October 19, 2014

  • UHALIFU MAENEO YA AJALI UKOMESHWE!



    Upo usemi kuwa, ajali haina kinga. Ni bahati mbaya kwamba usemi huu unasikika kila inapotokea ajali au janga, nasi tunajifariji kuwa ni mpango wa Mungu.

    Matokeo ya mazoea ni kuongezeka kwa ajali zinazoua au hata kuwajeruhi watu wengi. Ajali hizo pia zimesababisha hasara, huku tukiendelea kusema ajali haina kinga.

    Ni nadra kutokea kwa ajali, kisha ikasababisha moto ambao hatimaye husababisha maafa kama ilivyotokea mwishoni mwa wiki,
    Mbagala jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo, lori la mafuta lililokuwa limebeba lita 38,000 lilianguka, yakaibwa mafuta yaliyosababisha moto, ambao ulisababisha maafa makubwa kwa watu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
    Hatujui kama uzembe ndio uliosababisha ajali hiyo, tunachojua ni kwamba uchu wa baadhi ya wakazi wa eneo hilo kutaka kupata fedha kwa njia za mkato, ndio uliochangia ukubwa wa maafa hayo.
    Tatizo hilo linakuzwa na mienendo au tabia inayoendelea kukua ya baadhi yetu kukimbilia maeneo ya ajali bila kuchukua hadhari na wengine kufanya uhalifu, ukiwamo wizi, uporaji au udokozi.
    Ni mwenendo huo hasi ambao umetusukuma leo tuone ulazima wa kukemea na kuiambia jamii iwe makini kila zinapotokea ajali.
    Ipo mifano lukuki ya ajali za malori ya mafuta zilizotokea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha maafa makubwa kama yale yaliyotokea hapa jijini mwishoni mwa wiki. Moja ya ajali zitakazokumbukwa kwa muda mrefu ni ile iliyotokea mkoani Mbeya miaka kadhaa iliyopita, ambako watu 42 waliungua vibaya wakati wakiiba mafuta kutoka kwenye lori lililoanguka katika Kijiji cha Idweli, wilayani Rungwe.
    Tukio hilo liliandika historia mbaya kwa nchi yetu kutokana na kuua watu wengi ambao waliungua vibaya kiasi cha kutotambuliwa kirahisi, hivyo kuilazimisha Serikali kuwazika katika kaburi la pamoja.
    Ni vigumu kusahau pia tukio la miaka michache iliyopita, ambapo watu walivamia lori lililoanguka Barabara ya Mandela, Dar es Salaam likiwa na shehena ya dawa ya kutengeneza sabuni na kuanza kuichota wakidhani yalikuwa mafuta ya kula.
    Bila hadhari yoyote, watu hao walijaza vyombo vyao kabla ya kuondolewa na polisi baada ya kuelezwa kuwa yale hayakuwa mafuta ya kula, bali dawa za kutengeneza sabuni, ambazo hazikuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
    Katika tukio la Mbagala juzi, madereva wa pikipiki na watu wengine walikaidi amri ya kutokaribia eneo la ajali, wakaanza kufungua betri za lori hilo, huku wengine wakikinga mafuta ambayo yalikuwa yakivuja.
    Wapo waliohamisha madumu ya petroli na kwenda kuyaficha kwenye nyumba za jirani na eneo hilo.
    Matokeo yake, mali nyingi zikiwamo baa, nyumba ya kulala wageni, pikipiki, magari na maduka viliungua muda mfupi baada ya lori hilo kulipuka kwa kishindo kikubwa, mithili ya bomu.
    Sisi tunasema tukio hilo na mengine mengi yaliyotangulia ni fundisho kwamba uhalifu kwenye maeneo ya ajali ni janga linaloisumbua jamii yetu, jambo ambalo halikubaliki.
    Wizi wa mafuta kwenye malori barabarani unaofanywa na vijana lazima ukomeshwe, kwani pamoja na umaskini walionao wananchi kutafuta kipato kwa njia haramu ni jambo lisilokubalika hata kidogo.
    Nguvukazi muhimu katika ujenzi wa uchumi ndiyo inayopotea. Yafaa Serikali ichukue hatua sasa.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.