October 11, 2014

  • Mkuu wa Wilaya ya Korogwe ajisalimisha kwenye Baraza la Maadili na kupewa onyo, Nchambi apewa nafasi kufika kikao


    Mkuu wa Wilaya ya Korogwe ajisalimisha kwenye Baraza la Maadili na kupewa onyo, Nchambi apewa nafasi kufika kikao
    Na. Ally Mataula – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma

    Wakati Vikao vya Baraza la Maadili vikiendelea siku yake ya pili kusikiliza mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995, Baraza hilo likiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Balozi Jaji (Mst.) Hamisi Msumi limetoa onyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Gambo kwa kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza hilo kujibu tuhuma zinazomkabili.

    Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga ambaye alilieleza Baraza kuwa wao kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamejiridhisha kuwa wito wa kuitwa mbele ya Baraza hilo ulimfikia Mlalamikiwa zaidi ya wiki tatu kabla ya kuanza vikao vya Baraza na hivyo Mhe. Gambo amelidharau Baraza kwa kitendo chake cha kutofika tarehe 9/10/2014. Hata hivyo, Bw. Mayunga aliliomba Baraza hilo kuahirisha shauri hilo mpaka Jumatatu tarehe 13 Oktoba, 2014.

    Naye Mhe. Gambo alipopewa nafasi ya kujitetea kwa kitendo chake cha kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza alisema kuwa wito wa kumtaka yeye kufika mbele ya Baraza haukumfikia kutokana na yeye kuwa nje ya kituo chake cha kazi na badala yake alipata taarifa ya kutakiwa kukamatwa kupitia vyombo vya habari. Mhe Gambo aliendelea kulieleza Baraza kuwa hakuwa na sababu ya yeye kukaidi wito huo na kwamba baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari aliwasiliana na Katibu Muhtasi wake ambaye alimuagiza afungue barua zote zilizofika ofisini kwake kwa jina lake na kama kuna barua kutoka Tume ya Maadili amtumie kwa njia ya fax. Mhe. Gambo alisema kuwa baada ya kutumiwa barua hiyo alianza safari ya kuja Dar es Salaam kuitikia wito wa Baraza.

    Akitoa hitimisho kuhusu shauri hilo, Mhe. Jaji Msumi alisema kuwa amri ya kukamatwa mlalamikiwa imefutwa. "Mlalamikiwa amepewa onyo la kumtaka kutii amri ya kisheria ya Baraza. Shauri litasikilizwa tarehe 13/10/2014 saa tatu asubuhi" alisema Mhe. Jaji Msumi.

    Kuhusu Shauri linalomhusu Mbunge wa Kishapu Mhe. Suleiman Masoud Nchambi Suleiman ambaye analalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kutowasilisha Tamko la Mali na Madeni kwa kipindi cha mwaka 2012 halikusikilizwa kutokana na Mhe. Nchambi kutofika mbele ya Baraza hilo. Mhe. Nchambi ambaye shauri lake liliahirishwa kusikilizwa katika vikao vya Baraza vilivyofanyika mwaka jana 2013 katika Manispaa ya Tabora hakuweza kufika katika vikao vya Baraza vinavyoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Karimjee bila taarifa rasmi ya maandishi.

    Kwa Mujibu wa Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Mwanarabu Talle ambaye aliliambia Baraza kuwa Mlalamikiwa anaonekana kuwa ni mkaidi hivyo alipendekeza Baraza kutumia fungu la 24 (4) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya 1995 ambalo linatoa mamlaka kwa Mwenyekiti kutoa hati ya kukamatwa Mlalamikiwa na Afisa wa Polisi na kufikishwa mbele ya Baraza.

    Akihitimisha Shauri hilo Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Jaji Msumi alisema kuwa hii ni mara ya pili kwa Mlalamikiwa kuomba usikilizwaji wa lalamiko lake kuahirishwa.

    "Baraza lina wasiwasi kuwa huenda Mlalamikiwa ametumia mbinu za kuchelewesha lalamiko hili. Hata hivyo tunaona ni busara tutoe muda mwingine ambao utakuwa ni wa mwisho. Hivyo lalamiko linahairishwa hadi kikao kijacho. Mlalamikiwa afahamishwe kuwa Baraza halitakubali sababu yeyote tena ya kuahirisha lalamiko hili" Alifafanua Mhe. Msumi.

    Kwa upande mwingine, Baraza la Maadili limeweza kusikiliza mashauri mengine yanayowahusu viongozi watatu ambao ni Bw. Venance Kenneth Ngunga – Mhasibu Mkuu, Taasisi ya Technoloji Dar Es Salaam (DIT), Mhe. Mohamed Ally Chambuso – Diwani Kata ya Mzimuni na Bibi Florence Sastony Masunga – Diwani Viti Maalum, Kinondoni, wote walikuwa wanalalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kushindwa kuwasilisha Tamko la Mali na Madeni kwa mujibu wa Sheria.

    Pia, Mhe. Msumi ametoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mbele ya Baraza hilo Bibi Sarah Kinyamfura Barahomoka ambaye ni Mkurugenza Msaidizi – Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza kujibu tuhuma zinazomkabili. Kwa mujibu wa ratiba, vikao vya Baraza la Maadili vitaendelea tena siku ya Jumatatu tarehe 13 Oktoba, 2014.
    Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho Gambo akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kuahirishwa kusikilizwa Shauri lake mbele ya Baraza la Maadili.
    Afisa Sheria Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Filotheus Manula akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu yaliyojiri katika Baraza la Maadili katika siku yake ya pili ya kusikiliza mashauri yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.