NA UPEPO MKALI ULIOAMBATANA NA MVUA KIJIJI CHA MAPOGOLO WILAYANI CHUNYA

    Mkuu wa Wilaya hiyo Deodatus Kinawiro alipowatembelea wahanga kuwapa pole. akifuatana na Mkurugenzi wa Halmashauri Sophia Kumbuli.







    Mkuu wa Wilaya hiyo Deodatus Kinawiro akiongea na wahanga hao

    Baadhi ya wahanga wakimsikiliza mkuu wa Wilaya Chunya


    Zaidi ya nyumba 38 zimeezuliwa na upepo ulioambatana na mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma katika kijiji cha Mapogolo Kata ya Chokaa wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

    Hayo yamethibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Deodatus Kinawiro alipowatembelea wahanga akifuatana na Mkurugenzi wa Halmashauri Sophia Kumbuli ambapo walitembelea wahanga na kuwapa pole.

    Janga hilo pia lileta athari kwa kanisa la EAGT ambalo liliezuliwa paa lote na kusababisha mabati yaliyoezekwa hivi karibuni baadhi kuharibika vibaya hivyo kutofaa kuezekewa tena.

    Kwa mujibu wa Taarifa ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Mapogolo Samwel Komba iliyosomwa na Mtendaji wa Kijiji Linus Mkumbwa imesema kuwa hakuna vifo wala madhara yoyote kwa binadamu ingawa baadhi ya vyakula vimeharibika na wahanga wamehifadhiwa na ndugu na marafiki.

    Kutokana na baadhi ya familia kuwa na hali ngumu ya maisha na wengi wao kuwa ni wazee Mkuu wa Wilaya aliongoza Harambee ya papo hapo ambapo jumla ya shilingi laki nane na elfu ishirini zilipatikana kutoka kwa viongozi walioambatana na Mkuu wa Wilaya na wananchi waliofika kumsikiliza Mkuu wa Wilaya.

    Hata hivyo Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa wananchi kuwa fedha hizo zitumike kununua mahitaji muhimu kama misumari,mbao na mabati kwa watu wasio na uwezo pia mafundi wajitolee kusaidia kuezeka ili wahanga wapate hifadhi.

    Aidha ametoa agizo kwa Mhandisi wa Ujenzi Nuru Ndelwa kusaidia kusimamia ukarabati wa nyumba hizo kwani nyingi ya nyumba zilizoezuliwa zilikuwa haziko kwenye kiwango hali ilyosababisha kuezuliwa kutokana na mabati kupigwa bila mtambaa panya.

    Kinawiro ametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia michango ya hali na mali wananchi hao na kwamba suala hilo lipo ndani ya uwezo wao na Wilaya kwa ujumla kwani kutoa ni moyo wala si utajiri.

                                    Na   Mbeya yetu




  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.